Tuesday, 27 April 2010

Marufuku kuchimba mchanga kwenye fukwe - Mazingira

Mwanajuma Abdi na Maryam Ally (MSJ)
IDARA ya Mazingira Zanzibar imesimamisha uchimbaji wa mchanga wa pwani katika Hoteli ya kitalii ‘Uroa Bay Beach Resort’ iliyopo Uroa Wilaya ya kati Unguja.

Hatua hiyo inafuatia Mkurugenzi wa Mazingira, Ali Juma na watendaji wa Idara walipofanya ziara ya ghafla katika hoteli hiyo na kujionea chungu za mchanga pembezoni mwa fukwe hiyo.

Alimuagiza Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo, Mussa Durio Savio kuwa haruhusiwi kuchimba mchanga katika fukwe kwani kufanya hivyo anaharibu mazingira kukiuka sheria za nchi.

Alisema sheria za nchi haziruhusu kuchimbwa mchanga wa pwani kwa ajili ya kufanya ujenzi katika sehemu nyengine.

Alimueleza kwamba, kuanza jana hawaruhusiwi kuendelea na uchimbaji huo ambapo wakikaidi amri hiyo atawafikisha mahakamani.

Aidha alionya juu ya tabia ya baadhi ya wamiliki wa hoteli kuchimba mchanga kwa ajili ya ujenzi na kuwataka kuacha mara moja.

Alisema fukwe nyingi katika ukanda wa utalii zimekumbwa na mmong’onyoko wa ardhi unaosababishwa na uchimbaji mchanga katika fukwe, ukataji ovyo wa mikoko na kuongezeka kina cha maji ya bahari.

Meneja Mkuu wa hoteli hiyo, Mussa alikiri kuchimba mchanga huo kwa ajili ya kujaza katika maeneo mbali mbali ya Hoteli yake kutokana kujitokeza kwa mashimo yanayosababishwa na mawimbi ya maji ya bahari yanayopiga kwa kasi kubwa.

Alisema wamelazimika kujenga ukuta ili kusaidia hali hiyo, ambayo inayojitokeza kutokana na mawimbi ya maji ya bahari yanapojaa.

Aidha alifafanua kuwa, hoteli hiyo haijaanza kazi rasmi, ambapo wanategemea kuifungua Julai mwaka huu katika msimu wa utalii.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Mkurugenzi wa Mazingira Ali Juma, alikwenda katika kijiji cha Kiwengwa, ambapo ametoa wiki mbili kuondosha vigogo vya miti vilivyowekwa pembenzoni mwa fukwe kwa ajili ya kuzuia mawimbi ya maji ya bahari, sambamba na uchimbaji wa mchanga wa pwani.

No comments:

Post a Comment