Saturday 24 April 2010

Wanafunzi wa kike waiomba FAWE iendelee kuwapiga jeki

Husna Mohammed
WANAFUNZI wawili wa Skuli ya Mwanakwerekwe ‘C’ Unguja, wameiomba Jumuiya ya wanawake wasomi Afrika kanda ya Zanzibar (FAWE), kuendelea kutoa misaada yao ya kielimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Wanafunzi hao Haitham Ali Khamis (17) kidatu cha tatu na Arafa Rashid Mohammed (17) kidatu cha pili, waliyasema hayo walipokuwa wakizungumza na gazeti hili wakati tofauti huko skuli ya Mwanakwerekwe ‘C’.

Walisema iwapo FAWE itaendelea na misaada yake hiyo hasa kwa mtoto wa kike, ni wazi watoto hao wataweza kupata wataalamu wazuri wa kike hapo baadae.

Walifahamisha kuwa, katika jamii hasa zinazoishi katika maisha duni kumekuwa na watoto wenye vipaji lakini wamekuwa wakishindwa kupata elimu kutokana na hali ngumu ya umasikini waliyonayo.

“Kama mimi nilikuwa katika hali mbaya kimaisha, lakini naishukuru FAWE, imeweza kuniinua na hivi sasa naendelea na masomo yangu hapa”, alisema Haitham.

Alisema hasa baadhi ya sehemu za vijijini kumekuwa na maisha magumu na hivyo baadhi ya watoto wamekuwa wakishindwa kupata elimu.

Kwa upande wake mwanafunzi Arafa Rashid, aliishukuru jumuiya ya FAWE kwa kuweza kumsaidia kielimu ambapo hivi sasa anaendelea vizuri na masomo yake.

Alisema FAWE iko katika mstari wa mbele katika kuwahakikishia elimu hasa kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika jamii.

“Naishukuru sana FAWE kama sio wao hivi sasa ningekuwa katika hali nyengine”, alisema.

Alisema FAWE imekuwa ikiwasaidia katika mahitaji mbalimbali ya kielimu ikiwa ni pamoja na kuwapa fedha za unifomu, madaftari, fedha za kujikumu na mambo mbali mbali yenye kuhusina na elimu.

Hata hivyo aliiomba FAWE kuiongeza jitihada zao hizo kwa lengo la kuziinua jamii masikini kwa msalahi yao na taifa.

No comments:

Post a Comment