Monday 26 April 2010

Sherehe za Muungano zafana

Na Rajab Mkasaba, Dar es Salaam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, leo ameungana na viongozi mbali mbali katika maadhimisho ya kutimiza miaka 46 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru mjini Dar-es-Saalam.

Katika sherehe hizo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrishso Kikwete.

Mara baada ya kuwasili Rais Kikwete katika uwanja huo ambao ulifurika maelfu ya wananchi kutoka sehemu mbali mbali za nje na ndani ya jiji la Dar-es-Saalam Gwaride lilitoa salamu ya Rais na Mizinga 21 ilipigwa.

Kamanda wa gwaride alimkaribisha Rais na Amiri Jeshi Mkuu kukagua gwaride na baada ya hapo gwaride lilipipita mbele yaa Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa mwendo wa pole na haraka na baada ya hapo gwaride lilisonga mbele hatua 15 na kutoa salamu ya za kutimiza miaka 46 ya Muungano.

Viongozi wa dini mbali mbali walisoma dua ya kuiombea nchi na kuomba kudumishwa kwa muungano na kuwatakia heri na fanaka viongozi na wanancho wote wa Tanzania katika maisha yao.

Kwaya na maonesho ya halaiki vyote kwa pamoja vilitumbuiza katika sherehe hiyo, jumla ya wanafunzi 700 kati ya hao 200 kutoka Zanzibar walishiriki halaiki hiyo. Pia, wanafunzi kutoka skuli ya Hazina walitumbuiza kwa kuonesha uwezo wao mkubwa wa kucheza sarakasi.

Vikundi maalum vya ngoma za asili kutoa Tanzania Bara na Zanzibar vilitumbuiza katika sherehe hizo ikiwemo ngoma ya nindo ngulilo kutoka Dodoma, ngoma ya Kibati kutoka Zanzibar, ngoma ya kubwaya kutoka Zanzibar na ngoma ya nyangira kutoka Shinyanga. Msanii maarufu Mrisho Mpoto (Mjomba) nae alitumbuiza.

Viongozi wengine wakuu waliohudhuria katika sherehe hizo ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Muhammed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuia Nahodha na Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ali Juma Shamuhuna walihudhuria.

Wake wa viongozi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwemo Mama Fatma Karume, Maria Nyerere, Shadya Karume na Mwanamwema Shein walihudhuria.

Katika sherehe hizo zenye kauli mbiu isemayo ‘Tudumishe Muungano Mhimili wa Taifa letu’ pia viongozi mbali mbali wa vyama na serikali zote mbili nao walihudhuria, Mabalozi wanaoziwakilishanchi zao na wananchi kutoka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar walihudhuria.

Aidha, Mzee Hassan Omar Mzee, Hadija Abass na Sifueli Shima, walioshiriki kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar miaka 46 iliyopita nao walitoa salamu katika sherehe hizo.

No comments:

Post a Comment