Saturday 3 April 2010

Wananchi ndio wataoamua Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar: Nahodha

Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imesema hakijafanya uamuzi wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kabla ya kuwapelekea wananchi kura ya maoni ili watowe ridhaa yao.

Kauli hiyo aliitoa jana, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha wakati akiahirisha kikao cha Baraza la Wawakilishi hadi Juni tisa mwaka huu, ambapo mkutano wa 19 wa Baraza hilo, uliochukuwa muda wa wiki mbili.

Mkutano huo Wawakilishi walipata nafasi ya kuuliza maswali 66 ya msingi na kujibiwa, miswada mitano ya sheria, ikiwemo Mswada wa sheria ya kufuta sheria ya Baraza la Michezo na kuanzisha sheria mpya ya Baraza la Taifa la Michezo na Mswada wa sheria ya kuweka Haki na Wajibu wa Serikali katika kesi za madai na utaratibu wa mwenendo wa madai dhidi ya Serikali.

Alieleza wapo baadhi ya watu wanaowaambia wananchi kuwa uamuzi wa kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa tayari umeshafanywa, jambo ambalo sio kweli bado uamuzi huo haujafanywa.

“Mwezi Januari tulijadili hoja ya kufanya kura ya maoni katika kikao hiki na tumepitisha mswada wa sheria ya kuitaka Tume ya Uchaguzi kuandaa kura ya maoni ya kuwauliza wananchi iwapo wanataka au hawataki iundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa”, alifafanua Nahodha.

Alisema maoni hayo ya wananchi ndio yatakayoamua kuanzishwa au kusianzishwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu (2010).

Alifahamisha kuwa, kura ya maoni ni utaratibu unaotumiwa na nchi nyingi zenye demokrasia iliyoshamiri katika kutoa uamuzi wa masuala mazito ya kitaifa, kwani inatoa fursa ya mfumo wa demokrasia moja kwa moja katika nchi.

“Wapo baadhi ya wasomi wanasema uamuzi wetu hauna maana na tunapoteza fedha za walipa kodi bure sisi wawakilishi tulipaswa tuamue kwa niaba ya wananchi, ni kweli lakini busara inaonesha kwamba kuwashirikisha watu wote katika maamuzi ya jinsi wanavyotaka waongozwe ni bora zaidi”, alieleza Nahodha.

Aliongeza kusema kwamba wananchi wanapaswa waelimishwe kiasi cha kutosha ili wafanye maamuzi ya busara na hekima, ambapo kazi hiyo inawakabili Tume ya Uchaguzi Zanzibar iliyoachiwa jukumu la kuandaa kura ya maoni.

Alieleza kuwa Zanzibar inafungua ukurasa mpya katika historia demokrasia ikiwa ni miongoni mwa nchi chache katika ukanda wa Afrika Mashariki kuanzisha kura ya maoni katika kutoa uamuzi wa masuala mazito ya kitaifa kwa kuwavutia hisia za watu wengi ndani na nje ya nchi.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume kwa kuhimiza umoja, mshikamano na kuimarisha amani na utulivu kwa lengo la kukuza maendeleo nchini.

Alifahamisha kwamba, maridhiano ya kisiasa kati ya Rais Karume na Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu CUF, yamefungua milango ya maelewano kati ya vyama hivyo na wananchi kwa ujumla na kudumu kwa amani na utulivu nchini.

Alisema kuwepo kwa amani na utulivu kutasaidia sana kuwavutia wawekezaji mbali mbali kuja kuwekeza nchini, ambapo mandhari nzuri ya visiwa inasaidia katika shughuli za kibiashara.

No comments:

Post a Comment