Tuesday, 6 April 2010

Uongozi kutenda si maneno matupu – Mansoor

MWANAJUMA ABDI.
WAZIRI wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume hajauza nchi na badala yake kairudisha katika misingi ya ASP.

Mansoor alitoa kauli hiyo jana, katika sherehe za kukabidhiwa nyumba za fidia za waliovunjiwa nyumba zao kupisha ujenzi wa nyumba za maendeleo Michezani mjini Unguja.

Alisema Rais Karume hakuuza nchi,na alichofanya ni kairejesha katika misingi ya Chama cha Afro Shirazi ya kuwaletea maendeleo wananchi wake wote kwa vitendo.

Alimueleza Rais Karume kuwa ni kiongozi anayesimamia vizuri matumizi ya fedha za Serikali ili kuifanya nchi kuweza kujiendesha.

Alifahamisha kuwa wakati Rais Karume anaomba ridhaa ya wananchi kupewa madaraka kuongoza dola mwaka 2000 aliahidi kukamailisha ujenzi wa nyumba hizo.

Alisema ahadi hiyo ilipotekelezwa kwa vitendo imewezesha jana wananchi kushuhudia ugawaji wa nyumba hizo kuwafidia wanafamilia ambao zilikuwa bado wanadai.

Alisema pia Dk. Karume ameweza kufufua Mashirika ya Umma, likiwemo la Shirika la Umeme Zanzibar kwa kuweza kulipia gharama zote za matengenezo ya huduma ya umeme hadi kurudi katika hali yake kwa kutumia shilingi bilioni moja ambazo ni fedha za Shirika lenyewe.

No comments:

Post a Comment