Friday 10 December 2010

MSHITAKIWA WIZI WA BASKELI ANYIMWA DHAMANA.

Mshitakiwa wizi baiskeli anyimwa dhamana



Na Khamis Amani
Jumatano 8 Disemba 2010

MAHAKAMA ya Mwanzo Mwanakwerekwe, imemnyima dhamana na kumpeleka rumande kwa muda wa siku 14, kijana mmoja anayeshitakiwa kwa wizi wa baiskeli yenye makisio ya thamani ya shilingi 65,000.

Mahakama hiyo iliyo chini ya hakimu Ndame Ali Mkanga, imechukuwa uwamuzi huo baada ya mshitakiwa huyo kushindwa kuwasilisha wadhamini mahakamani hapo.

Mtuhumiwa huyo ni Hassan Bakari Mohammed (22) mkaazi wa Nyerere wilaya ya Mjini Unguja, ambaye pamoja na kushindwa kuwasilisha wadhamini hao, lakini aliiomba mahakama hiyo impatie dhamana.

Kabla ya maamuzi hayo ya mahakama, Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Koplo wa Polisi Hassan Mussa Mshamba, alimsomea mshitakiwa huyo shitaka hilo la wizi chini ya kifungu cha 267 (1) na 274 (1) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, ambalo alilikana.

Katika madai yake, Mwendesha Mashitaka huyo alidai kuwa Disemba Mosi mwaka huu, majira ya saa 8:30 za mchana huko Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi Unguja, aliiba baiskeli moja aina ya Sport Sehewa.

Alifahamisha kuwa, baiskeli hiyo yenye rangi nyeusi ina thamani ya shilingi 65,000 kwa kukisia, mali ya Suleiman Mohammed Salum.

Pamoja na kukana shitaka hilo, upande wa mashitaka ulidai upo tayari kuthibitisha kosa hilo, kwa madai upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba ipangiwe tarehe ya kusikilizwa pamoja na kutolewa kwa hati za wito kwa mashahidi.

Hakimu Ndame Ali Mkanga, alikubaliana na hoja hizo aliliahirisha shauri hilo hadi Disemba 22 mwaka huu kwa kusikilizwa, na kuuamuru upande huo wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

No comments:

Post a Comment