Tuesday, 20 April 2010

SMOLE kutumia Euro milioni 9 kupiga vita umasikini

Na Mwanajuma Abdi
MRADI wa Usimamizi Endelevu wa Ardhi na Mazingira (SMOLE II) umepanga kutumia Euro 9,000,000 katika kipindi cha miaka minne kutekeleza majukumu mbali mbali yaliyopangwa katika kupiga vita umasikini nchini.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Mradi huo Zanzibar, Saleh Kombo wakati akizungumza na gazeti hili mjini hapa.

Alisema mradi huo umepanga kutumia fedha hizo katika kutekeleza kwa vitendo majukumu yake kuhusina na usimamizi endelevu wa ardhi kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka huu hadi 2013.

Alieleza kuwa mradi wa SMOLE II, ni unaendeshwa kwa ushirkiano kati ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Mazingira na Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi na Serikali ya Finland kupitia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya nchi hiyo.

Mratibu huyo, alifahamisha kuwa, utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi chote cha miaka minne utafanyika kwa ushirkiano kati ya Idara tano zinazohusika na Ardhi, Mazingira na Maliasili, Idara hizo ni pamoja na Idara ya Upimaji na Mipangp Miji, Idara ya Ardhi na Usajili na Idara ya Utawala wa Ardhi.

Alizitaja Idara nyengine ni Idara ya Mazingira, Idara ya Mazao ya Biashara, Matunda na Misitu, mradi huo pia unaunga mkono malengo ya mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUZA II).

Aidha alieleza lengo kuu la SMOLE II ni kupunguza umasikini kupitia usimamizi endelevu wa ardhi na mazingira Zanzibar, ambayo yakisimamiwa ipasavyo itasaidia katika kupambana na umasikini nchini.

Hata hivyo, alisema mradi huo pia umekusudia kuzijengea uwezo taasisi hizo tano zinazotekeleza mradi wa SMOLE II ili ziweze kumudu majukumu yake kwa ufanisi zaidi.









No comments:

Post a Comment