Friday 2 April 2010

5357 wajiandikisha Mtambwe

Na Bakari Mussa, Pemba
WANANCHI 5357 wa Jimbo la Mtambwe, wamejiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura linaloendelea kisiwani Pemba.

Mwandishi wa habari hizi ameeleza kuwa kazi hiyo inakwenda kwa kasi sambamba na kutawaliwa na amani na utulivu licha ya wananchi wengi kuhamasika na zoezi hilo la marejeo baada ya awamu ya kwanza kutojitokeza katika vituo hivyo.

Habari zilizopatikana kutoka Afisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), zinaeleza kuwa katika wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wananchi wamekuwa na hamasa kubwa katika zoezi hilo tafauti na awamu ya kwanza ambapo waliojitokeza walikuwa wachache.

Kwa mujibu wa Afisa Uandikishaji wilaya ya Wete, Bakari Suleiman Ali ni kuwa kati ya wananchi waliojiandikisha katika Jimbo hilo wanawake walikuwa 2935 na wanaume 2422.

Zoezi hilo linaendeshwa kwa muda wa siku tatu katika Shehia sita zilizomo ndani ya Jimbo hilo.

Shehia ambazo ziliendesha zoezi hilo ni Mtambwe Kaskazini, Mtambwe Kusini, Piki A, Piki B, Kisiwani na Mzambarau Takao.

Kati ya Shehia hizo sita , iliyoongoza kwa kujitkeza Wananchi wengi kuliko zote ni ya Uondwe Mtambwe Kaskazini, ambapo jumla ya wananchi 1991, walijiandikisha katika zoezi hilo la marejeo.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Salim Abdalla Hamad, alieleza kuwa zoezi hilo kwa kiasi kikubwa limekwenda kwa vizuri kwani wananchi wote waliokuwa na sifa ya kuandikishwa walijiandikisha, isipokuwa wale ambao hadi sasa hawana sifa kamili za kuingizwa katika Daftari hilo.

No comments:

Post a Comment