Wednesday 7 April 2010

Watanzania wauombea Dua Marehemu Karume

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Amani Abeid Karume, ameungana na viongozi wa dini, vyama vya siasa na serikali na wanachi mbali mbali katika hitma ya kumuombea dua Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo pia ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, viongozi wastaafu, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi, wakuu wa Mashirika pamoja na Mabalozi wadogo kutoka nchi mbali mbali waliopo hapa Zanzibar.

Awali hafla hiyo ilitanguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na Sheikh Jafar Rashid na kuongozwa na Sheikh Mohammed Kasim kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar.

Aidha, mara tu baada ya hitma hiyo Alhaj Sheikh Mussa Salum kutoka Mkoa wa Dar es Salaam alitoa mawaidha na kusifu juhudi kubwa zilizochukuliwa na marehemu Sheikh Abeid Amani Karume katika uongozi wake wote ikiwa ni pamoja na kusimamia Mapinduzi yaliyowakomboa wananchi wa Zanzibar na hatimae kujiletea maendeleo.

Sheikh Mussa alieleza kuwa kuna kila sababu ya kumkubuka marehemu mzee Abeid Karume kutokana na mema mengi aliyoyafanya na kuwafanyia wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Alisema kuwa mara zote , Mzee Karume alikuwa akisisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukiendelezwa na viongozi wote wa Tanzania hadi hivi leo.

Sheikh Mussa alieleza kuwa Dk. Amani Abeid Karume ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye ni mtoto wa muasisi huyo wa Mapinduzi ameweza kuendeleza maendeleo makubwa ambayo misingi yake imewekwa na Mzee Abeid Karume ikiwa ni pamoja na ukamilishwaji wa nyumba za maendeleo Michenzani na miradi mengine ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, mawasiliano, elimu, afya sanjari na demokrasia iliyo imara.

Alieleza kuwa ikiwa ni miaka 38 tangu kifo cha Mzee Karume Zanzibar na Tanzania kwa jumla imeweza kushuhudia maendeleo makubwa kutokana na juhudi za viongozi wake ambao wamekuwa wakifuata nyayo za mzee Karume akiwemo Rais Amani Abeid Karume na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika Aprili saba kila mwaka , viongozi hao na wananchi walimuombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui iliyoongozwa na viongozi wa dini mbali mbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Aprili 7, 1972 ndio siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini.



No comments:

Post a Comment