Thursday, 29 April 2010

Uchambuzi wetu

Usikurupuke kuwania Urais
Na Ramadhan Makame
HUU ni mwaka wenye matukio yenye kusubiriwa kwa hamu, nikisema hivyo kila mmoja atakuwa analo lake lililomkaa kichwani.

Kwa upande wa wanamichezo hasa soka akili zao zitajikita kwenye fainali za kombe la dunia ambazo kwa mara ya kwanza zitapigwa barani Afrika, kule nchini Afrika Kusini.

Lakini kwa upande wa wanasiasa wao hasa Tanzania na Zanzibar, akili na fikra zao ni juu ya uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Naam! hayo ni matukio makubwa na kila moja lina msisimko wa aina yake, lakini kwenye waraka huu mfupi acha tuogelee japo kidogo kwenye siasa hasa tuwazungumzie wale wanaojiita wana nia za kugombea.

Vyama vimepuliza mazumari huku michakato ya kuwapata wagombea ikipita kwenye hatua na njia tofauti baina ya chama kimoja na chengine.

Pamoja na kutofika rasmi wakati wa kampeni lakini ni dhahiri kila anayetaka kugombea kwa wadhifa ambao amejipangia ama kwa hiari au kushawishiwa ameshaanza kampeni.

Hii inaashiria hali ya uchaguzi mkuu mwaka huu utakavyokuwa mgumu sio kwa wale wenye kutetea nafasi zao, bali hata kwa hao wapya wanaojiandaa kuingia kwenye mchezo huo usiotabirika.

Michakato ya vyama hivyo kwangu mimi hainishughulishi wala hainibabaishi, ila kinachonipa shida hao watu watakaoshinda michakato na hatimaye kupewa tiketi za kugombea na vyama vyao.

Najua kwa njia moja ama nyengine na wakitaka wasitake vipo vyama vitakosea kutupatia wagombea wenye kuhitajiwa na wananchi kwa maslahi ya maendeleo yao.

Wagombea wa namna hii watapenya kwa sababu mbali mbali zikiwemo kuonewa huruma na vyama kutokana na pengine michango yao ya kifedha wanayoitoa, pengine uzuri wa ukoo wa mgombea, uzuri wa sura zao, rangi zao, historia zao na kadhalika.

Sidhani kama wakati mwengine ni vyema vikatumika vigezo kama hivyo, nafikiri vyama viwe makini na kuongozwa na sifa moja kuu nayo ni je! mgombea huyu waliyempata anakubalika na wananchi?

Kwa mfano hivi sasa kuna mchakato wa chinichini wa kumtafuta mrithi wa Dk. Amani Abeid Karume atakayewania kiti cha Urais wa Zanzibar.

Katika hili kuna majina kadhaa wa kadhaa kupitia vyama kadhaa wa kadhaa yanatajwa kuwa yatachukua fomu za kuwania kiti hicho.

Ninalotaka kusema mimi ni dogo nalo ni kabla ya mgombea kuchukua fomu ajiulize jamii ya kizanzibari inamuonaje! na sio kufuata mkumbo wa wapambe ambao baada ya uchaguzi ambao hudoea nafasi za bure (political opportunist).

Ni vyema mgombea akajitathmini na kujihakiki vya kutosha kwenye nafsi yake na kujipa jibu sahihi kabla ya kuwauliza watu wenye hekima na busara, chonde chonde mgombea usikurupuke kwenda kuwauliza wapambe.

Katika kujihakiki na kujitathmini huko ni vyema pia ukaliangalia vyema suala zima la imani yako thabiti mbele ya Wazanzibari na jinsi unavyoguswa na maisha yao ya kila siku.

Jiulize pia ulipokuwa kiongozi aidha iwe ngazi ya chini, kati na hata ile ya juu, lipi la kujisifia mbalo wewe binafsi umewahi kuwasidia Wazanzibari sio familia yako wala ukoo wako, kwenye shida zao.

Suali jengine je! umejipima kiwango chako cha ubinafsi ulionao kwenye moyo wako? na ulipokuwa kiongozi wa ngazi yeyote ile hapo awali, Wazanzibari wangapi uliwanyima haki zao huku ukiwa unajua kwa yakini kwamba ile uliyowanyima ni haki yao.

Ningependa pia mgombea ujiulize je! unayajua mahitaji (intrests) ya Wazanzibari katika kipindi hichi na umejiuliza nini wanakitaka na nini hawakitaki na utawasaidia je?

Suala hili ni la msingi kwa maana mahitaji ya Wazanzibari katika miaka ya 1960 ni tofauti sana na kipindi hichi, hofu yangu usijekuwa na mawazo mgando ukadhani Wazanzibari wa miaka ile ndio wale wale na wanahitaji mambo yale yale ya kale.

Kama una mawazo ya aina hiyo utakuwa umekosea sana, mimi nastahiki kukuita wewe ni mvivu wa kufikiri na ni mvivu wa kusoma alama za nyakati ambapo kwa wanasiasa maradhi haya ni ya kawaida.

La mwisho nakukumbusheni wagombea kuwa Wazanzibari wa sasa hawahitaji rais bubu, atakayekuwa anabana midomo kimya sio wa kuongea wa kuwatetea wananchi kwenye dhiki zao mbali mbali.

Tulia mgombea usipandwe na hasira juu ya masuali haya, huu ni waraka niliyoupa jina la muongozo wangu kwa kiongozi ajae, si kwa maslahi yangu bali ya Wazanzibari wote.

Kwa hisia zangu, mgombea yeyote asiyeweza kuyafuata yaliyokuwemo kwenye muongozo huu, ni vyema akajitoa mapema na tena fomu aiogope kama ukoma.

Wakatabahu naomba kutoa hoja!

No comments:

Post a Comment