Monday, 12 April 2010

Nahodha awataka Wazanzibari kufanya maamuzi sahihi

Abdalla Ali, AWK
WAZIRI Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha amewahimiza wananchi wa Zanzibar kufanya maamuzi yatakayo endeleza amani na utulivu nchini.

Nahodha alisema hayo katika mahojiano maalum kati yake na Mwandishi wa Habari, Antar Sangali wa Redio Uhuru.

Alisema amani na utulivu ndio utaoharakisha maendeleo na uelewano nchini kama iliyvodhihirika kipindi kifupi tokea Rais Dk. Amani Karume na Maalim Seif Sharifu kufanya mazungumzo yaliyomaliza tofauti na mivutano ya kisiasa nchini.

Nahodha alisema ana matumaini kwa viongozi wa CCM hawatokuwa wa mwisho kuunga mkono suala hilo kwa kuwa amani na utulivu ndio Sera ya chama hicho.

Kuhusu ushughulikiaji wa matatizo ya Muungano, Waziri Kiongozi, alisema kuwa matatizo hayo yamegawika katika sehemu mbili kubwa mbazo ni Fedha na Biashara na hivyo yanahitaji mfumo maalum au fomula ili yaweze kutatuliwa kwa ridhaa yapande zote mbili.

Alisema tayari Tume ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshawasilisha ripoti yake katika Serikali za pande zote za Muungano kwa mapitio ili mgawanyo wa mapato ufanyike kwa faida ya pande zote mbili jambo ambalo litawezesha ufanisi wa ufumbuzi wa matatizo hayo kwa zaidi ya asilimia 60.

Akijibu suala kuhusu hali ya Zanzibar itavyofaidika na Soko la Jumuia ya Afrika Mashariki, alisema changamoto zipo katika utaalamu na mitaji maeneo ambayo yanaweza kukwamisha biashara.
 
Hata hivyo, alisema Zanzibar inaweza kufaidika kama itakuwa na viwanda vidogo vidogo vya samaki na maabara za kuchunguza bidhaa hizo zitazosafirishwa nje ya Jumuia hiyo.

No comments:

Post a Comment