Friday, 2 April 2010

Dk. Karume azindua matembezi ya UVCCM

Na Mwanajuma Abdi
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amewataka vijana kuendeleza fikra za muasisi wa mapinduzi ya Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kudumisha mshikamano, umoja, utulivu na amani katika kuleta maendeleo nchini.

Rais Karume aliyasema hayo jana, Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, wakati akizindua matembezi ya kumuenzi Muasisi wa Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, miaka 38 baada ya kifo chake, yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) yaliyowashirikisha vijana 150 wa Mikoa 26 ya Tanzania, ambapo matembezi hayo yatafanyika kwa mikoa mitatu ya Unguja kwa siku tano.

Mara baada ya uzinduzi huo Rais Karume aliongoza vijana hao na viongozi mbali mbali wa Chama, vyama vya upinzani na Serikali akiwemo Mke wa Muasisi Mama Fatma Karume, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Shadya Karume na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, katika matembezi hayo yaliyoanzia Makunduchi Kiongoni hadi Msikiti Mkubwa wa Makunduchi huku mvua kubwa ikinyesha.

Aliwaeleza vijana wayaenzi mafanikio hayo ya kudumisha umoja na mshikamano na watafautiane katika itikadi za siasa na sio kujengeana uadui kwa vile wote ni wamoja.

Rais Karume aliongezea kusema kijana wa CCM akivua sare ya chama chake na kijana kutoka chama cha upinzani CUF akivua sare yake, halafu wakae katika mkahawa akitokea mgeni atashindwa kuwatafautisha huyo wa chama gani, kwa vile wote ni ndugu.

Alisema mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anayekataa Umoja na mshikamano, huyo atakuwa siye kwa vile Chama hicho sera na ilani zake zote zinaeleza kudumisha mshikamano na kuweka amani na utulivu nchini.

Aliwaeleza kauli mbiu katika matembezi hayo, 'Vijana Tukithubutu Tunaweza', lengo limefanikiwa kwa vile matembezi hayo yamewashirikisha vijana wa CCM na bila ya kuwasahau vijana wenzao wa vyama vya upinzani (CUF) kwa kuwashirikisha, kwa vile suala la kuwaenzi viongozi linawagusa wote na maendeleo kwa ujumla bila ya kujali itikadi za siasa.

Mapema akimkaribisha Rais Karume, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa, Hamad Masauni alisema miaka 38 ya kifo cha Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kuna kila sababu ya kumuenzi kwa vile ni mkombozi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Alifafanua kuwa, fikra ya kuwaenzi waasisi imetokana mwezi Agosti mwaka jana, katika kikao walichofanya kisiwani Pemba, ambapo tayari wameshafanya matembezi kama hayo yaliyoanzia Mwanza hadi Butiama ya kumuezi Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambapo pia hivi karibuni wameshaingiza siku ya kumuenzi Marehemu Rashid Mfaume Kawawa.

Nae Katibu Mkuu wa Umoja Vijana Taifa, Shekela alieleza matembezi hayo yana lengo la kuthamini na kuelezea mchango mkubwa wa mwanamapinduzi huyo wakati wa uhai wake katika kuvikomboa visiwa vya Unguja na Pemba na kuleta maendeleo na kuasisi Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Alisema kutambua kwa hatua nzuri iliyofikiwa kati ya CCM na CUF katika kuwaletea maelewano wananchi wa visiwa vya Zanzibar ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa na mshikamano wa Wazanzibari.

No comments:

Post a Comment