Thursday, 1 April 2010

Wanasiasa ndiyo chanzo cha vurugu nchini - Tindwa

Na Mwanajuma Abdi
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa, amewataka viongozi wa siasa kuacha kuchochea wananchi, akiweka wazi kuwa wao ndio chanzo kikuu cha migogoro, vurugu zinazotokea hapa nchini kwa maslahi yao binafsi na sio wananchi.

Tindwa ameeleza hayo alipokuwa akichangia Mswada wa sheria ya kuweka masharti ya kura ya maoni katika Baraza la Wawakilishi katika kikao kinachoendelea mjini hapa, ambao ulipitishwa jana.

Alidai kwamba wapo baadhi ya viongozi wa juu wa kisiasa wanahusika moja kwa moja kutokea kwa vurugu hizo, katika nchi kwa maslahi yao huku waathirika wakubwa ni wananchi.

Alisema vurugu hizo zinatokea sio bure lazima kuna mradi wa watu wamejiwekea ambapo zikitokea wao wanafaidika bila kuwajali wananchi wanaathirika kwa kiasi gani, sambamba na nchi kukosa utulivu na amani, jambo ambalo linachangia kushuka kwa uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Meja Mstaafu Tindwa, alieleza wakati unapofika uchaguzi Pemba kunakuwa hatari zaidi kila mmoja haamini akiwa huko, ambapo alisema fedha nyingi zinatumika kwa kutumia vikosi vya ulinzi vya SMZ, kuimarisha ulinzi kisiwani humo, ambapo ingekuweko amani zingetumika kwa miradi ya maendeleo.

"Siku moja nilikuwa nasali sala ya adhuhuri kwa wasiwasi katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, mara simu ikaita nikakata sala mbio kusikiliza simu kumbe Waziri Samia Suluhu akaniambia njoo upesi tutauliwa huku, nikatoka kufika njiani nakutana watu na mapanga tayari wanakwenda kuizunguuka nyumba, sasa haya tumeshachoka nayo", alieleza.

Aliwataka wananchi wasikubali kutumiliwa na wanasiasa kwa kusababisha vurugu na migogoro katika nchi kwani hawawatakii mema katika nchi, jambo ambalo linasababisha watu kuishi kwa kutoaminiana.

Alieleza kwa kipindi kifupi matokeo yameanza kuonesha kuna mafanikio makubwa, kwa vile katika zoezi linaloendelea la awamu ya pili, Wilaya ya Micheweni, Wete limemaliza kwa utulivu wakati mwanzo masheha walipigwa na kuchomewa nyumba zao moto na Tumbatu mwanamke alitolewa jicho lakini sasa mambo shwari.

Mkuu wa Mkoa huyo, alifahamisha kuwa, vyama vingi vimekuwa nuksi katika nchi ndio vimesababisha matatizo yote, ambapo mswada huo utasaidia kuwarejesha katika utulivu na amani na kuendelea kushirikiana katika maendeleo.

Alimsifu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume kwa kupewa uwezo na Mwenyezi Mungu kwa kupigania kuwepo kwa utulivu na amani nchini na kuwahimiza wananchi wasahau yaliyopita na wajenge Zanzibar mpya.

No comments:

Post a Comment