Saturday 11 December 2010

WATAKA UBAGUZI WA KIUCHUMI UONDOSHWE.

Wataka ubaguzi wa kiuchumi uondoshwe

Na Mwantanga Ame
Jumapili 12 Disemba 2010

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeshauriwa kuzifuta sheria zinazoonekana kuleta ubaguzi kwenye nyaja ya uchumi, ili kukuza pato la taifa pamoja na maisha katika jamii.

Mwanasheria wa kujitegemea Awadh Said, alieleza hayo alipokuwa akichangia kwenye kongamano la siku moja la kuadhimisha siku ya haki za Binadamu, lililofanyika Ukumbi wa EACROTANAL Mjini Zanzibar.

Alisema kama serikali imekubali kufuata haki za binadamu lazima iondoshe ubaguzi kwenye eneo la kiuchumi hasa katika kilimo, masoko na masuala ya kijamii.

Mwanasheria huyo alitoa mfano wa zao la karafuu ambalo alisema liko chini ya usimamizi wa serikali huku wakulima wakiwa wanapangiwa bei, sehemu ya kuuzia ambapo wakulima wengine wakiwa wako huru kuuza kwa bei na mahali wanapotaka.

Alisema huo ni aina ya ubaguzi wa kiuchumi kwa vile umekuwa ukiwapa haki wakulima wa mazao mengine kufanya watakavyo huku wakulima wa zao la karafuu wakibanwa.

Alisema kama serikali imefikia hatua ya kupinga ubaguzi lazima suala la wakulima wa karafuu nalo liwekwe wazi kusiwe na ubaguzi.

“Inashangaza mazao yote ya wakulima wamekuwa wakiachiwa kijipangia na kuuza kwa bei wazitakazo, lakini zao la karafuu bado linaendelea kubanwa kwa kufanywa na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) pekee”, alisema Awadh.

Alisema kuendelea kuweka zao hilo kufanywa na ZSTC, ni sawa na ubaguzi unaonyima utoaji wa Haki za binadamu kiuchumi na ni lazima serikali iliangalie.

"Sheria ya karafuu inambagua mkulima kwani imewekewa mipaka huku wakulima wengine wanaachiwa kuuza bidhaa zao watakavyo" alisisitiza.

Aidha, Mwanasheria huyo alisema ili kilimo hicho kiweze kuwa na tija ni vyema kwa serikali ikauangalia upya uamuzi wa kuendelea kulisimamia zao hilo kwani ubaguzi wa kilimo hautaweza kuleta maendeleo katika kukuza pato la taifa.

Nao washiriki wengine kwenye kongamano hilo, walisema ipo haja ya usimamizi wa sheria za kazi, usalama barabarani na maslahi ya wafanyakazi ni mambo ya msingi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi Zanzibar.

Mmoja wa wachangiaji hao Mohammed Yussuf ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Utafiti (ZIPPOR), alisema, Zanzibar inapaswa kujivunia kutokana na kuongezeka kwa utawala bora ikilinganishwa na miaka ya nyuma, lakini ipo haja serikali ikalisimamia tatizo la rushwa na wizi wa fedha za serikali.

Alisema baadhi ya watumishi wamekuwa kero kwa jamii kutokana na kuiibia serikali kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo linadhoofisha uchumi wa nchi.

Nae Amrani Umbaya Vuai, alisema kuwepo kwa ongezeko la usafiri wa magari serikali inapaswa kuanza kufikiria mkakati utaoutumika kupunguza ajali kwani tayari kumekuwa na madereva wanaogonga watu ovyo na kisha kukimbia huku wakiacha familia nyingi kuwa mayatima.

Nae Profesa Chris Peter Maina, alisema ipo haja ya kuangaliwa kwa sheria ya ukaazi kwani wanawake wanaoolewa huzuiliwa kupiga kura eneo ambalo mume wake anaishi huku mume huyo akiachwa huru kuchagua kupiga kura kwenye nyumba yeyote anayoamkia ikiwa ana zaidi ya mke mmoja.

Alisema hali hiyo inamnyima uhuru mwanamke hilo ni lazima liangaliwe kwa vile bado limekuwa halimpi haki mwanamke huku likimuacha mwanamme huyo kupiga kura apatakapo haki ambayo ilitakiwa iwe kwa wote.

No comments:

Post a Comment