Sunday, 5 December 2010

jana stori

Mansoor awataka wakulima kuzikabili changamoto



Na Ali Mohamed, Maelezo



WAZIRI wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid, amesema kilimo ni sekta yenye umuhimu mkubwa lakini inakabiliwa na changamoto kadhaa.



Waziri huyo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wanakikundi wa skuli ya wakulima wa migomba huko Chukwani wilaya ya Magharibi Unguja.



Alisema kazi ya kilimo inakabiliwa na changamoto nyingi lakini ndiyo yenye umuhimu kwa maisha ya binadamu kwani hujitosheleza kwa chakula kupitia sekta hiyo.



"Kilimo ni kazi iliyotukuka zaidi miongoni mwa kazi nyengine kwa sababu ni kazi inayotumainiwa na kila binadamu kwa chakula hivyo wakulima kuweni wavumilivu na wastahamilivu mambo mazuri yanakuja", alisema Waziri huyo.



Alifahamisha kuwa kwa mujibu wa maagizo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, sekta ya kilimo inapaswa kupewa kipaumbele zaidi katika sera ya mapinduzi ya kijani na upatikanaji wa chakula cha kutosha.



Mansoor aliwaahidi wakulima kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili kwa kuhakikisha upatikanaji wa zana za kilimo, mbegu za kisasa, mbolea pamoja na kuzipitia sheria hasa za kuwadhibiti wahalifu wa mazao.



Awali wanakikundi hicho walimlalamikia Waziri Mansoor juu ya kuwepo tatizo na wizi wa mazao unaofanya na baadhi ya watu ambapo umekuwa ni tatizo kwa maendeleo yao.



Akiambatana na Maafisa wa Programu za kuimarisha huduma za kilimo na sekta ya kuendeleza mifugo (ASSP na ASDPL), Waziri Mansoor alitembelea shamba la migomba Chukwani na Buyu pamoja na kitengo cha kulinda mimea Mwanakwerekwe.

No comments:

Post a Comment