Thursday 22 April 2010

Bahari yaanza kumong’onyoa visiwa vya Zanzibar

Na Mwanajuma Abdi
KUFUATIA kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari duniani, kisiwa Panza Pemba, tayari kimekumbwa na athari za matokeo hayo kutokana na baadhi ya nyumba za wananchi na makaburi yaliyokuwemo katika pembezoni mwa bahari kufunikwa kabisa na kuwa sehemu ya maji chumvi.

Hali hiyo pia imejitokeza katika ukanda wa pwani kwa Unguja katika maeneo ya Jambiani nyumba za wakaazi zimepasuka na Michamvi baadhi ya hoteli zimekumbwa na mkasa huo.

Afisa wa Mazingira, Makame Machano Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili, mjini hapa, ambapo alisema hali hiyo imejitokeza kutokana kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari duniani.

Alisema kutoweka kwa baadhi ya eneo la kisiwa Panza kumesababisha baadhi ya mifupa ya miili ya binaadamu kukutwa ikielea katika maji kutokana kuchimbuka kwa makaburi hayo yaliyofunikwa na maji ya bahari.

Aliongeza kuwa, mifupa ya miili hiyo huchukuliwa na kuzikwa katika eneo jengine.

Alieleza kwamba, eneo hilo ukienda kuangalia hivi sasa huwezi kujua kama kulikuwa na nyumba za makaazi ya watu, sambamba na makaburi kwa vile limezungukwa na maji chumvi ya bahari.

Alifahamisha kuwa, athari zimeanza kujitokeza katika ukanda wa pwani karibu wote makaazi na hoteli ya kitalii zilikuwa karibu na fukwe kuharibika kwa kubomoka au kupasuka kutokana na mawimbi kuwa makubwa na yanakuja kwa kasi sana.

Afisa huyo, alisema hali hiyo inajitokeza kwa sababu mbali mbali ikiwemo ya kimaumbile, sambamba na kuongezeka kwa joto ulimwenguni, ambalo husababisha barafu kuyayuka na maji kuongezeka katika bahari.

Alitaja sababu nyengine inayosababishwa na binadamu wenyewe ni ukataji wa mikoko, uchimbaji wa michanga katika fukwe na kuvunja matumbawe, jambo ambalo mawimbi ya maji ya bahari yanapokuja kwa kasi yanakuwa hayana kizuizi na badala yake hutokea athari hizo.

Alieleza hivi sasa fukwe nyingi zimemong’onyoka kutokana na matatizo hayo, hivyo aliwataka wananchi waache tabia ya kukata mikoko, kuchimba mchanga wa pwani kwa shughuli za ujenzi na kuvunja matumbawe, kwani kufanya hivyo ndiko kunakosababisha athari kama hizo za kutoweka kwa nyumba na mambo mengine.

Hata hivyo, alisema athari nyengine inayojitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani visima vinavyochimbwa maji yake ni ya chumvi badala ya kupatikana matamu kama zamani, ambapo hata Mji Mkongwe wa Zanzibar umekumbwa na tatizo hilo.

Alifahamisha kuwa, visima vilivyochimbwa katika Mji Mkongwe wa Zanzibar maji yake yanapatikana ya chumvi, jambo ambalo kitaalamu linaonesha kuongezeka kwa kina cha maji chumvi athari zake zimeanza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment