Thursday, 29 April 2010

1943 waliambukizwa VVU mwaka jana

Na Jamila Abdallah, Pemba
WAKAAZI wapatao 1934 wa Zanzibar walijitokeza kuchunguzwa damu zao katika vituo vya afya Zanzibar na wamegundulika kuwa na Virusi vinavyosababisha UKIMWI ambao ni miongoni mwa wakaazi 69,749 waliojitokeza kupima virusi vinavyosababisha UKIMWI mwaka jana.

Akitoa takwimu hizo Daktari wa Hospitali ya Chake Chake, na mjumbe wa mradi wa Uzazi wa Mpango na Malezi Bora Tanzania (UMATI ), Ali Shamte, alisema kati ya waliojitokeza kupima kwa hiyari wapo wanawake 33,096 kati yao 1,168 sawa na asilimia 3.5 waligundulikana na virusi vinavyosababisha UKIMWI.

Alisema kwa upande wa wanaume waliojitokeza kupima ni 36,653 sawa na asilimia 2.1 kati yao 756 waligundulikana wameathirika na virusi na 164 waliopima katika vituo tofauti walikataa kutajwa wanapokaa miongoni mwao 10 walikutwa na VVU ambao ni sawa na asilimia 6.1.

Takwimu hizo zilitolewa mara baada ya kumaliza kutoa mada katika mafunzo yaliyotolewa na wajumbe wa mradi wa DARAJA kwa baadhi ya wazazi na walezi,viongozi wa dini ,Masheha na walimu ma Skuli na Madrasa za wilaya ya Chake Chake Pemba.

Mradi huo wa DARAJA una lengo la kujenga mawasiliyano yanayoaminika baina ya mzazi mwema au tegemeo kwa vijana, yaani daraja kwa lengo la kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

Dk. Ali aliendelea kufafanua zaidi kwa kusema DARAJA ni kiunganishi na ni sababu ya kujifunza kuhusu mawasiliano kati ya mzazi mwema na vijana katika afya ya uzazi, kama vile magonjwa ya ngono, VVU, UKIMWI na mimba zisizotegemewa.

Akitaja baadhi ya malengo ya DARAJA Ali Shamte alisema kwanza kujilinda mwenyewe dhidi ya maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa.

Pia DARAJA imedhamiriya kujenga mawasiliano nyeti baina ya mzazi tegemeo na kijana na kuwasaidia vijana kuimarisha malengo binafsi na ndoto za kimaisha pia kubuni mipango ya kutimiza malengo hayo.

Naye mzazi, Saleh Hassan Suleiman, wakati akichangia mada alisema,``jambo kubwa linalosababisha kupanda kasi waathirika wa gonjwa la UKIMWIimwi ni zinaa ambayo inasababishwa na jamii kutofuata maamrisho ya dini zetu”.

Kwa upande wa mzazi wa kike Amina Said Ali alichangiya kwa kusema kuwa akina baba waachane na tabia ya kuwatupia mzigo wa ulezi wazazi wa kike tu bali washirikiane kwa kila hali katika kujenga familia bora na zenye maadili mema.

Amina, pia alisema wazazi kwa wakati huu wanalazimika kuwa wa wazi kwa vijana wao katika kuwapa elimu na kuwaeleza juu ya athari na madhara ya ugonjwa huo na wakae na familia zao na kuwaeleza ukweli juu ya hali ya ukimwi inavyotisha na kuongeza siku hadi siku.

No comments:

Post a Comment