Tuesday 7 December 2010

DK. BILAL AITOA HOFU MAHAKAMA MATUMIZI IT

Dk. Bilal aitoa hofu Mahakama matumizi IT



Said Ameir Dar es Salaam
Jumanne 7 Disemba 2010

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal amesema kuwa Idara ya Mahakama inakabiliwa na changamoto ya kuongeza na kuimarisha matumizi ya tekinolojia ya habari.

Alisema katika kipindi hicho ambacho matumizi ya tekinolojia ya habari yameingia katika kila sehemu ya maisha ya kikazi na binafsi, Idara hiyo nayo inapaswa kujipanga ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yake na kufikia malengo.

Makamu wa Rais, alisema hayo jana jijini Dar es Saalam, wakati alipokuwa akizindua rasmi Mfumo wa kurekodi mashauri Mahakamani kwa njia ya Kompyuta pamoja na kuzindua tovuti ya mahakama.

Dk. Bilal alisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya habari katika shughuli za mahakama na kueleza kuwa matumizi hayo hurahisisha uendeshaji wa kesi.

Dk. Bilal aliutaka uongozi wa Idara ya mahakama nchini, kufanya jitihada za kusambaza matumizi hayo ya tekinolojia ya habari katika Ofisi za mahakama nchini kote badala ya kuishia katika Ofisi za Mahakama Kuu Dar es salaam na vitengo vyake.

Mradi wa kuweka mfumo wa kurekodi mashauri mahakamani kwa kompyuta pamoja na uanzishwaji wa tovuti ya mahakama unafadhiliwa na Taasisi ya uendelezaji wa mazingira mazuri kwa uwekezaji Afrika-Investment Climate Facility for Africa-ICF.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya tovuti aliyoizindua Makamu wa Rais, alisema itakuwa vyema kuwa Idara ya Mahakama itafikiria kuondoa tovuti hiyo kutoka kuwa sehemu ya kupata habari(informative website) hadi kuwa tovuti ya upashaji habari (interactive website) ambapo wadau watapata fursa ya kuwasiliana na mahakama bila ya kuathiri Uhuru wa chombo(judiciary independence).

Kwa upande wake Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, alisema mbali ya kueleza furaha yake ya kuona kuwa hatimae mradi huo umeanza, alieleza changamoto mbali mbali zinazoukabili madi huo

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na namna ya kuwafanya majaji wauamini mfumo huo na kuukubali,kusambaza mfumo huo katika Ofisi za mahakama nyingine kote nchini, kuandaa kada mpya ya watumishi mahiri katika kurekodi mashauri na utoaji habari za mahakama.

Changamoto nyingine ni Ofisi za kuwekea miundombinu ya mfumo huo ambapo alibainisha kuwa Ofisi nyingi za mahakama hazikujengwa kurahisisha uwekaji wa miundombinu ya mfumo wa tekinolojia ya habari.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani, Jaji Kiongozi Fakih Jundu, majaji wa mahakama ya Rufaa na wa Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama ya Rufaa Francis Mutungi,Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Oliver Mhaiki na watumishi wengine wa mahakama kuu, Mtendaji Mkuu wa ICF Bwana Omari Issa.

No comments:

Post a Comment