Saturday 24 April 2010

Kombo: Wekezeni katika elimu ya watoto wenu

Na Mwanajuma Abdi
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwekeza suala la elimu kwa mtoto ndio shabaha kubwa ya kumsaidia kuondokana na umasikini katika maisha yake na Taifa kwa ujumla.

Hayo aliyasema wakati akiwatunuku vyeti wahitimu 56 wa kidato cha nne na 38 wa kidato cha sita, kuwapa zawadi wanafunzi bora kitaifa kwa masomo mbali mbali na walimu wao wa masomo yaliyofanya vizuri likiwemo la Biology na Kiarabu, sambamba na kuzindua skuli ya maandalizi katika Sunni Madressa School, iliyopo Mkunazini mjini hapa.

Alisema elimu ndio kichocheo kikubwa katika kuleta mabadiliko ya kupambana na umasikini na ujinga katika Taifa lolote duniani.

Alieleza dunia hivi sasa imekuwa kama kijiji kutokana na kukua kwa mfumo wa sayansi na teknolojia ya mawasiliano ikiwemo internet, hivyo aliwashauri waitumie vizuri kompyuta katika kuwapatia mambo mengi yatayowawezesha kuwanyanyua katika taaluma yao kwa lengo la kujifunza zaidi.

Naibu Waziri huyo, alitoa wito kwa wanafunzi hao kujiendeleza kusoma zaidi ili baadae waweze kuwa viongozi wazuri wa taifa hili, ambapo asilimia 50 kwa 50 ya wanawake katika vyombo vya kutunga sheria katika Bunge na Baraza la Wawakilishi liweze kufikiwa wakati watakapomaliza masomo yao.

Aidha alisema mafanikio ya elimu hayatoweza kupatikana ikiwa wazazi na walimu hawatoshirikiana katika kuwahimiza wanafunzi kuwa na maadili mema na kujiamini wakati wowote, ambalo hilo tayari limeanza kuonekana kama wanafunzi wa skuli hiyo wana uwezo mkubwa wa kujiamini kwa kusimama mbele za watu.

Mapema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Jabir Makame wakati akimkaribisha Kombo, aliwaeleza wanafunzi hao wakati wa kusoma unajisikia shida kweli lakini faida yake unapomaliza na kupata kazi ndio unasahau matatizo yote uliyoyapata wakati unatafuta elimu, ambapo aliwashajihisha walimu na wazazi kuwatia moyo watoto ili wasome kwa bidii na faida wataiona baadae.

Nae Mkurugenzi Mtendaji Sunni Madressa School, Hussein Ali Suleiman alisema skuli hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, ambapo wanafunzi mwaka 2008 hadi 2009 wamepata sifa za kutoa wanafunzi bora Tanzania nzima katika masomo mbali mbali, sambamba na mwanafunzi Fatma Saad ametoa bora kwa kuzungumza kiingereza.

Nae Mwalimu Mkuu Rajab Mzee Wambi, aliwausia wanafunzi hao kujiepusha na masuala yasiyowahusu kama kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na mambo yanatowasababishia kupata virusi vya UKIMWI.

Mkuu huyo aliwapongeza walimu kwa kuwajibika ipasavyo katika majukumu ya kazi zao, ambazo zinachangia kuwasaidia wanafunzi kufaulu vizuri katika mitihani yao ya kitaifa, sambamba na wazee kutoa ushirikiano wa karibu katika uongozi wa skuli hiyo.

No comments:

Post a Comment