Friday 23 April 2010

Changamoto za Muugano zifanyiwe kazi kuuimarisha

Na Halima Abdalla
PAMOJA na faida nyingi zinazopatikana katika Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar bado Muungano huo unakabiliwa na changamoto kadhaa zitakazoufanya uimarike zaidi.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Kikundi cha Wazanzibari wanaotetea Muungano, Rashid Yussuph, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari maelezo Rahaleo Mjini Zanzibar.

Katibu huyo alisema zipo kasoro kadhaa za Muungano ambazo leo hii zimegeuzwa na kuitwa kero ambapo kwa njia moja au nyengine zimekuwa zikiathiri maisha ya Watanzania.

Alifahamisha kuwa pamoja na Tume iliyoundwa na rais Kikwete ya kutatua kero hizo, bado tume hiyo haijafanyakazi ya kutosha katika kuzipatia ufumbuzi, jambo linalozua malalamiko kutoka kwa wananchi wa pande zote.

"Tume iliyoundwa haijaonesha uwiano utakaosaidia katika kutatua migogoro", alisema katibu huyo.

Katibu huyo alisema endapo kero za Muungano zitatakiwa zitatuliwe ni lazima serikali, iunde Tume itakayokuwa haijumuishi viongozi na watendaji wa Serikali.

Naye Amour Bamba, mjumbe wa kamati hiyo, alisema lazima pawe na mgawo wa haki sawa kwenye Muungano baina ya Watanzania wa Zanzibar na Watanzania bara.

Alisema matatizo mengi ya Muungano yanatokana na kutokuwepo usawa wa kiuchumi ndio maana yamekuwepo mawazo ya mmoja kunufaika zaidi ya mwengine.

''Kwa bahati mbaya tangu mwaka 1964 hadi leo watu wanazungumza kuhusu kero tu, hatujui lini kero hizi zitakwisha", alisema Bamba.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika Aprili 26 mwaka 1964, chini ya uasisi wa Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume ambapo mwaka huu unatimiza miaka 46.

No comments:

Post a Comment