Saturday, 10 April 2010

Mji Mkongwe waonywa kutumia magari kwenye mji

Na Mwanajuma Abdi
WAKAAZI wa Mji Mkongwe wa Zanzibar wameshauriwa kuacha tabia ya kutaka gari ziwashushe chini ya milango ya nyumba ili kuepusha uharibifu wa nyumba hizo.

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mwalim Ali Mwalim, wakati akizungumza na gazeti hili mjini hapa.

Alisema wananchi wamezoea kupelekwa na magari hadi chini ya milango ya nyumba zao, jambo ambalo linasababisha kero katika Mji Mkongwe, sambamba na kuzitia ubovu nyumba hizo kwa vile asili ya mji huo ilikuwa ni kwa watembea kwa miguu na sio magari.
 
Alieleza hivi karibuni alihudhuria mkutano wa Kimataifa wa dunia wa masuala ya Mji, ambao umewashirikisha wataalamu, wanasiasa na jumuia za asasi za kiraia juu ya kuilinda Miji, uliofanyika nchini Brazil, kuanzia Machi 22-26 mwaka huu.
 
Alisema katika mkutano huo changamoto mbali mbali zilitolewa jinsi ya kudumisha usafi na kuhifadhi takataka vizuri na masuala ya nishati.
 
Mwalim alifahamisha kuwa, kwa upande wa Zanzibar changamoto inawakabili katika mji huo ni hilo la uingiaji magari, kwa ajili ya kunusuru majengo hayo ya zamani kubakia katika uasili wake.
 
Akizungumzia gari makubwa yanayoingia kwa ajili ya kuchukua mizigo katika Bandari ya Forodha mchanga alisema bandari hiyo inahamia kwa muda pembezoni mwa bandari ya kuchukua abiria wa boti ziendazo kwa kasi ili kupunguza uingiaji wa gari kubwa katika eneo la Mji Mkongwe.

Alisema lengo kuu ni kuondoshea mzigo mji Mkongwe wa Zanzibar uingiaji wa gari kubwa kutokana mji huo kutomudu vishindo katika majengo hayo.

No comments:

Post a Comment