Na Halima Abdalla
ZAIDI ya kesi 229 ya udhalilishaji wa wanawake na watoto zimeripotiwa katika kituo cha huduma za sheria Zanzibar (ZLSC), mwaka 2009.
Kati ya kesi hizo, udhalilishaji wa wanawake majumbani zilizoripotiwa kwenye kituo hicho ni 93 kwa Unguja na Pemba.
Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kituo cha huduma za sheria Zanzibar, Is-shak Ismail Sharif, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema katika mwaka huo, kesi zinazohusiana na udhalilishaji wa watoto zilizoripotiwa kituoni ni 57 na kesi zilizoripotiwa kwa wasaidizi wa kisheria Unguja ni 50 kwa upande wa Unguja. huku wasaidizi wa Pemba wakiripotiwa kesi 29.
Is-shak alisema kesi hizi zilizoripotiwa za watoto zinahusiana na unyanyasaji wa watoto, ubakaji, kuingiliwa kinyume na maumbile pamoja na aina nyenginezo za udhalilishaji.
Alisema kesi hizi za udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa mwaka uliopita zimeonekana kuongezeka ikilinganishwa na mwaka 2008 ambazo zilikuwa chini ya hapo.
Alifahamisha mara nyingi malalamiko hayo yanapofika kituoni hapo, huwasilishwa polisi ambapo huingilia kwa kuzikwamua pale zinapokwama.
Aidha, alisema ikitokea kesi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa njia ya mauaji huwa wanaipeleka moja kwa moja katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka.
''Kama kesi ya mauaji huwa tunaipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka", alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa jamii kuachana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto kwani kufanya hivyo ni kinyume na haki za binadamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment