Saturday 11 December 2010

KILI STARS, IVORY COST ZAWANIA DOLA 30,000

 Kili Stars, Ivory Coast zawania dola 30,000

Na Mwandishi Wetu
Jumapili 12 Disemba 2010

BAADA ya kuzifunga timu za Ethiopia na Uganda katika michezo ya robo fainali juzi, timu za taifa za Tanzania Bara na Ivory Coast, leo zinajitupa katika uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam, kuwania taji la ubingwa wa michuano ya Chalenji.

Kabla kutinga hatua hiyo, Ivory Coast iliichapa Ethiopia mabao 2-1 katika nusu fainali, huku Kilimanjaro Stars ikiitoa jasho Uganda kwa dakika 120 kabla kuibuka na ushindi wa mabao 5-4 kwa changamoto ya mikwaju ya penelti.

Uganda ndio iliyokuwa ikiushikilia ubingwa huo kwa miaka mitatu na hivyo kubakisha kikombe cha zamani katika himaya yake.

Licha ya kupambana na moja kati ya timu vigogo barani Afrika, Kilimanjaro Stars inapewa nafasi kubwa kushinda leo, hasa kutokana na uwezo ilioonesha katika michezo iliyopita ambapo ngome yake imeruhusu kufungwa bao moja tu muda wa dakika 90 za michezo minne iliyocheza.

Ingawa Stars ilianza kwa kipigo cha bao 1-0 mbele ya Zambia katika mchezo wake wa kwanza, lakini ilionesha kuimarika hatua kwa hatua, hali inayowapa matumaini Watanzania kushuhudia ikifuta aibu ya kukosa mataji kwa miaka mingi sasa.

Kocha Jan Poulsen anatarajiwa kuwapanga nyota wake wote muhimu kuanza kusaka ushindi mapema akiwemo Mrisho Ngassa, John Boko, Nurdin Bakari, Shadrack Nsajigwa, Juma Nyoso, huku mlangoni kama kawaida akiwekwa Juma Kaseja ambaye alipangua penelti moja na kuipeleka timu hiyo katika fainali kwenye mchezo dhidi ya Uganda.

Hata hivyo, pamoja na kucheza kwenye uwanja wa nyumbani wakishajiishwa na maelfu ya mashabiki wake, lakini Stars itakuwa ikikabiliana na upinzani mkali kwani Ivory Coast si timu ya kubeza kwani ina uwezo wa kufuta ndoto za Watanzania kubakisha taji hilo kama haitakuwa makini.

Kimsingi Tanzania imeshatwaa kombe la Chalenji kwa kuwa inacheza na timu mwalikwa, ambayo hata kama itashinda, itakabidhiwa zawadi ya fedha bila kikombe, lakini kuibuka na ushindi ni kitu muhimu kitakachowapa faraja Watanzania.

Pambano hilo litatanguliwa na lile la kutafuta mshindi watatu ambalo litazikutanisha timu za Ethiopia na Uganda zilizopoteza michezo ya nusu fainali.

No comments:

Post a Comment