Thursday 29 April 2010

Nungwi walia na mikataba mibovu mahotelini

Na Salum Vuai, Maelezo
WANANCHI wa kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamesema iwapo hatua za haraka kurekebisha mfumo wa ajira katika mahoteli hazitachukuliwa, sekta ya utalii haitakuwa na manufaa yoyote kwao.

Hayo yalielezwa na Sheha wa Shehia ya Nungwi Kombo Haji Mkuni kwa niaba ya wanakijiji hao, kwenye mkutano wa kutambulisha mpango wa kutoa mafunzo yahusuyo njia za kutumia utalii kwa ajili ya kupunguza umasikini mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mpango wa mafunzo hayo uliendeshwa na Jumuia ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), kwa ushirikiano na taasisi inayotoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo Tanzania ya TGT.

Sheha huyo alifahamisha kuwa, kutokana na kutofuatwa sheria na haki katika suala zima la mikataba ya uajiri, matatizo waliyonayo wanakijiji wa huko ya ukosefu wa ajira hayawezi kutatuliwa kirahisi kwa kuwepo utalii.

Alisema kwa inavyoonekana ajira chache wanazopewa wananchi wa hapo zinalenga kuwaonesha tu jinsi ya mahoteli yalivyo, na baada ya miezi michache wengi wao hufukuzwa bila sababu za msingi.

Alifahamisha kuwa mikataba mingi wanayopewa ni ya kulazimishwa kwani imebainika kuwa wengi wa wanakijiji wanaoajiriwa katika baadhi ya Idara zisizohitaji utaalamu mkubwa mahotelini humo, hutakiwa kutia saini katika mikataba bila kujua kinachoelezwa kuhusiana na kile wanachokisaini na kupata tamaa kuwa tayari wameajiriwa.

"Tumebaini kuwa wenye mahoteli wengi ni wadhalilishaji tu, hawazingatii haki za ajira, huajiri wapendavyo na kutimua wafanyakazi wanapojisikia kufanya hivyo na hawana mikataba ya hiari bali ni ya kulazimisha tu", alieleza kwa uchungu.

Kutokana na hali hiyo, Kombo alisema wafanyakazi wengi wanaofungishwa mikataba ya miezi sita huachishwa kazi bila kuambulia chochote na hawawezi kudai kwa kuwa ndani ya mikataba yao ambayo walisaini bila kujua, huoneshwa wazi kuwa ajira zao ni za muda huo.

"Ninapata kesi kama hizi lakini nikiuliza naoneshwa mikataba na kukosa pa kushika, mikataba kama hii si halali kwa kuwa inawafunga na hivyo kukosa haki stahiki pale waajiri wanapochoka nao", alisema.

Kombo alisema katika hali isiyotarajiwa, imewahi kutokezea katika hoteli moja kufukuzwa watu sitini kwa pamoja, akionesha mshangao wake kama wote hao walikuwa na makosa au walitimuliwa kwa utashi wa waajiri.

Alishauri kuwepo mikataba ya pande tatu itakayoshuhudiwa na maofisa wa Kamisheni ya Kazi, waajiri pamoja na mtu anayeajiriwa na nakala zake kugaiwa kwao kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ili kuepusha mchezo mchafu na kuwajengea kiburi waajiri wasiopenda kufuata sheria.

Aidha alitaka kabla kusainiwa kwa mikataba hiyo, wale waombaji kazi wasiojua kusoma wasomewe na kufahamishwa vyema kilicho katika mkataba ili kama wana hoja waulize na kujibiwa.

Katika hatua nyengine, aliushukuru uongozi wa ZATI na TGT kwa kuichagua Nungwi kuwa miongoni mwa vijiji vya kupewa mafunzo ya kazi za amali zinazoweza kuimarisha utalii, na kuwataka wanachama wa vikundi vya akinamama kufanya bidii ili wapige hatua na kujipatia ajira.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa maofisa kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na wakufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii cha Zanzibar kilichopo Maruhubi.

2 comments:

  1. ABA HOTELS - TANZANIA
    www.arushabudgethotels.com
    place to stay in Arusha
    US$15 per person sharing Bed& Breakfast
    contact us through reservations@arushabudgethotels.com
    or by phone; +255785989175

    ReplyDelete
  2. We have shift from Pangani to Market Street our newly building with very good facilities...
    contact us through +255788989175,
    www.arushabudgethotels.com

    ReplyDelete