Wednesday 7 April 2010

Karume atembelea ujenzi Bodi ya Mapato Mbweni

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume jana alitembelea jengo la afisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), lililopo Mazizini na kusifu hatua ya ujenzi iliyofikiwa.

Rais Karume alitembelea jengo hilo na kupata maelezo ya kiufundi ambayo yameweza kumpa faraja kwa kuona juhudi zinazochukuliwa na kusifu mashirikiano yaliopo katika ujenzi huo.

Aliupongeza uongozi wa Bodi hiyo pamoja na Kampuni ya ujenzi ya China Railway Jianchang Engineering Co. (T) LTD, inayojenga jengo hilo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Meneja wa Kanda ya Zanzibar kutoka Kampuni hiyo, Xie ZhiXiang, alisema kwa mujibu wa mkataba, ujenzi huo unatarajiwa kumalizika mwezi Julai mwakani lakini juhudi zitafanywa na kampuni yake za kuhakikisha ujenzi huo unamalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Meneja ZhiXiang alisifu ushirikiano alioupata kutoka kwa uongozi wa Bodi ya Mapato na ule wa serikalini katika uendelezaji wa ujenzi huo.

Nae Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar Mohammed Hashim, alieleza kuwa ujenzi huo ni kwa ajili ya afisi za wafanyakazi wa Bodi hiyo ambapo pia imetengwa sehemu maalum kwa ajili ya afisi ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ambapo hadi kumalizika kwake kutagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 6.

Kamishna huyo alieleza kuwa kabla ya hapo ujenzi huo ulikuwa ufanyike hapo kilimani lakini haikuwezekana kutokana na ardhi ya eneo hilo na ndio maana ujenzi ukahamishiwa sehemu hiyo hivi sasa ambapo kwa hatua za awali jengo hilo litakuwa na ghorofa nne.

No comments:

Post a Comment