Monday, 6 December 2010

SERIKALI KUWAPA KIPAUMBELE WALEMAVU

Serikali kuwapa kipaumbele walemavu


Na Luluwa Salum,TSJ


Jumapili5 Disemba 2010


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeahidi kuwapa kipau mbele watu wenye ulemavu kwa kuwapatia nafasi za uongozi pamoja na vyombo vya utoaji maamuzi.

Akihutubia katika maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani huko katika uwanja wa michezo Gombani, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa watu wenye ulemavu.

Waziri huyo alisema kutokana na hali hiyo, itahakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika mambo yote yanayohusu.

Alisema ni vyema kuondokana na dhana ya kuwa watu wenye ulemavu hawawezi kufanya kazi ambapo dhana hiyo inachangia hali duni ya maisha yao, hivyo ni lazima dhana hiyo iondoke vichwani mwa watu.

Alifahamisha kuwa kutokana na kuwajali watu wenye ulemavu serikali imeunda Baraza la Taifa la watu wenye Ulemavu na Idara yake, ili kuweza kufikisha matatizo yao na kuweza kufanyiwa kazi.

Kwa upande wao watu wenye Walemavu walisema wanahitaji kupewa upendo wao na jamaa zao,na kupatiwa mambo yote muhimu yanayohitajika katika maisha ya kila siku na wanahitaji kushirikishwa katika mambo mbali mbali ili kujikwamua katika umaskini.

Walisema Baraza la Taifa la watu wenye Ulemavu linakabiliwa na changamoto mbali mbali ikwa ni ukosefu wa fedha ambazo kwa kiasi kikubwa zinakwamisha shughuli za kiutendaji za Baraza hilo sambamba na kupatiwa vitendea kazi.

Maadhimisho ya watu wenye Ulemavu huadhimishwa kila ifikapo Disemba 3 ambapo mwaka huu Kitaifa yamefanyika Kisiwani Pemba, yakibeba ujumbe usemao ‘Timiza Ahadi ya Ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu katika kufikia malengo ya Melenia’.

No comments:

Post a Comment