Na Ali Mohamed, Maelezo
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman, ameutaka uongozi wa kituo cha kulelea watoto cha SOS, kuweka nia ya kushirikiana na serikali katika kuimarisha elimu.
Alisema serikali itatoa kila msaada unaohitajika kwa kituo hicho katika dhamira ya kuimarisha ushirikiano yatakayosaidia kuimarisha elimu nchini.
Akizungumza na ujumbe wa Shirika hilo ulioongozwa na Mkurugenzi Mkaazi Wilhelm Humber, Waziri Haroun alisema serikali inapenda kuliona shirika hilo linafungua vituo vya kulelea watoto kila Mkoa hapa Zanzibar.
Alisema kufunguliwa vituo hivyo kila mkoa kutaisaidia serikali katika kutoa fursa kwa watoto yatima, masikini na wanaoishi kwenye mazingira magumu kupata elimu na huduma nyengine.
Haroun alibainisha dhamira ya Serikali kuwa haina nia ya kuingilia utaratibu wa utendaji wa kituo hicho na inafarajika kukiona kikiendelea kutoa huduma kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Ujumbe huo wa SOS ulifika wizara ya elimu kuonana na waziri Haroun, kuomba ushirikiano na serikali hasa kupatiwa walimu kutoka serikalini ili waweze kujiimarisha zaidi kutoa elimu visiwani hapa.
Aidha hapo awali katika miaka ya 1980 na 1990 kulikuwepo na mashirikiano hayo ambapo yalikwama kutokana na dhana potofu ya uongozi wa kituo hicho wakati huo kuwa kuendelea na mashirikiano hayo Serikali ingewaingilia katika shughuli zao za utendaji.
Mkurugenzi huyo Wilhelm Humber alishtushwa na kusikitishwa na hali hiyo iliyojitokeza na ameahidi kufufua ushirikino na serikali kwa vile bila kushirikiana na serikali inakuwa vigumu kupata mafanikio.
Waziri Haroun aliuagiza uongozi wa kituo hicho kuandaa mikakati ikiwa ni pamoja na kuwa na vikao vya pamoja na watendaji wa Wizara ya Elimu ili kuepuka hitilafu zilizojitokeza hapo awali.
No comments:
Post a Comment