Tuesday, 13 April 2010

Awamu yapili maji Mjini Magharibi kukamilika Juni

Mwanajuma Abdi
AWAMU ya pili ya mradi mkubwa wa Maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu ili kurejesha huduma hiyo kwa wananchi ambapo hivi sasa hawaipati kwa uhakika.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Hemed Salim Hemed alito kauli hiyo ya matumaini, jana, wakati wa mahojiano na gazeti hili katika Afisi za Mamlaka hiyo, Mabluu mjini hapa.

Alisema mradi wa maji awamu ya pili umekamilika kwa asilimia 80 kwa sasa, ambao utakuwa umegharimu shilingi Bilioni 23 hadi kukamilika takriban miezi miwili na nusu ijayo kuanzia sasa.
 
Alisema majaribio ya kiufundi yatarajiwa kufanyika Mei mwaka huu, kabla ya kupeleka huduma hiyo kwa wananchi ifikapo Juni, mradi huo utakapokamilika.

Mradi wa Maji Mjini Magharibi, unafadhiliwa na Serikali ya Japan, ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetumia shilingi Bilioni moja kulipa fidia na kupeleka umeme mkubwa kwa matumizi katika mradi huo.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu huyo, awamu ya pili ya mradi huo umehusisha uchimbaji wa visima vitano, ambapo Kinu moshi visima vitatu, viwili vimechimbwa Kinuni, ujenzi wa matangi Dole na Kinuni, ambapo hivi sasa upo katika harakati za kukamilisha kuta za ndani katika matangi hayo.
 
Hata hivyo, alisema kazi ya ulazaji wa mabomba inaendelea huku mafundi wengine wakijihusisha na ukataji wa barabara kupitisha mabomba ya maji ikiwemo barabara ya MAGOMENI.

Mkurugenzi huyo, alieleza kuwa mradi huo utakapokamilika utakuwa na vituo vikubwa vinne vyenye kazi ya usambazaji wa maji kwa wananchi katika maeneo mbali mbali.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Welezo ambacho kitakuwa kinasambaza maji katika Wilaya ya Mjini, Dole kitasambambaza maeneo ya Mfenesini, Dole, Bububu wakati Kinuni katika maeneo ya Mombasa, Kinuni na maeneo jirani, na Saateni kitasambaza huduma hiyo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar, ambavyo vyote vitakuwa vinaungana ili viweze kupokezana inapotokea hitilafu.
 

No comments:

Post a Comment