Tuesday 6 April 2010

Nyumba za Michenzani zafunguliwa

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amekabidhi funguo kwa wananchi waliobakia ambao walivunjiwa nyumba zao kupisha ujenzi wa nyumba za maendeleo Michenzani baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Ujenzi huo ni kuimarisha makaazi ya kisasa kwa wananchi wote na kuondokana na makaazi duni ambayo nyengine zilikuwa ni nyumba za makuti ‘full suti”.

Katika makabidhiano hayo Dk. Karume alisema wananchi waliokabidhwa ni wale ambao bado familia zao zilikuwa hazijalipwa fidia za nyumba zao zilizobomolewa, enzi za Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Alisema yapo maombi ya mahitaji ya nyumba hizo yapatayo 450 wakati nyumba zote zilizopo ni 182, lakini kipaumbele kinatolewa kuwafidia waliovunjiwa wakati huo.

Marehemu Karume aliamua kwa makusudi kuwajengea makaazi bora wananchi na kuondokana na makaazi ya unyonge kuishi katika nyumba za makuti (full suti), nyumba za mawe, ambazo juu zimeezekwa madebe.

Dk. Karume alisema familia hizo ndizo zilizobakia, ambazo bado hazijalipwa fidia na jana waliweza kukabidhiwa nyumba hizo wananchi hao ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo ahadi ya Marehemu Mzee Karume ambaye aliuawa kwa kudhulumiwa na mahaini.

Muasisi huyo wa Afro Shiraz leo anaadhimishiwa kumbukumbu ya kifo chake na wananchi watamkumbuka kwa dua mbali mbali.

Aliwaeleza wananchi kwamba siku ya jana imeangukia vizuri kwa kuweza kukamilisha zoezi la kuwalipa fidia wananchi waliokuwa wakidai nyumba zao kabla ya leo ambayo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha Mzee Karume.

Aidha alitoa wito kwa wananchi waliokabidhiwa nyumba hizo kuzitunza na kulinda mazingira ya eneo hilo, ambapo alisisitiza kwamba anayetaka kufanya ujenzi mwengine ndani ya nyumba hizo lazima apate kibali kutoka Idara ya Majenzi na sio kujifanyia, ili kuepusha kusababisha madhara kwa wengine na kuzitia ubovu.

Alifafanua kwamba, nyumba hizo zikitunzwa zinaweza kutumika miaka mingi, ambapo hadi miaka 300 zinaweza kufika, hivyo lazima watumiaji wawe waangalifu kwa hilo la kufanya ujenzi mwengine wa kubomoa kuta bila ya kupata kibali cha maelekezo.

Hata hivyo, alisema baadhi ya watu waliziita nyumba hizo ‘matreni ya Karume’ lakini kwa sasa zimekuwa na tija, kwa wamiliki kwa kuuza hadi shilingi milioni 20 kwa nyumba moja.

Alieleza nyumba hizo ameweza kuziendeleza ujenzi kutokana na mkopo kutoka kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) na fedha nyengine kutoka Serikalini baada ya kudhibiti mapato.

Aidha aliwausia wananchi waendelee kushirikiana na kujenga umoja katika kudumisha utulivu na amani nchini kwani bila ya mambo hayo hakuna maendeleo ya kweli.

Ujenzi nyumba hizo ulihusisha jumba namba tisa fleti 48 na jumba namba 10 fleti 142 na maduka, ambapo ujenzi wake ulifanywa na Vikosi vya SMZ, ambavyo vilipongezwa na Rais Karume.

No comments:

Post a Comment