Dk. Shein: Ahadi zote zilizotolewa kwenye kampeni zitatekelezwa
• Asema Zanzibar imegeuka chuo cha demokrasia
• Ashukuru na kuwataka WanaCCM kuimarisha chama
• Awatoa hofu kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Jumapili 12 Disemba 2010
Na Rajab Mkasaba
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewashukuru WanaCCM na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kumchagua yeye na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuiongoza Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Aidha, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi wa haki, amani na utulivu mkubwa ulioonesha kupevuka kwao kidemokrasia ambao umeipa heshima kubwa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.
Dk. Shein ambaye katika ziara hiyo alifuatana na mkewe Mama Mwanamwema Shein, aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Viongozi wa CCM, Jumuiya za CCM na Wazee wa CCM wa ngazi ya Tawi, Wadi na Jimbo.
Ikiwa ni siku yake ya awali ya kufanya ziara katika Wilaya zote kumi za Zanzibar Dk. Shein alianza Makunduchi Wilaya ya Kusini na hatimae alizungumza huko Dunga Wilaya ya Kati na kueleza madhumuni ya ziara hiyo ikiwa ni kutoa shukurani kwa wananchi na wanaCCM kwa kufanya uchaguzi kwa salama na amani sambamba na amani na utulivu.
Alitoa pongezi kwa Mkoa huo wa Kusini kufanya vizuri katika uchaguzi Mkuu uliopita kwa kuendeleza historia ya ushindi na kuwapongeza kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yao ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita.
Dk. Shein aliwapongeza Wazanzibari wote kwa kushiriki katika uchaguzi kwa amani na utulivu na kueleza kuwa kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kutekeleza ahadi na kuimarisha maendeleo.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba anayoiongoza yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa itafanya kazi vizuri na ataisimamia vyema bila ya hofu katika kutekeleza majukumu yake na atatenda haki kwa Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti ya itikadi za kisiasa.
Alieleza kuwa asilimia ya ushindi iliyopatikana katika Mkoa wa Kusini Unguja ni kubwa na imeweza kuthibitisha wazi kuwa Mkoa huo ndio ngome ya CCM.”Hiyo ndio sifa ya CCM ya kuahidi na kufanya” alisema Dk.Shein.
Dk. Shein alieleza kuwa nia ni kuona ahadi zote alizozitoa wakati wa Kampeni za uchaguzi uliopita zinafanikiwa ikiwa ni pamoja na kupata maendeleo na kuahidi kuwawezesha akina mama kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi na kusema kuwa lengo lipo vile vile la kuanzisha Benki ya Wanawake.
Alieleza kuwa aliahidi kutekeleza kampeni kwa ustaarabu yeye na viongozi wenziwe na ndivyo ilivyofanyika hatua ambayo imeipelekea Zanzibar kupata sifa ndani na nje ambayo ilipelekea uchaguzi uwe wa amani na utulivu. Pia Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote walioshiriki kwa njia zote katika kufanya kampeni zilizoipa ushindi CCM.
Alisema kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yanabeba umuhimu mkubwa kwa wananchi kwa kuwawezesha kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuweza kuimarisha maendeleo katika sekta zote zikiwemo elimu, afya, huduma muhimu ikiwemo maji safi na salama na nyenginezo kazi ambayo itaendelea kuimarishwa.
Dk. Shein alieleza kuwa ahadi yake ya kuimarisha sekta ya michezo na kuwajengea mazingira mazuri wasanii wa vikundi vyote kwa kuwajengea studio ya kisasa lipo pale pale.
Pia, Dk. Shein alitoa wito kwa wanaCCM kushirikiana na kuwa kitu kimoja ili kuweza kukiimarisha Chama na kueleza kuwa ana imani kuwa kundi lililopo hivi sasa ni kundi la CCM.
Alieleza kuwa chama chake kitaendelea kufuata Katiba na Sheria za nchi katika mfumo mzima wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambayo itaendelea kuwepo sambamba na nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dk. Shein alitawaka wanaCCM kutoa kuwa na hofu na kuwaelezwa kuwa ipo kikatiba kwa kutekelezwa matakwa ya wananchi wa Zanzibar na si maslahi ya mtu binafsi au kiongozi fulani.
Alisema akiwa Rais aliyechaguliwa na wananchi atatekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha maslahi ya wananchi yanalindwa na kutekelezwa na si vinginevyo na kiongozi yoyote aliyepewa madaraka akayatumia kinyume hatokuwa pamoja nae.
Nae Mama Mwanamwema alitoa salamu zake za pongezi na shukurani kwa WanaCCM wa Mkoa wa Kusini kwa kuweza kumuunga mkono Dk Shein na kuwashukuru kwa kutimiza ahadi zao kwa vitendo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Ferouz, nae alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kufanya kampeni ambazo hatimae CCM imepata ushindi mkubwa sana katika ushindi wa Majimbo kwa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.
Alisifu juhudi za Dk. Shein alizochukua mchana na usiku, ambazo zimeweza kuleta ushindi mkubwa, na kumpongeza kwa niaba ya wanaCCM kwa umakini na busara kubwa aliyofanya ya kuunda Baraza la Mawaziri.
Nao wanaCCM wa Wilaya ya Kusini Unguja walieleza kutekeleza ahadi yao ya Wadi zote 11 na Majimbo mawili kuwa yatachukuliwa na CCM ahadi ambayo waliitoa wakati Dk. Shein alipofika Wilayani humo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita na kueleza kuwa Mkoa wa Kusini ni Ngome ya CCM.
Wametoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuunda Baraza zuri la Mawaziri na kueleza kufarajika kwao na Baraza hil la Mawaziri na kujenga matumaini makubwa ya kuweza kupata maendeleo zaidi.
Mapema Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mashirikiano makubwa waliompa na hatimae CCM kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliopita.
Dk.Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar katika ukumbi wa ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui mjini Unguja.
Alisema kuwa kuzungumza na wazee ni utamaduni na heshima ya CCM kwa kutambua umuhimu wa wazee ikiwa ni pamoja na kupata busara zao.
Dk. Shein alitoa shukurani kwa wazee hao na kueleza kuwa juhudi zao zimeweza kuzaa matunda na hatimae chama cha CCM kuweza kupata ushindi pamoja na kuendeleza amani na utulivu iliyopo nchini.
Aidha, Dk. Shein aliwahakikishia wazee hao kuwa ataendelea kufanya kazi nao ikiwa ni pamoja na kupokea busara, hekima na ushauri wao ili kuweza kuimarisha chama pamoja na kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.
Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa wito kwa wazee hao kuendelea kufanya kazi kwa pamoja, kuendeleza mashirikiano kwa lengo la kufuata nyayo za chama cha ASP za umoja na mashirikiano.
Alieleza imani yake kuwa wazee hao wataendelea kushirikiana kwa pamoja ili kukiimarisha chama na kuweza kuwasaidia viongozi wao pamoja na kuweza kuwapa nguvu vijana kufanya kazi zao vizuri.
Nao wazee walieleza matumaini yao kwa Dk. Shein kuwa atakuwa mtendaji bora zaidi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuwa muumini mzuri wa kuendeleza Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.
Wazee hao walimpongeza Dk. Shein kwa ushindi alioupata katika uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment