Friday, 30 April 2010

Dk.Karume na Balozi Alfonso E. Lenhardt

RAIS wa Zanzibar na Mwnyekiti wa Baraza la Mapinduzi Amani Abeid Karume akizungumza na balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso E. Lenhardt  aliyefika Ikulu mjini Zanzibar.

Huduma za sheria wapokea kesi 229 za udhalilishaji

Na Halima Abdalla
ZAIDI ya kesi 229 ya udhalilishaji wa wanawake na watoto zimeripotiwa katika kituo cha huduma za sheria Zanzibar (ZLSC), mwaka 2009.


Kati ya kesi hizo, udhalilishaji wa wanawake majumbani zilizoripotiwa kwenye kituo hicho ni 93 kwa Unguja na Pemba.


Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kituo cha huduma za sheria Zanzibar, Is-shak Ismail Sharif, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema katika mwaka huo, kesi zinazohusiana na udhalilishaji wa watoto zilizoripotiwa kituoni ni 57 na kesi zilizoripotiwa kwa wasaidizi wa kisheria Unguja ni 50 kwa upande wa Unguja. huku wasaidizi wa Pemba wakiripotiwa kesi 29.

Is-shak alisema kesi hizi zilizoripotiwa za watoto zinahusiana na unyanyasaji wa watoto, ubakaji, kuingiliwa kinyume na maumbile pamoja na aina nyenginezo za udhalilishaji.


Alisema kesi hizi za udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa mwaka uliopita zimeonekana kuongezeka ikilinganishwa na mwaka 2008 ambazo zilikuwa chini ya hapo.


Alifahamisha mara nyingi malalamiko hayo yanapofika kituoni hapo, huwasilishwa polisi ambapo huingilia kwa kuzikwamua pale zinapokwama.

Aidha, alisema ikitokea kesi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa njia ya mauaji huwa wanaipeleka moja kwa moja katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka.


''Kama kesi ya mauaji huwa tunaipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka", alisema Mkurugenzi huyo.


Aidha Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa jamii kuachana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto kwani kufanya hivyo ni kinyume na haki za binadamu.

Makunduchi sekondari kuadhimisha miaka 100

Na Ali Mohamed, Maelezo
SKULI ya Sekondari Makunduchi inatarajia kufanya sherehe za kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa kwake pamoja na miaka 20 ya urafiki na skuli ya Stone Comprehension ya Uingereza.

Akizungumza na wanakamati ya skuli hiyo na wanafunzi, Katibu wa kamati hiyo, Haji Simba Hassan amesema sherehe hizo zitafanyika mapema Julai, 2010.

Alisema maadhimisho hayo ni sehemu muhimu ya kukumbuka historia refu ya skuli hiyo na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mikaa 100.

Mwenyekiti huyo aliwataka watu waliosoma skuli hiyo kushiriki kikamilifu katika sherehe hizo ili ziweze kupata ufanisi mkubwa.

Aidha, katika maelezo yake, Katibu huyo hakuainisha nani ataongoza maadhimisho hayo ya kihistoria.
 
Wakati huo huo, Katibu Haji Simba Hassan, alisema skuli hiyo ina mpango wa kuyatengeneza upya mabanda ya skuli yaliyochakaa kwa kujengea mazingira mazuri wanafunzi.

Alisema katika mpango huo wa ujenzi, zaidi ya shilingi milioni 100 zinatarajiwa kutumika ambapo amewataka wote waliosoma katika skuli hiyo kuchangia kwa hali na mali.

Skuli ya Sekondari Makunduchi ni miongoni mwa skuli za muda mrefu kujengwa katika Mkoa wa Kusini ambapo watu wengi wakiwemo viongozi wa ngazi za juu serikalini walisoma skuli hiyo.

Mradi wa usambazaji waya wa umeme watiwa saini Ikulu

Na Mwanajuma Abdi

TAASISI ya Millennium Challenge Account ya Tanzania (MCA-T) imetilia saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa utengezaji wa utandazaji waya wa pili wa kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar na kampuni ya VISCAS ya Japan utaogharimu dola za Marekani 28,210,400.

Sherehe hizo zilifanyika jana, Ikulu mjini hapa, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso E. Lenhardt walishuhudia.

Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha aliwaongoza Mawaziri na watendaji wengine wa SMZ, katika kushuhudia hafla hiyo adhimu kwa wananchi wa Zanzibar.

Wengine waliohudhuria ni Mkurugenzi Mkaazi wa MCC, viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, pamoja na Maofisa wa MCC, MCA-T, TANESCO, ZECO na wawakilishi kutoka kampuni ya ESB International ya Ireland.

Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Marekani na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pia nayo inachangia dola milioni 3.1, katika kufanikisha mradi huo kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCA-T, Bernard Mchomvu alisaini kwa niaba ya Tanzania na Tetsuji Ohno ameiwakilisha Kampuni ya VISCAS- Japan, ambao utatumia dola za Marekani 28,210,400 hadi kukamilika kwake Disemba 2012.

Akizungumza mara ya utiaji wa Saini huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania wa Millennium Challenge Account, Bernard Mchomvu, alisema mradi huo ni muhimu katika kukuza uchumi na kupambana na umasikini nchini.

Aliongeza kusema kwamba MCA-T imekuwa ikifanya kazi pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanzania katika kusimamia miradi ya Shirika la Changamoto la Millenia (MCC) inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani, ambapo jumla ya Dola za Marekani 698.1 zimetolewa na Serikali ya Marekani kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, usafirishaji wa maji safi na ujenzi wa waya wa pili wa umeme kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo na kukuza uchumi wa nchi ili kuweza kupambana na umasikini.

Nae Mwakilishi wa Kampuni ya VISCAS, Tetsuji Ohno alieleza utiaji wa saini wa mkataba huo umefungua hostoria mpya kwa kampuni yake katika Bara la Afrika kwa nchi ya Tanzania, Zanzibar kushinda zabuni ya ujenzi wa kuweka waya wa pili utaokuwa na megawati 100, ambao utakuwa na nguvu zaidi katika upatikanaji wa huduma hiyo ya uhakika Zanzibar.

Alieleza mradi huo utasaidia kuimarisha mfumo mzuri wa biashara, sambamba na kukuza uchumi na kujenga mustakabali mzuri wa maendeleo ya baadae kwa nchi na wananchi kwa ujumla.

Nae Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso E. Lenhardt aliongeza kusema kwamba, sherehe za utiaji wa saini huo ni kuongezea nguvu huduma ya umeme utaosafirishwa kutoka Tanzania Bara hadi Unguja kwa kufikia megawait 100 na utagharimu Dola za Marekani milioni 28.

Alifahamisha kuwa, mradi huo ni muendelezo wa miradi mbali mbali inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia kwa Shirika lake la Changamoto (MCC), tokea mwaka 2008 ilipasainiwa kufanya kazi nchini, ambapo jumla ya Dola za Marekani milioni 698.1 imeshasaidia kwa nchi ya Tanzania.

Alifafanua kuwa, Taasisi MCC imesaidia katika uwekaji wa miuondombinu ya maji, barabara, afya na umemem ili kuwa na nguvu zaidi katika matumizi katika skuli na biashara, ambayo hayo yote yanafanyika kwa ajili ya kukuza uchumi.

Aidha alitoa salamu za watu wa Marekani na Rais wao Obama kuwa wanajivunia kusaidia mradi huo wa umeme Zanzibar katika kuongezea nguvu zaidi.

Alisema kuongezewa nguvu kwa waya wa umeme utasaidia kuweka sera nzuri za mazingira ya watu binafsi kuwekeza nchini.


Mkurugenzi Mtendaji wa MCA-T, Bernard Mchomvu (kulia), akisaini mradi wa utengenezaji waya wa umeme kwa niaba ya Tanzania na Tetsuji Ohno anayeiwakilisha Kampuni ya VISCAS- Japan, mradi huo utatumia dola za Marekani 28,210,400 hadi kukamilika kwake Disemba 2012.(Picha na Othman Maulid).

Dk. Karume mgeni rasmi kilele cha Mei day

Na Ramadhan Makame
WAFANYAKAZI wa Zanzibar, kesho wanaungana na wafanyakazi wenzao kusherehekea siku ya wafanyakazi duniani Mei mosi.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), limeeleza kuwa sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika hoteli ya Bwawani iliyopo mjini hapa.

Shirikisho hilo, lilieleza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za leo.

Sherehe hizo zitaanza kwa maandamano ya wafanyakazi wa taasisi mbali mbali yatakayoanzia viwanja vya Malindi na kuelekea hoteli ya Bwawani.

Siku ya wafanyakazi duniani huwapa fursa wafanyakazi kujitathmini kwa kuangalia utendaji wao kwa maendeleo yao na taifa.

Ujumbe wa mwaka huu wa sherehe za wafanyakazi, ‘uchaguzi mkuu usaidie kuboresha maslahi na ushirikishwaji wa wafanyakazi’.

Mawaziri

MAWAZIRI wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waliofika Ikulu mjini Zanzibar jana kwenye ghafla ya utiaji saini wa utengenezaji wa waya mpya wa kusambazia umeme.(Picha na Othman Maulid).


Tubadilishene hati

Mkurugenzi Mtendaji wa MCA-T, Bernard Mchomvu  (kulia), akibadilishana hati na muwakilishi wa kampuni ya VISCAS ya Japan,  Tetsuji Ohno, baada ya kusainiwa mkataba wa utengenezaji wa waya wa kusambazia umeme. (Picha na Othman Maulid). 

Kaimu hebu tueleze

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (ZECO), akizungumza na waandishi wa habari baada ya utiaji saini utengenezaji wa waya mpya wa kutoa umeme Tanzania bara hadi Zanzibar.(Picha na Othman Maulid).

Thursday, 29 April 2010

Uchambuzi wetu

Usikurupuke kuwania Urais
Na Ramadhan Makame
HUU ni mwaka wenye matukio yenye kusubiriwa kwa hamu, nikisema hivyo kila mmoja atakuwa analo lake lililomkaa kichwani.

Kwa upande wa wanamichezo hasa soka akili zao zitajikita kwenye fainali za kombe la dunia ambazo kwa mara ya kwanza zitapigwa barani Afrika, kule nchini Afrika Kusini.

Lakini kwa upande wa wanasiasa wao hasa Tanzania na Zanzibar, akili na fikra zao ni juu ya uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Naam! hayo ni matukio makubwa na kila moja lina msisimko wa aina yake, lakini kwenye waraka huu mfupi acha tuogelee japo kidogo kwenye siasa hasa tuwazungumzie wale wanaojiita wana nia za kugombea.

Vyama vimepuliza mazumari huku michakato ya kuwapata wagombea ikipita kwenye hatua na njia tofauti baina ya chama kimoja na chengine.

Pamoja na kutofika rasmi wakati wa kampeni lakini ni dhahiri kila anayetaka kugombea kwa wadhifa ambao amejipangia ama kwa hiari au kushawishiwa ameshaanza kampeni.

Hii inaashiria hali ya uchaguzi mkuu mwaka huu utakavyokuwa mgumu sio kwa wale wenye kutetea nafasi zao, bali hata kwa hao wapya wanaojiandaa kuingia kwenye mchezo huo usiotabirika.

Michakato ya vyama hivyo kwangu mimi hainishughulishi wala hainibabaishi, ila kinachonipa shida hao watu watakaoshinda michakato na hatimaye kupewa tiketi za kugombea na vyama vyao.

Najua kwa njia moja ama nyengine na wakitaka wasitake vipo vyama vitakosea kutupatia wagombea wenye kuhitajiwa na wananchi kwa maslahi ya maendeleo yao.

Wagombea wa namna hii watapenya kwa sababu mbali mbali zikiwemo kuonewa huruma na vyama kutokana na pengine michango yao ya kifedha wanayoitoa, pengine uzuri wa ukoo wa mgombea, uzuri wa sura zao, rangi zao, historia zao na kadhalika.

Sidhani kama wakati mwengine ni vyema vikatumika vigezo kama hivyo, nafikiri vyama viwe makini na kuongozwa na sifa moja kuu nayo ni je! mgombea huyu waliyempata anakubalika na wananchi?

Kwa mfano hivi sasa kuna mchakato wa chinichini wa kumtafuta mrithi wa Dk. Amani Abeid Karume atakayewania kiti cha Urais wa Zanzibar.

Katika hili kuna majina kadhaa wa kadhaa kupitia vyama kadhaa wa kadhaa yanatajwa kuwa yatachukua fomu za kuwania kiti hicho.

Ninalotaka kusema mimi ni dogo nalo ni kabla ya mgombea kuchukua fomu ajiulize jamii ya kizanzibari inamuonaje! na sio kufuata mkumbo wa wapambe ambao baada ya uchaguzi ambao hudoea nafasi za bure (political opportunist).

Ni vyema mgombea akajitathmini na kujihakiki vya kutosha kwenye nafsi yake na kujipa jibu sahihi kabla ya kuwauliza watu wenye hekima na busara, chonde chonde mgombea usikurupuke kwenda kuwauliza wapambe.

Katika kujihakiki na kujitathmini huko ni vyema pia ukaliangalia vyema suala zima la imani yako thabiti mbele ya Wazanzibari na jinsi unavyoguswa na maisha yao ya kila siku.

Jiulize pia ulipokuwa kiongozi aidha iwe ngazi ya chini, kati na hata ile ya juu, lipi la kujisifia mbalo wewe binafsi umewahi kuwasidia Wazanzibari sio familia yako wala ukoo wako, kwenye shida zao.

Suali jengine je! umejipima kiwango chako cha ubinafsi ulionao kwenye moyo wako? na ulipokuwa kiongozi wa ngazi yeyote ile hapo awali, Wazanzibari wangapi uliwanyima haki zao huku ukiwa unajua kwa yakini kwamba ile uliyowanyima ni haki yao.

Ningependa pia mgombea ujiulize je! unayajua mahitaji (intrests) ya Wazanzibari katika kipindi hichi na umejiuliza nini wanakitaka na nini hawakitaki na utawasaidia je?

Suala hili ni la msingi kwa maana mahitaji ya Wazanzibari katika miaka ya 1960 ni tofauti sana na kipindi hichi, hofu yangu usijekuwa na mawazo mgando ukadhani Wazanzibari wa miaka ile ndio wale wale na wanahitaji mambo yale yale ya kale.

Kama una mawazo ya aina hiyo utakuwa umekosea sana, mimi nastahiki kukuita wewe ni mvivu wa kufikiri na ni mvivu wa kusoma alama za nyakati ambapo kwa wanasiasa maradhi haya ni ya kawaida.

La mwisho nakukumbusheni wagombea kuwa Wazanzibari wa sasa hawahitaji rais bubu, atakayekuwa anabana midomo kimya sio wa kuongea wa kuwatetea wananchi kwenye dhiki zao mbali mbali.

Tulia mgombea usipandwe na hasira juu ya masuali haya, huu ni waraka niliyoupa jina la muongozo wangu kwa kiongozi ajae, si kwa maslahi yangu bali ya Wazanzibari wote.

Kwa hisia zangu, mgombea yeyote asiyeweza kuyafuata yaliyokuwemo kwenye muongozo huu, ni vyema akajitoa mapema na tena fomu aiogope kama ukoma.

Wakatabahu naomba kutoa hoja!

Karume na viongozi wa BADEA, Saud Fund


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, akisalimiana na viongozi wa BADEA na Saud Fund uliofika Ikulu Mjini Zanzibar kuonana nae jana.(Picha na Ramadhan Othman).

1943 waliambukizwa VVU mwaka jana

Na Jamila Abdallah, Pemba
WAKAAZI wapatao 1934 wa Zanzibar walijitokeza kuchunguzwa damu zao katika vituo vya afya Zanzibar na wamegundulika kuwa na Virusi vinavyosababisha UKIMWI ambao ni miongoni mwa wakaazi 69,749 waliojitokeza kupima virusi vinavyosababisha UKIMWI mwaka jana.

Akitoa takwimu hizo Daktari wa Hospitali ya Chake Chake, na mjumbe wa mradi wa Uzazi wa Mpango na Malezi Bora Tanzania (UMATI ), Ali Shamte, alisema kati ya waliojitokeza kupima kwa hiyari wapo wanawake 33,096 kati yao 1,168 sawa na asilimia 3.5 waligundulikana na virusi vinavyosababisha UKIMWI.

Alisema kwa upande wa wanaume waliojitokeza kupima ni 36,653 sawa na asilimia 2.1 kati yao 756 waligundulikana wameathirika na virusi na 164 waliopima katika vituo tofauti walikataa kutajwa wanapokaa miongoni mwao 10 walikutwa na VVU ambao ni sawa na asilimia 6.1.

Takwimu hizo zilitolewa mara baada ya kumaliza kutoa mada katika mafunzo yaliyotolewa na wajumbe wa mradi wa DARAJA kwa baadhi ya wazazi na walezi,viongozi wa dini ,Masheha na walimu ma Skuli na Madrasa za wilaya ya Chake Chake Pemba.

Mradi huo wa DARAJA una lengo la kujenga mawasiliyano yanayoaminika baina ya mzazi mwema au tegemeo kwa vijana, yaani daraja kwa lengo la kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

Dk. Ali aliendelea kufafanua zaidi kwa kusema DARAJA ni kiunganishi na ni sababu ya kujifunza kuhusu mawasiliano kati ya mzazi mwema na vijana katika afya ya uzazi, kama vile magonjwa ya ngono, VVU, UKIMWI na mimba zisizotegemewa.

Akitaja baadhi ya malengo ya DARAJA Ali Shamte alisema kwanza kujilinda mwenyewe dhidi ya maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa.

Pia DARAJA imedhamiriya kujenga mawasiliano nyeti baina ya mzazi tegemeo na kijana na kuwasaidia vijana kuimarisha malengo binafsi na ndoto za kimaisha pia kubuni mipango ya kutimiza malengo hayo.

Naye mzazi, Saleh Hassan Suleiman, wakati akichangia mada alisema,``jambo kubwa linalosababisha kupanda kasi waathirika wa gonjwa la UKIMWIimwi ni zinaa ambayo inasababishwa na jamii kutofuata maamrisho ya dini zetu”.

Kwa upande wa mzazi wa kike Amina Said Ali alichangiya kwa kusema kuwa akina baba waachane na tabia ya kuwatupia mzigo wa ulezi wazazi wa kike tu bali washirikiane kwa kila hali katika kujenga familia bora na zenye maadili mema.

Amina, pia alisema wazazi kwa wakati huu wanalazimika kuwa wa wazi kwa vijana wao katika kuwapa elimu na kuwaeleza juu ya athari na madhara ya ugonjwa huo na wakae na familia zao na kuwaeleza ukweli juu ya hali ya ukimwi inavyotisha na kuongeza siku hadi siku.

Nungwi walia na mikataba mibovu mahotelini

Na Salum Vuai, Maelezo
WANANCHI wa kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamesema iwapo hatua za haraka kurekebisha mfumo wa ajira katika mahoteli hazitachukuliwa, sekta ya utalii haitakuwa na manufaa yoyote kwao.

Hayo yalielezwa na Sheha wa Shehia ya Nungwi Kombo Haji Mkuni kwa niaba ya wanakijiji hao, kwenye mkutano wa kutambulisha mpango wa kutoa mafunzo yahusuyo njia za kutumia utalii kwa ajili ya kupunguza umasikini mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mpango wa mafunzo hayo uliendeshwa na Jumuia ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), kwa ushirikiano na taasisi inayotoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo Tanzania ya TGT.

Sheha huyo alifahamisha kuwa, kutokana na kutofuatwa sheria na haki katika suala zima la mikataba ya uajiri, matatizo waliyonayo wanakijiji wa huko ya ukosefu wa ajira hayawezi kutatuliwa kirahisi kwa kuwepo utalii.

Alisema kwa inavyoonekana ajira chache wanazopewa wananchi wa hapo zinalenga kuwaonesha tu jinsi ya mahoteli yalivyo, na baada ya miezi michache wengi wao hufukuzwa bila sababu za msingi.

Alifahamisha kuwa mikataba mingi wanayopewa ni ya kulazimishwa kwani imebainika kuwa wengi wa wanakijiji wanaoajiriwa katika baadhi ya Idara zisizohitaji utaalamu mkubwa mahotelini humo, hutakiwa kutia saini katika mikataba bila kujua kinachoelezwa kuhusiana na kile wanachokisaini na kupata tamaa kuwa tayari wameajiriwa.

"Tumebaini kuwa wenye mahoteli wengi ni wadhalilishaji tu, hawazingatii haki za ajira, huajiri wapendavyo na kutimua wafanyakazi wanapojisikia kufanya hivyo na hawana mikataba ya hiari bali ni ya kulazimisha tu", alieleza kwa uchungu.

Kutokana na hali hiyo, Kombo alisema wafanyakazi wengi wanaofungishwa mikataba ya miezi sita huachishwa kazi bila kuambulia chochote na hawawezi kudai kwa kuwa ndani ya mikataba yao ambayo walisaini bila kujua, huoneshwa wazi kuwa ajira zao ni za muda huo.

"Ninapata kesi kama hizi lakini nikiuliza naoneshwa mikataba na kukosa pa kushika, mikataba kama hii si halali kwa kuwa inawafunga na hivyo kukosa haki stahiki pale waajiri wanapochoka nao", alisema.

Kombo alisema katika hali isiyotarajiwa, imewahi kutokezea katika hoteli moja kufukuzwa watu sitini kwa pamoja, akionesha mshangao wake kama wote hao walikuwa na makosa au walitimuliwa kwa utashi wa waajiri.

Alishauri kuwepo mikataba ya pande tatu itakayoshuhudiwa na maofisa wa Kamisheni ya Kazi, waajiri pamoja na mtu anayeajiriwa na nakala zake kugaiwa kwao kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ili kuepusha mchezo mchafu na kuwajengea kiburi waajiri wasiopenda kufuata sheria.

Aidha alitaka kabla kusainiwa kwa mikataba hiyo, wale waombaji kazi wasiojua kusoma wasomewe na kufahamishwa vyema kilicho katika mkataba ili kama wana hoja waulize na kujibiwa.

Katika hatua nyengine, aliushukuru uongozi wa ZATI na TGT kwa kuichagua Nungwi kuwa miongoni mwa vijiji vya kupewa mafunzo ya kazi za amali zinazoweza kuimarisha utalii, na kuwataka wanachama wa vikundi vya akinamama kufanya bidii ili wapige hatua na kujipatia ajira.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa maofisa kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na wakufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii cha Zanzibar kilichopo Maruhubi.

Tuesday, 27 April 2010

Marufuku kuchimba mchanga kwenye fukwe - Mazingira

Mwanajuma Abdi na Maryam Ally (MSJ)
IDARA ya Mazingira Zanzibar imesimamisha uchimbaji wa mchanga wa pwani katika Hoteli ya kitalii ‘Uroa Bay Beach Resort’ iliyopo Uroa Wilaya ya kati Unguja.

Hatua hiyo inafuatia Mkurugenzi wa Mazingira, Ali Juma na watendaji wa Idara walipofanya ziara ya ghafla katika hoteli hiyo na kujionea chungu za mchanga pembezoni mwa fukwe hiyo.

Alimuagiza Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo, Mussa Durio Savio kuwa haruhusiwi kuchimba mchanga katika fukwe kwani kufanya hivyo anaharibu mazingira kukiuka sheria za nchi.

Alisema sheria za nchi haziruhusu kuchimbwa mchanga wa pwani kwa ajili ya kufanya ujenzi katika sehemu nyengine.

Alimueleza kwamba, kuanza jana hawaruhusiwi kuendelea na uchimbaji huo ambapo wakikaidi amri hiyo atawafikisha mahakamani.

Aidha alionya juu ya tabia ya baadhi ya wamiliki wa hoteli kuchimba mchanga kwa ajili ya ujenzi na kuwataka kuacha mara moja.

Alisema fukwe nyingi katika ukanda wa utalii zimekumbwa na mmong’onyoko wa ardhi unaosababishwa na uchimbaji mchanga katika fukwe, ukataji ovyo wa mikoko na kuongezeka kina cha maji ya bahari.

Meneja Mkuu wa hoteli hiyo, Mussa alikiri kuchimba mchanga huo kwa ajili ya kujaza katika maeneo mbali mbali ya Hoteli yake kutokana kujitokeza kwa mashimo yanayosababishwa na mawimbi ya maji ya bahari yanayopiga kwa kasi kubwa.

Alisema wamelazimika kujenga ukuta ili kusaidia hali hiyo, ambayo inayojitokeza kutokana na mawimbi ya maji ya bahari yanapojaa.

Aidha alifafanua kuwa, hoteli hiyo haijaanza kazi rasmi, ambapo wanategemea kuifungua Julai mwaka huu katika msimu wa utalii.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Mkurugenzi wa Mazingira Ali Juma, alikwenda katika kijiji cha Kiwengwa, ambapo ametoa wiki mbili kuondosha vigogo vya miti vilivyowekwa pembenzoni mwa fukwe kwa ajili ya kuzuia mawimbi ya maji ya bahari, sambamba na uchimbaji wa mchanga wa pwani.

Chanjaani walalamikia mavuno kidogo

Aisha Mohammed, Pemba
WAKULIMA wanaojishughulisha na kilimo cha mpunga bonde la Bundani katika shehia ya Chanjaani Wilaya ya Chake Chake Pemba walisema kilimo cha mpunga kinawakatisha tamaa kutokana na kupungua kwa mavuno siku hadi siku.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika bonde hilo walisema mavuno ya zao hilo yamekuwa yakipungua kwa kasi hali inayochangia kuwarudisha nyuma kimaendeleo.


Walisema wanajitahidi kulima zao hili ili kukuza kipato kitakachowawezesha kujikimu kimaisha na familia zao lakini wamekuwa wakivunjika moyo kuendelea na kilimo hicho.

Walifahamisha kuwa mbali na juhudi zao mavuno wanayoyapata hayasaidii hata kwa matumizi ya chakula seuze biashara.

“ Tunalima kilimo cha mpunga mwaka mzima lakini mavuno tunayoyapata hayatuwezeshi kupata hara chejio cha siku kumi 10”, walielezea wakulima hao.

Walifahamisha kuwa matayarisho ya kilimo hicho huanza mapema kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa kilimo lakini hawafaidiki na matunda ya kilimo hicho.

Walifafanua kuwa baada ya uvunaji wa kunde wanaendelea na kusia mpunga na kushughulikia mpunga huo hadi wanapofikia hatua ya mavuno.

Sambamba na hayo walisema mpunga huo unapofikia hatua ya kuvunwa huingiwa na wadudu na kupata maradhi hivyo mipunga huharibika na kupelekea kutozaa mazao bora, huku wakikabiliwa na ukosefu wa rutuba katika mabonde hayo.

Aidha wakulima hao wamelalamikia wizi wa mbegu za mpunga hali inayochangia upungufu wa mbegu hizo wakati wa msimu.

Pamoja na juhudi za kupambana na wadudu waharibifu wa mpunga wakulima hao wameiomba Serikali kuwapatia mbolea ili mashamba yao yaweze kuzalisha mazao kwa wingi na kuchangia juhudi za serikali za kupambana na umasikini kupitia sekta ya kilimo.

Mtoto wa kambo aunguzwa maji ya moto

Na Jumbe Ismailly, Singida
POLISI Mkoani Singida inamshikilia mwanamke kwa tuhuma za kwa kumwagia maji ya moto na kusababisha kumuunguza sehemu mbali mbali za mwili wake kwa kilichodaiwa kuwa hapendi kuishi naye.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Mkoa wa Singida, Celina Kaluba, mwanamke huyo ni Maria Eliasi (30) mkaazi wa mtaa wa Sokoine, mjini Singida alimuunguza Amina Mustafa mwenye miaka 2 na miezi kumi.

Hata hivyo, kamanda huyo alisema tukio hilo lilitokea tarehe 21 mwezi huu saa nne asubuhi katika mtaa wa kituo cha zamani cha magari, kata ya Majengo.

“Ajali hiyo ilisababisha mtoto huyo kuungua vibaya”, alisisitiza Kaluba.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi chanzo cha tukio hilo ni kutokumpenda mtoto ambaye alikuwa akiishi pamoja naye.

Hata hivyo kamanda Kaluba hakusita alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa na wakati mtoto huyo aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida hali yake ni mbaya.

Monday, 26 April 2010

Maadhimisho ya Muungano

VIONGOZI wa kitaifa wakiwa kwenye jukwaa kuu la uwanja wa Uhuru jijini Dar-es-Salaam walipohudhuria sherehe za miaka 46 ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika. (Picha na Ramadhan Othman).

Sarakasi ya Muungano

VIJANA wa sarakasi wakipandisha bendera ya taifa ikiwa ni shamra shamra za sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.(Picha na Ramadhan Othman).

Sherehe za Muungano zafana

Na Rajab Mkasaba, Dar es Salaam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, leo ameungana na viongozi mbali mbali katika maadhimisho ya kutimiza miaka 46 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru mjini Dar-es-Saalam.

Katika sherehe hizo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrishso Kikwete.

Mara baada ya kuwasili Rais Kikwete katika uwanja huo ambao ulifurika maelfu ya wananchi kutoka sehemu mbali mbali za nje na ndani ya jiji la Dar-es-Saalam Gwaride lilitoa salamu ya Rais na Mizinga 21 ilipigwa.

Kamanda wa gwaride alimkaribisha Rais na Amiri Jeshi Mkuu kukagua gwaride na baada ya hapo gwaride lilipipita mbele yaa Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa mwendo wa pole na haraka na baada ya hapo gwaride lilisonga mbele hatua 15 na kutoa salamu ya za kutimiza miaka 46 ya Muungano.

Viongozi wa dini mbali mbali walisoma dua ya kuiombea nchi na kuomba kudumishwa kwa muungano na kuwatakia heri na fanaka viongozi na wanancho wote wa Tanzania katika maisha yao.

Kwaya na maonesho ya halaiki vyote kwa pamoja vilitumbuiza katika sherehe hiyo, jumla ya wanafunzi 700 kati ya hao 200 kutoka Zanzibar walishiriki halaiki hiyo. Pia, wanafunzi kutoka skuli ya Hazina walitumbuiza kwa kuonesha uwezo wao mkubwa wa kucheza sarakasi.

Vikundi maalum vya ngoma za asili kutoa Tanzania Bara na Zanzibar vilitumbuiza katika sherehe hizo ikiwemo ngoma ya nindo ngulilo kutoka Dodoma, ngoma ya Kibati kutoka Zanzibar, ngoma ya kubwaya kutoka Zanzibar na ngoma ya nyangira kutoka Shinyanga. Msanii maarufu Mrisho Mpoto (Mjomba) nae alitumbuiza.

Viongozi wengine wakuu waliohudhuria katika sherehe hizo ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Muhammed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuia Nahodha na Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ali Juma Shamuhuna walihudhuria.

Wake wa viongozi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwemo Mama Fatma Karume, Maria Nyerere, Shadya Karume na Mwanamwema Shein walihudhuria.

Katika sherehe hizo zenye kauli mbiu isemayo ‘Tudumishe Muungano Mhimili wa Taifa letu’ pia viongozi mbali mbali wa vyama na serikali zote mbili nao walihudhuria, Mabalozi wanaoziwakilishanchi zao na wananchi kutoka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar walihudhuria.

Aidha, Mzee Hassan Omar Mzee, Hadija Abass na Sifueli Shima, walioshiriki kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar miaka 46 iliyopita nao walitoa salamu katika sherehe hizo.

Sunday, 25 April 2010

Tumerudi salama

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Amani Abeid Karume mkewe Shadya Karume wakisalimiana na wananchi waliofika kuwapokea katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Zanzibar wakirejea kutoka Uingereza. (Picha na Ramadhan Othman).

Saturday, 24 April 2010

Usafi Mjimkongwe

Kijiko kikifanya usafi katika eneo la Vuga ambalo linayatarishwa kwa ajili ya kiwanja cha michezo kwa watoto. (Picha na Othman Maulid).

‘Wanahabari watetee maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano’

• Watakiwa kutowaachia suala hilo wanasiasa pekee

• Muungano uimarishwe kwa kutatuliwa kwa vitendo kero
Na Mwanajuma Abdi
WAANDISHI wa Habari Zanzibar, wametakiwa kuungana pamoja katika kuibua mambo muhimu kwa maslahi ya Zanzibar na Taifa hili katika kutatua kero za Muungano na sio kuwaachia wanasiasa pekee.
 
Kauli hiyo imetolewa na washiriki wa kongamano la siku moja la mchango wa waandishi wa habari katika kustawisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililoandaliwa na Jumuiya ya Kuwaendeleza Waandishi wa Habari Wachanga Zanzibar (ODEYJO), lilifanyika katika Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar, Vuga mjini hapa.
 
Katika kongamano hilo mada mbili ziliwasilishwa, ikiwemo Mchango wa waandishi wa Habari katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao unatimiza miaka 46, iliyowasilishwa na Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Abdulla Mohammed Juma na Changamoto kwa wanahabari wa Zanzibar katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliwasilishwa na Mwandishi wa Habari Muandamizi, Rashid Omar.

Walisema waandishi wa habari wakiiungana pamoja itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo yanayoikabili Zanzibar likiwemo la kero za Muungano, kwa maslahi ya wananchi wa chini na sio maslahi ya viongozi peke yao.
 
Walieleza kero za Muungano zimekuwa zikizungumzwa juu juu na Serikali na wanasiasa mezani bila ya kushirikishwa ipasavyo vyombo vya habari, jambo ambalo uwakilishi wa wananchi wa chini unakosekana kufikishwa taariza zao.

Aidha walifahamisha kuwa, kero nyingi za Muungano zinazozungumzwa ni maslahi ya wakubwa na Serikali lakini watu wa chini hawaguswi, ambao ndio wanaoumia zaidi likiwemo suala la kupandishiwa bei kwa vitu mbali mbali kutokana na wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Akichangia mada hizo, Mwandishi wa Habari Muandamizi, Enzi Talib Aboud alisema waandishi wa habari hawana umoja katika kusaidiana kuondosha kero mbali mbali zinazoikabili Zanzibar, ambapo suala la Muungano nalo limekuwa watu wakipiga kelele za mdomo mtupu.
 
Alifafanua kuwa, kero za Muungano zinashindwa kutatuliwa kutokana na watu wanapinga kelele, ambapo wanapokwenda Tanzania Bara viongozi wetu wanashindwa kutokana hawazungumzi kisheria wao wanabakia katika kupiga kelele.
 
Alieleza masuala yanayoigusa Zanzibar kimaslahi moja kwa moja wananchi, waandishi wa habari na wanasiasa waweke nyuma tofauti zao na kinachobakia mbele ni kuungana kwa maslahi ya Taifa, ambapo katika Bunge wa Jamhuri ya Muungano Tanzania wapo wajumbe wa CUF ni bora wawe wanaungana na wanaCCM wa Zanzibar katika kuzuia miswada ya kisheria inayoibana Zanzibar ili isipite kwani ikishapita ndio matatizo yanaongezeka.
 
Nae Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Ali Vuai alisema kero za Muungano haziwezi kutatuliwa na kamati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa SMZ, katika meza lazima masuala hayo yarejeshwe katika vyombo vya kutunga sheria Bunge ili kupatikana kwa theluthi za wajumbe juu ya utatuzi huo.
 
Alisema kero za Muungano hizo zimeanza muda mrefu, ambapo pale Zanzibar ilipotaka kujiunga uanachama wa Jumuiya ya OIC, ambapo ikakataliwa na Jamhuri ya Muungano Tanzania, sambamba na Jumuiya ya Afrika Masharikiri kuingia moja kwa moja na badala yake iingie kupitia Serikali ya Tanzania.
 
Mwandishi wa Habari kutoka Idara ya Habari Maelezo, Salama Njani, akichangia mjadala huo alisema vyombo vya habari bado havina uhuru wa kutosha katika kuandika na kufichua uovu unaendelea kutokea na kujitokeza siku hadi siku, hususani vyombo vya Serikali vinabanwa katika kuibua mambo ambayo yanakiuka katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo likiwemo hilo la kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Mapema Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti la Serikali Zanzibar, Abdulla Mahammed Juma aliwasilisha mada juu ya mchango wa waandishi wa habari katika kuimarisha Muungano huo, alisema habari nyingi zinazoandikwa ni za upande mmoja wa muungano huvutia kwake, ambapo wale wa Tanzania Bara kinachozungumzwa na viongozi wa Zanzibar dhidi ya Muungano ndiyo huwa habari na wale wa Zanzibar nao hutumia hicho kama habari muhimu kwa maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano huo.
 
"Hali hii kwa kweli kwa kiasi kikubwa inadhoofisha muungano kwa wanahabari kutumika katika kuonesha zaidi upande mmoja ambao mara nyingi huwa Zanzibar kuonekana unachafua au kupinga muungano wakati pengine vyombo au waandishi hao vingeweza kuonesha kwamba Zanzibar inadai haki na fursa zake ndani ya muungano na kuchangia uimarikaji wake", alisisitiza Abdulla.
Alisema wengi wanathubutu kusema kuwa matatizo ya muungano yameanza tokea unazaliwa ambapo hapakuwa na uwazi kuhusiana na mipaka yake na maamuzi ya upande mmoja wa muungano huo ambao ni Zanzibar, unaoelezwa kwamba muafaka ulikosekana katika Baraza la Mapinduzi kuhusiana na kuunganisha nchi hiyo.
 
"Baada ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar na muasisi wa Muungano huu, Marehemu Mzee Abeid Karume, ambae alizieleza wazi kero za muungano na kuzikataa wazi wazi kasoro za Muungano, kasoro hizo zilikuwa zikiogopwa hata kuzungumzwa na aliyejaribu kufanya hivyo alitiwa muhuri wa uchochezi na wengine wamepoteza ajira zao", alieleza.

Alisema kutokana na kasoro hizo Zanzibar imepoteza utaifa, kutotambulikana kimataia kwa mfano UN, Jumuiya ya Madola na AU, pia imepoteza hadhi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuundwa kwa Benki Kuu ya Tanzania ambayo haina maslahi na Zanzibar, japokuwa mtaji wake ulitumika kupitia Bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki kuanzisha benki hiyo.

Alifahamisha kuwa, makubaliano ya awali ya Muungano yalikuwa ni mambo 11 lakini sasa yamefikia 22, hivyo kunaonesha dhahiri kuna ujanjaujanja unafanyika, ambapo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania sehemu ya kwanza ibara ya tisa kifungu cha 34 (1) Rais wa Tanzania atakuwa na mamlaka ya mambo ya muungano na mambo yahusuyo Tanzania Bara, jambo ambalo linaikosesha haki Zanzibar ya kumpata mdau waliyeungana nae miaka 46 iliyopita.
 
Alileleza kwamba, wakati kifungu cha 34 (2) na (3) kinaeleza kwamba iwapo Rais wa Jamhuri wa Muungano hayupo nchini atakaimiwa na Makamo wa Rais kama hayupo Spika wa Bunge kama hayupo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
 
"Sehemu ya pili inayohusiana na Makamu wa Rais nayo pia ina kasoro tokea Rais wa Zanzibar kufutiwa fursa ya kuwa makamu wa Rais moja kwa moka kama iliyvokuwa katika makubaliano ya kwanza ya Muungano wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere.

Mhariri Mtendaji huyo, alisema mchango wa wanahabari ni muhimu katika kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar, bila ya kukubali kuambukizwa jazba za wanasiasa, wanahabari wajifunze kwa kuongeza uelewa wao katika kuwasaidia watanzania.

Akizungumzia hatma ya muungano, Mhariri huyo alisema ili uimarike ni lazima serikali mbili zilizouanzisha ya Tanganyika (Tanzania Bara) na Zanzibar zikae tena kufikiria muundo mpya wa muungano ambao utapunguza malalamiko ya upande mmoja kunung’unika au kumezwa.
 
Pia alisema kutokana na mabadiliko ya ulimwengu na kukua kwa demokrasia, suala la kufanyika maamuzi ya wananchi kuhusu muungano huu sasa limefikia wakati wake, ambapo njia muafaka ni kutumia kura ya maoni kama zinavyofanya nchi nyengine duniani, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekwa hadharani mkataba wa muungano ‘articles of union’ ambao unaaminika kuwa umeelekeza mambo mengi ambayo hadi sasa hayajafanyika.
 
Nae Rashid Omar Mwandishi Mwandamizi, akitoa mada alisema changamoto za kimtizamo wa itikadi za vyama baadhi ya wanahabari kuzungumza Muungano kwa uwazi linamshabaha sana na itikadi za vyama vya siasa, kutokana na hali hiyo baadhi yao wameamua kukaa kimya ama kuwa na kigugumizi na huku wengine wakijaribu kuandika makala na kutayarisha vipindi vyenye mtazamo wa kutetea zaidi kuliko uhalisia, ambao wananchi wanapaswa kupatiwa kupitia juhudi za vyombo vya habari.

Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi wa Vijana, Mohammed Salim aliipongeza Jumuiya ya ODEYJO kwa kufanya kongamano hilo, ambalo linakwenda na wakati katika shamra shamra za kilele cha maadhimisho ya miaka 46 ya Muungano huo tokea Aprili 26, 1964.
 
Alisema kongamano hilo litajadili mafanikio yaliyofikiwa na Muungano huo kwa lengo la kuimarishwa zaidi na matatizo yaweze kujadiliwa na kuondosha ili uweze kuwepo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.
 
Alisema changamoto kubwa zinazowakabili waandishi wa habari waache tabia ya kuandika habari za uchochezi zinazosababisha migogoro katika nchi na badala yake waandike habari zenye kuleta umoja na kudumisha utulivu na amani nchini.
 

Kombo: Wekezeni katika elimu ya watoto wenu

Na Mwanajuma Abdi
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwekeza suala la elimu kwa mtoto ndio shabaha kubwa ya kumsaidia kuondokana na umasikini katika maisha yake na Taifa kwa ujumla.

Hayo aliyasema wakati akiwatunuku vyeti wahitimu 56 wa kidato cha nne na 38 wa kidato cha sita, kuwapa zawadi wanafunzi bora kitaifa kwa masomo mbali mbali na walimu wao wa masomo yaliyofanya vizuri likiwemo la Biology na Kiarabu, sambamba na kuzindua skuli ya maandalizi katika Sunni Madressa School, iliyopo Mkunazini mjini hapa.

Alisema elimu ndio kichocheo kikubwa katika kuleta mabadiliko ya kupambana na umasikini na ujinga katika Taifa lolote duniani.

Alieleza dunia hivi sasa imekuwa kama kijiji kutokana na kukua kwa mfumo wa sayansi na teknolojia ya mawasiliano ikiwemo internet, hivyo aliwashauri waitumie vizuri kompyuta katika kuwapatia mambo mengi yatayowawezesha kuwanyanyua katika taaluma yao kwa lengo la kujifunza zaidi.

Naibu Waziri huyo, alitoa wito kwa wanafunzi hao kujiendeleza kusoma zaidi ili baadae waweze kuwa viongozi wazuri wa taifa hili, ambapo asilimia 50 kwa 50 ya wanawake katika vyombo vya kutunga sheria katika Bunge na Baraza la Wawakilishi liweze kufikiwa wakati watakapomaliza masomo yao.

Aidha alisema mafanikio ya elimu hayatoweza kupatikana ikiwa wazazi na walimu hawatoshirikiana katika kuwahimiza wanafunzi kuwa na maadili mema na kujiamini wakati wowote, ambalo hilo tayari limeanza kuonekana kama wanafunzi wa skuli hiyo wana uwezo mkubwa wa kujiamini kwa kusimama mbele za watu.

Mapema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Jabir Makame wakati akimkaribisha Kombo, aliwaeleza wanafunzi hao wakati wa kusoma unajisikia shida kweli lakini faida yake unapomaliza na kupata kazi ndio unasahau matatizo yote uliyoyapata wakati unatafuta elimu, ambapo aliwashajihisha walimu na wazazi kuwatia moyo watoto ili wasome kwa bidii na faida wataiona baadae.

Nae Mkurugenzi Mtendaji Sunni Madressa School, Hussein Ali Suleiman alisema skuli hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, ambapo wanafunzi mwaka 2008 hadi 2009 wamepata sifa za kutoa wanafunzi bora Tanzania nzima katika masomo mbali mbali, sambamba na mwanafunzi Fatma Saad ametoa bora kwa kuzungumza kiingereza.

Nae Mwalimu Mkuu Rajab Mzee Wambi, aliwausia wanafunzi hao kujiepusha na masuala yasiyowahusu kama kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na mambo yanatowasababishia kupata virusi vya UKIMWI.

Mkuu huyo aliwapongeza walimu kwa kuwajibika ipasavyo katika majukumu ya kazi zao, ambazo zinachangia kuwasaidia wanafunzi kufaulu vizuri katika mitihani yao ya kitaifa, sambamba na wazee kutoa ushirikiano wa karibu katika uongozi wa skuli hiyo.

Wanafunzi wa kike waiomba FAWE iendelee kuwapiga jeki

Husna Mohammed
WANAFUNZI wawili wa Skuli ya Mwanakwerekwe ‘C’ Unguja, wameiomba Jumuiya ya wanawake wasomi Afrika kanda ya Zanzibar (FAWE), kuendelea kutoa misaada yao ya kielimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Wanafunzi hao Haitham Ali Khamis (17) kidatu cha tatu na Arafa Rashid Mohammed (17) kidatu cha pili, waliyasema hayo walipokuwa wakizungumza na gazeti hili wakati tofauti huko skuli ya Mwanakwerekwe ‘C’.

Walisema iwapo FAWE itaendelea na misaada yake hiyo hasa kwa mtoto wa kike, ni wazi watoto hao wataweza kupata wataalamu wazuri wa kike hapo baadae.

Walifahamisha kuwa, katika jamii hasa zinazoishi katika maisha duni kumekuwa na watoto wenye vipaji lakini wamekuwa wakishindwa kupata elimu kutokana na hali ngumu ya umasikini waliyonayo.

“Kama mimi nilikuwa katika hali mbaya kimaisha, lakini naishukuru FAWE, imeweza kuniinua na hivi sasa naendelea na masomo yangu hapa”, alisema Haitham.

Alisema hasa baadhi ya sehemu za vijijini kumekuwa na maisha magumu na hivyo baadhi ya watoto wamekuwa wakishindwa kupata elimu.

Kwa upande wake mwanafunzi Arafa Rashid, aliishukuru jumuiya ya FAWE kwa kuweza kumsaidia kielimu ambapo hivi sasa anaendelea vizuri na masomo yake.

Alisema FAWE iko katika mstari wa mbele katika kuwahakikishia elimu hasa kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika jamii.

“Naishukuru sana FAWE kama sio wao hivi sasa ningekuwa katika hali nyengine”, alisema.

Alisema FAWE imekuwa ikiwasaidia katika mahitaji mbalimbali ya kielimu ikiwa ni pamoja na kuwapa fedha za unifomu, madaftari, fedha za kujikumu na mambo mbali mbali yenye kuhusina na elimu.

Hata hivyo aliiomba FAWE kuiongeza jitihada zao hizo kwa lengo la kuziinua jamii masikini kwa msalahi yao na taifa.

Waziri Haroun aitaka SOS ishirikiane na Serikali

Na Ali Mohamed, Maelezo
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman, ameutaka uongozi wa kituo cha kulelea watoto cha SOS, kuweka nia ya kushirikiana na serikali katika kuimarisha elimu.

Alisema serikali itatoa kila msaada unaohitajika kwa kituo hicho katika dhamira ya kuimarisha ushirikiano yatakayosaidia kuimarisha elimu nchini.

Akizungumza na ujumbe wa Shirika hilo ulioongozwa na Mkurugenzi Mkaazi Wilhelm Humber, Waziri Haroun alisema serikali inapenda kuliona shirika hilo linafungua vituo vya kulelea watoto kila Mkoa hapa Zanzibar.

Alisema kufunguliwa vituo hivyo kila mkoa kutaisaidia serikali katika kutoa fursa kwa watoto yatima, masikini na wanaoishi kwenye mazingira magumu kupata elimu na huduma nyengine.

Haroun alibainisha dhamira ya Serikali kuwa haina nia ya kuingilia utaratibu wa utendaji wa kituo hicho na inafarajika kukiona kikiendelea kutoa huduma kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Ujumbe huo wa SOS ulifika wizara ya elimu kuonana na waziri Haroun, kuomba ushirikiano na serikali hasa kupatiwa walimu kutoka serikalini ili waweze kujiimarisha zaidi kutoa elimu visiwani hapa.

Aidha hapo awali katika miaka ya 1980 na 1990 kulikuwepo na mashirikiano hayo ambapo yalikwama kutokana na dhana potofu ya uongozi wa kituo hicho wakati huo kuwa kuendelea na mashirikiano hayo Serikali ingewaingilia katika shughuli zao za utendaji.

Mkurugenzi huyo Wilhelm Humber alishtushwa na kusikitishwa na hali hiyo iliyojitokeza na ameahidi kufufua ushirikino na serikali kwa vile bila kushirikiana na serikali inakuwa vigumu kupata mafanikio.

Waziri Haroun aliuagiza uongozi wa kituo hicho kuandaa mikakati ikiwa ni pamoja na kuwa na vikao vya pamoja na watendaji wa Wizara ya Elimu ili kuepuka hitilafu zilizojitokeza hapo awali.

Afisa wa Ubalozi wa Marekani

Afisa wa Ubalozi wa Marekani Bill Strassberger (kushoto), akipokea maelezo kutoka kwa mtaalamu wa IT katika Shirika la Magazeti ya Serikali, Yussuf Ali Hassan (kulia), katikati ni Naibu Mhariri Mtendaji wa Shirika hilo Nasima Haji Choum. (Picha na Othman Maulid). 

Friday, 23 April 2010

Uchaguzi mkuu 2010 wagombea wawindana 'kumfuata babu'

Na Mwantanga Ame
VITUKO vya imani za ushirikina kwa baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi za Uongozi uchaguzi Mkuu ujao, vimepamba moto baada Mwakilishi wa Pemba kulisukua ndumba la chupa ya damu mlangoni mwa nyumba yake.

Tukio hilo limetokea wiki iliopita huko kisiwani Pemba baada ya Mwakilishi huyo (jina linahifadhiwa) ambaye ni kijana mdogo, kuelezea Zanzibar Leo kukutwa na tukio hilo huko nyumbani kwake kati ya Majimbo yaliomo katika Mkoa wa Kaskazini.

Mwakilishi huyo alisema aliikuta chupa ya ndumba hiyo iliyozikwa katika mlango wake wa mbele wakati akilima kwa lengo la kupunguza majani nyumba kwake.

Mwakilishi huyo anaeishi na familia yake alieleza kuwa alishangazwa na tukio hilo baada ya jembe alilokuwa akilimia kugonga chupa hiyo na kulazimika kuita jamaa zake kuwafahamisha mkasa huo.

Alieleza kuwa baada kuifahamisha familia hiyo yeye binafsi halikumpa mshtuko kutokana na familia yake kumpa moyo kwa kuitisha kisomo cha Kur-ani ghafla na baadae kuendelea kuisukua chupa hiyo ya ndumba iliyozikwa ardhini.

Alieleza kuwa, baada ya kusukuliwa chupa hiyo ambayo hutumiwa kuwekea maji ndani yake waliikuta ikiwa na damu inayosadikiwa kuwa ni ya binadamu, vipande vya memo ya mnyama pamoja na vipande vinne vya nyama.

Kutokana na kukutwa vitu hivyo, Mwakilishi huyo alisema familia yao ilivichukua na kumruhusu yeye binafsi aivunje chupa hiyo kwa jembe alilokuwa akilitumia kwa kulimia na kisha kuichoma moto.

Alifahamisha kuwa tangu akutwe na mkasa huo ana mashaka makubwa waliotenda hilo ni kati ya wagombea wenzake waliojitokeza kuchukua fomu kwa Chama cha CUF kwa vile wapo waliomtishia na hilo.

Alisema usiku wa kuamkia siku hiyo ilinyesha mvua kubwa ikiambatana lakini walisikia kuwapo kwa vishindo, lakini familia yake haikuvitilia manani kwa kuona ni nguvu ya mvua.

Kwa mujibu wa Mwakilishi huyo, alifahamisha katika Jimbo ambalo yeye anaendelea kulishikilia tayari waliojitokeza kuwania nafasi ya Uwakilishi kwa hivi sasa wamefikia wagombea wanane huku nafasi ya Ubunge wakiwa ni 18.

Alieleza suala la ushirikina kwa wanaotaka kugombea nafasi mbali mbali katika uchaguzi mkuu ujao, hivi sasa lipo kwa kiasi kikubwa ambapo wengi wa waganga wanaona ni njia moja wapo ya kunufaika huku wengine wakishindana kupata waganga wakali zaidi.

Alisema hilo linajionesha baada ya kujitokeza kwa baadhi ya wagombea kuwahamishia waganga hao majumbani mwao huku wengine wakiwatoa nje ya Zanzibar.

Alifahamisha hivi sasa wapo watu wameamua kuwapa nyumba watu wanaosadikiwa kuwa ni waganga wa kienyeji kutoka sehemu mbali mbali ikiwa ni lengo la kupiga kambi kwa muda ili wafanye shughuli zao za biashara kwa msimu huu wa Uchaguzi.

“Hapa wapo wa kisiri siri wanatoka nje ya Zanzibar sijui wa Sumbawanga hawa ama Nigeria sijui hata wametokea wapi nasikia wapo” alisema Mwakilishi huyo.

Alifahamisha wengi wa wagombea hao wanaonekana kutojiamini kuingia katika mchakato wa uchaguzi ujao bila ya kutumia waganga huku wengine wakitoa hata vitisho vya kuwang’oa kwa kutishia maisha.

Hata hivyo, Mwakilishi huyo alisema licha ya kukutwa na mkasa huo bado hajavunjika moyo wa kuendelea na mchakato huo na atahakikisha kuwa anafanikiwa kuibuka kidedea katika kura za maoni.

Alisema hilo anaamini kuwa litatokea kutokana na kuweza kufanikisha mambo kadhaa ya maendeleo katika Jimbo analoliongoza huku bado akiwa na ushawishi kutoka makundi tofauti.

Wakati hilo likiwa kwa Upande wa Pemba wagombea walioonesha nia katika majimbo ya Unguja nao wanalilalamikia hilo kutokana na baadhi yao kukutwa na mikasa ya aina hiyo.

Akisimulia mmoja wa watu wenye nia ya kuwania nafasi ya Ubunge kwa Jimbo la Rahaleo, ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema yeye binafsi alipatwa na maradhi ya kupooza viungo vya miguu na kumlazimu kutibiwa kwa siri na familia yake kwa muda wa wiki mbili.

Alisema alipatwa na hali hiyo wakati akiwa nyumbani kwake jambo ambalo liliifanya familia yake kuzuiya kuonana na mtu yoyote wakati akiwa matibabuni jambo ambalo alieleza ugonjwa huo ulimshangaza.

“Bwana ushirikina upo na unafanywa kweli kweli mimi binafsi ndio nimeanza kutoka nje sasa nilikuwa siinuki wiki mbili nilikuwa ndani miguu hii nilitiwa kama nanga na viungo vikubwa unavyolemazwa mikono na miguu” alisema Mgombea huyo.

Alifahamisha kubwa zaidi wakati akiwa matibabuni mmoja jamaa yake anayejishughulisha na kazi za tiba ya jadi alifuatwa na mtu kutaka amsaidiea dawa ya kukatisha maisha yake lakini jamaa yake huyo alikataa kwa vile hakufahamu kama anauhusiano naye na ndie aliyeshiriki kumtibu wakati alipokutwa na tatizo hilo.

Kutokana na hali hiyo Mwanachama huyo alieleza hivi sasa tayari ameweza kupata matibabu na amerudi katika hali yake ya kawaida na kueleza kuwa ushirikina upo wa hali ya juu katika mbio hizo.

“Mie nasema kinywa kipana kweli ushirikina unafanywa mimi yamenikuta na hivi nimetoka matibabuni kwani kinanishangaza hata simu zangu zilizimwa watu wananambia sipatikani wakati ilikuwa wazi na hili sio langu pekee yangu katika Jimbo hilo yupo na mwengine sasa hivi mkono umeshapooza” alisema Mwanachama huyo.

Mwanachama mwengine ambaye nae ameonesha nia ya kugombania katika Jimbo la Jang’ombe, alidai suala la kutumia imani za ushirikina hivi sasa lipo kubwa na tayari limeanza kuwaandama wanaoonekana nyota zao kung’ara katika majimbo wayotaka kugombea.

Mwanachama huyo alidai kuwa hali hiyo tayari imeshamkumba mmoja wa wagombea hao kwa kupooza viungo vya miguu na mikono ambapo hivi sasa tayari familia yake inaendelea kumpatia matibabu.

Wakati hilo likitokea katika Jimbo la Jang’ombe, tukio jengine linadaiwa kutokea katika Jimbo la Fuaoni, ambapo mmoja wa waonesha nia ya kugombea katika Jimbo hilo amejikuta kukutwa na masahiba ya kuvunjwa nguvu za kupoteza kumbu kumbu kila anapojaribu kutaka kuzungumzia azma yake.

Mmoja ya wanachama wa CCM, alidai kuwa inasikitisha kuwapo kwa vituko hivyo ambavyo vinaonekana kutishia maisha kwa waonesha nia pamoja na kujawa kwa ghofu ya kupoteza maisha.

Alisema sehemu kubwa ya matatizo yanayoendelea kuwapa kwa imani hizo za kishirikina hivi sasa wengi waliokutwa na masahiba hayo wamepoozeshwa viungo vya miguu na mikono.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo tayari Tume ya Uchaguzi hivi sasa imo katika matayarisho mbali mbali.

Mgombea Urais Z'bar kuweka dhamana milioni 3 ZEC

Na Issa Mohammed
TUME ya Uchaguzi Zanzibar imepandisha kima cha fedha za dhamana kwa watakaogombea nafasi ya urais,uwakilishi na udiwani katika uchaguzi Mkuu ujao.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume hiyo kwa vyombo vya habari, mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu atatakiwa kuweka dhamana ya fedha shilingi milioni tatu badala ya shilingi milioni moja.

Taarifa hiyo imefahamisha kwamba mgombea uwakilishi atatakiwa kuweka dhana ya shilingi laki tatu badala ya shilingi hamsini elfu wakati mgombea udiwani ataweka dhamana ya shilingi hamsini elfu badala ya shilingi elfu kumi na tano.

Tume hiyo imesema kwamba maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri na kwamba imo katika jitihada za kuhakikisha kuwa ratiba ya kazi zote zilizopangwa kwa ajili ya uchaguzi huo zinakwenda kama ilivyokusudiwa.

Aidha, Tume hiyo imetangaza tarehe za kuchukuwa fomu kwa wagombea watakaowania nafasi ya urais, uwakilishi na udiwani katika

uchaguzi huo utakaokuwa wa tatu chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Tume katika taarifa hiyo, imefahamisha kuwa uchukuwaji fomu za kugombea urais utaanza Agost 10 hadi 30, wakati uchukuaji fomu za uwakilishi na udiwani utaanza tarehe Agosti 15 hadi 30 Augosti.

Kwa upande wa kampeni za uchaguzi, tume imesema shuhuli hizo zitaanza Septemba 10 hadi 30 na kuwa siku ya kupiga kura itakuwa tarehe 31 Oktoba.

Hatutaki ujenzi kwenye eneo hili

Wananchi wa Mchangani wakibomoa mabati kupinga ujenzi kwenye eneo la wazi.(Picha na Abdulla Masangu).

Changamoto za Muugano zifanyiwe kazi kuuimarisha

Na Halima Abdalla
PAMOJA na faida nyingi zinazopatikana katika Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar bado Muungano huo unakabiliwa na changamoto kadhaa zitakazoufanya uimarike zaidi.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Kikundi cha Wazanzibari wanaotetea Muungano, Rashid Yussuph, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari maelezo Rahaleo Mjini Zanzibar.

Katibu huyo alisema zipo kasoro kadhaa za Muungano ambazo leo hii zimegeuzwa na kuitwa kero ambapo kwa njia moja au nyengine zimekuwa zikiathiri maisha ya Watanzania.

Alifahamisha kuwa pamoja na Tume iliyoundwa na rais Kikwete ya kutatua kero hizo, bado tume hiyo haijafanyakazi ya kutosha katika kuzipatia ufumbuzi, jambo linalozua malalamiko kutoka kwa wananchi wa pande zote.

"Tume iliyoundwa haijaonesha uwiano utakaosaidia katika kutatua migogoro", alisema katibu huyo.

Katibu huyo alisema endapo kero za Muungano zitatakiwa zitatuliwe ni lazima serikali, iunde Tume itakayokuwa haijumuishi viongozi na watendaji wa Serikali.

Naye Amour Bamba, mjumbe wa kamati hiyo, alisema lazima pawe na mgawo wa haki sawa kwenye Muungano baina ya Watanzania wa Zanzibar na Watanzania bara.

Alisema matatizo mengi ya Muungano yanatokana na kutokuwepo usawa wa kiuchumi ndio maana yamekuwepo mawazo ya mmoja kunufaika zaidi ya mwengine.

''Kwa bahati mbaya tangu mwaka 1964 hadi leo watu wanazungumza kuhusu kero tu, hatujui lini kero hizi zitakwisha", alisema Bamba.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika Aprili 26 mwaka 1964, chini ya uasisi wa Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume ambapo mwaka huu unatimiza miaka 46.