Saturday, 3 April 2010

‘Hongereni kwa kuwaandalia mazingira bora kielimu watoto’

Na Rajab MkasaWAZEE, walimu na wananchi wa Shumba Mjini, Wingwi na Pondeani kisiwani Pemba, wamepongezwa kwa juhudi zao zinazolenga kuwapatia watoto elimu itakayowakomboa katika maisha yao na kuleta maendeleo kwa taifa.

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amewapongeza katika ziara yake ya siku mbili kiswani Pemba alipovitembelea vijiji hivyo na kuweka mawe ya msingi na kuzindua madarasa ya skuli ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.
 
Akizungumza na wananchi hao kwa nyakati tafauti, Rais Karume alisema wazo la wananchi, wazee na walimu wa vijiji hivyo la kuendeleza miradi ya elimu kwa kujenga madarasa ya skuli ni la busara kwa mustakabali wa maisha yao na kuahidi kuungwa mkono na serikali ya Mapiduzi Zanzibar.

Rais Karume aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi ya kuwasogezea wananchi wake huduma muhimu za maendeleo Unguja na Pemba, ikiwemo miundombinu ya barabara, mawasiliano, afya, elimu, maji safi na salama, huduma ya umeme na nyenginezo ambapo kisiwa cha Pemba karibuni watapata umeme wa uhakika.

Alieleza kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kusambaza umeme vijijini ambapo hatua kubwa imeshafikiwa na kutoa shukurani kwa wananchi wa kisiwa cha Pemba kwa uvumilivu wao wa huduma hiyo ya umeme iliyopo sasa sambamba na kujituma katika kujiletea maendeleo endelevu.
 
Rais Karume alisisitiza kuwa kutokana na mafanikio yaliyofikiwa Zanzibar hali hiyo imewapelekea hata Washirika wa Maendeleo kuweza kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo.

Kutokana na hatua hiyo, Rais Karume aliwasisitiza wanafunzi wa skuli zilizopo katika vijiji hivyo kusoma kwa bidii ili wapate kufanikiwa kwani tayari mazingira mazuri wameshawekewa na wazee wao, walimu na serikali kwa jumla.

Alieleza kuwa kwa upande wa serikali tayari imeshajenga skuli za sekondari, vyuo vikuu na kuahidi kuwa iwapo watafaulu zaidi serikali itawasomesha katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.
 
Pamoja na hayo, Rais Karume alizisifu Kamati za Skuli zilizopo katika vijiji hivyo, kutokana na kazi nzuri wanazozifanya ambazo zimeonesha maendeleo katika sekta ya elimu na sekta nyenginezo na kuwahakikishia kuwa majengo yao waliyowakabidhi Wizara ya Elimu kutokana na hatua ya ujenzi ilipofika yatamalizwa na kuwekwa samani.
 
Akiwa katika skuli ya Pondeani baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo lenye vyumba vinne, ikiwemo chumba cha maabara na cha Kompyuta, Rais Karume alitoa pongezi kwa Wizara ya Elimu kwa kwa kujenga madarasa ya skuli ya chekechea.



No comments:

Post a Comment