Wednesday, 14 April 2010

Waziri Haroun aridhishwa na mchango wa FAWE

Yunus Sose,STZ
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imependekeza kuwepo kwa ushirikiano zaidi baina yake na Mtandao wa jumuia ya wanawake wasomi barani Afrika( Fawe- Zanzibar).
 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman, alisema mchango wa Jumuia ya Fawe Zanzibar, pamoja na mashirika mengine ya nje na ndani katika kumuendeleza mtoto wa kike unastahili kupongezwa kwani umekuwa ukitoa msukumo wa kuwaendeleza kielimu watoto wa kike.
 
Waziri Haroun alisema jitihada za kuwapa elimu ya sayansi watoto wakike ni miongoni mwa mkakati wa kumjengea uwezo motto huyo, katika kumudu maisha yake ya baadae.
 
Alifahamisha kuwa wizara yake imekuwa ikiridhishwa na mashirikiano mazuri yaliyokuwepo na Fawe Zanzibar, katika kusimamia masuala ya Elimu ya hasa kwenye kumuendeleza mtoto wa kike.
 
Waziri Haroun alitaja baadhi ya hatua iliyochukuliwa kwa pamoja kati ya wizara yake na Fawe Zanzibar, ni ushiriki wao katika programu za masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa kike, pamoja na kuanzisha kambi za sayansi zinazoandaliwa kila mwaka kwa lengo la kuwahamasisha wanafunzi hasa wa kike kuyapenda masomo ya sayansi na hesabati.

Kambi hizo ziliwashirikisha jumla ya wanafunzi wa kike 80 kutoka skuli za Unguja na Pemba na kuweza kutoa msukumo kwa wanafunzi hao na kuisaidia sana wizara ya elimu katika mpango wa kukuza na kuendeleza elimu.

Nae mratibu wa Fawe- Zanzibar, Asma Ismail alisema jumuia yake kupitia shirika la kimataifa la maendeleo la Marekani(USAID), imekuwa kitoa misaada mbali mbali ya moja moja katika masomo pamoja na vifaa kwa wanafunzi.
 

No comments:

Post a Comment