Tuesday 13 April 2010

Mawasiliano yazifutia leseni gari tisa kwa kupandisha nauli

Na Haji Nassor ZJMMC
WIZARA ya Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imezikamata na kuzifutia leseni gari tisa za abiria kutokana na kupandisha nauli.

Akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali afisini kwake Malindi Mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya madereva na makondakta kukamatwa kwa kosa hilo.

Alisema msako huo ambao ulifanywa hivi karibuni pia uliihusisha Idara ya Usafiri na Leseni, na gari hizo tayari zimefutiwa leseni na kusisitiza kuwa zoezi hilo litaendelea kwa kutumia mbinu mbali mbali ili kuwabana madereva na makondakta wenye tabia hiyo.

Aidha, Waziri Machano alifafanua kuwa Wizara yake wala taasisi nyengine yoyote haijatangaza bei mpya ya nauli na wanachokifanya madereva na makondakta ni kinyume na sheria za usafiri, na Wizara kamwe haitasita kumchukulia hatua za kisheria yeyote atakaekiuka utaratibu wa nauli.

“Hawa madereva na makondakta wanashangaza sijui hii amri ya kupandisha bei wamepewa na nani, maana sisi kama wadau wao wakuu hatujakaa nao kuzungumzia jambo hilo na sasa wanajiamulia wao wenyewe kupandisha bei, hili hatulivumilii’’, alifafanua Waziri Machano.

Katika hatua nyengine, Waziri huyo alisema hivi karibuni Chama cha wenye Daladala kilipeleka maombi Wizarani hapo kikitaka kupandisha nauli kutoka shilingi 300 ambapo Wizara haikukubali na imemuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Usafiri na Leseni, kuwataka wenye chama hicho kuwasilisha mchanganuo wao wa gharama ili kufikiriwa ombi lao.

No comments:

Post a Comment