Tuesday 27 April 2010

Chanjaani walalamikia mavuno kidogo

Aisha Mohammed, Pemba
WAKULIMA wanaojishughulisha na kilimo cha mpunga bonde la Bundani katika shehia ya Chanjaani Wilaya ya Chake Chake Pemba walisema kilimo cha mpunga kinawakatisha tamaa kutokana na kupungua kwa mavuno siku hadi siku.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika bonde hilo walisema mavuno ya zao hilo yamekuwa yakipungua kwa kasi hali inayochangia kuwarudisha nyuma kimaendeleo.


Walisema wanajitahidi kulima zao hili ili kukuza kipato kitakachowawezesha kujikimu kimaisha na familia zao lakini wamekuwa wakivunjika moyo kuendelea na kilimo hicho.

Walifahamisha kuwa mbali na juhudi zao mavuno wanayoyapata hayasaidii hata kwa matumizi ya chakula seuze biashara.

“ Tunalima kilimo cha mpunga mwaka mzima lakini mavuno tunayoyapata hayatuwezeshi kupata hara chejio cha siku kumi 10”, walielezea wakulima hao.

Walifahamisha kuwa matayarisho ya kilimo hicho huanza mapema kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa kilimo lakini hawafaidiki na matunda ya kilimo hicho.

Walifafanua kuwa baada ya uvunaji wa kunde wanaendelea na kusia mpunga na kushughulikia mpunga huo hadi wanapofikia hatua ya mavuno.

Sambamba na hayo walisema mpunga huo unapofikia hatua ya kuvunwa huingiwa na wadudu na kupata maradhi hivyo mipunga huharibika na kupelekea kutozaa mazao bora, huku wakikabiliwa na ukosefu wa rutuba katika mabonde hayo.

Aidha wakulima hao wamelalamikia wizi wa mbegu za mpunga hali inayochangia upungufu wa mbegu hizo wakati wa msimu.

Pamoja na juhudi za kupambana na wadudu waharibifu wa mpunga wakulima hao wameiomba Serikali kuwapatia mbolea ili mashamba yao yaweze kuzalisha mazao kwa wingi na kuchangia juhudi za serikali za kupambana na umasikini kupitia sekta ya kilimo.

No comments:

Post a Comment