• Watakiwa kutowaachia suala hilo wanasiasa pekee
• Muungano uimarishwe kwa kutatuliwa kwa vitendo kero
Na Mwanajuma Abdi
WAANDISHI wa Habari Zanzibar, wametakiwa kuungana pamoja katika kuibua mambo muhimu kwa maslahi ya Zanzibar na Taifa hili katika kutatua kero za Muungano na sio kuwaachia wanasiasa pekee.
Kauli hiyo imetolewa na washiriki wa kongamano la siku moja la mchango wa waandishi wa habari katika kustawisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililoandaliwa na Jumuiya ya Kuwaendeleza Waandishi wa Habari Wachanga Zanzibar (ODEYJO), lilifanyika katika Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar, Vuga mjini hapa.
Katika kongamano hilo mada mbili ziliwasilishwa, ikiwemo Mchango wa waandishi wa Habari katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao unatimiza miaka 46, iliyowasilishwa na Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Abdulla Mohammed Juma na Changamoto kwa wanahabari wa Zanzibar katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliwasilishwa na Mwandishi wa Habari Muandamizi, Rashid Omar.
Walisema waandishi wa habari wakiiungana pamoja itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo yanayoikabili Zanzibar likiwemo la kero za Muungano, kwa maslahi ya wananchi wa chini na sio maslahi ya viongozi peke yao.
Walieleza kero za Muungano zimekuwa zikizungumzwa juu juu na Serikali na wanasiasa mezani bila ya kushirikishwa ipasavyo vyombo vya habari, jambo ambalo uwakilishi wa wananchi wa chini unakosekana kufikishwa taariza zao.
Aidha walifahamisha kuwa, kero nyingi za Muungano zinazozungumzwa ni maslahi ya wakubwa na Serikali lakini watu wa chini hawaguswi, ambao ndio wanaoumia zaidi likiwemo suala la kupandishiwa bei kwa vitu mbali mbali kutokana na wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akichangia mada hizo, Mwandishi wa Habari Muandamizi, Enzi Talib Aboud alisema waandishi wa habari hawana umoja katika kusaidiana kuondosha kero mbali mbali zinazoikabili Zanzibar, ambapo suala la Muungano nalo limekuwa watu wakipiga kelele za mdomo mtupu.
Alifafanua kuwa, kero za Muungano zinashindwa kutatuliwa kutokana na watu wanapinga kelele, ambapo wanapokwenda Tanzania Bara viongozi wetu wanashindwa kutokana hawazungumzi kisheria wao wanabakia katika kupiga kelele.
Alieleza masuala yanayoigusa Zanzibar kimaslahi moja kwa moja wananchi, waandishi wa habari na wanasiasa waweke nyuma tofauti zao na kinachobakia mbele ni kuungana kwa maslahi ya Taifa, ambapo katika Bunge wa Jamhuri ya Muungano Tanzania wapo wajumbe wa CUF ni bora wawe wanaungana na wanaCCM wa Zanzibar katika kuzuia miswada ya kisheria inayoibana Zanzibar ili isipite kwani ikishapita ndio matatizo yanaongezeka.
Nae Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Ali Vuai alisema kero za Muungano haziwezi kutatuliwa na kamati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa SMZ, katika meza lazima masuala hayo yarejeshwe katika vyombo vya kutunga sheria Bunge ili kupatikana kwa theluthi za wajumbe juu ya utatuzi huo.
Alisema kero za Muungano hizo zimeanza muda mrefu, ambapo pale Zanzibar ilipotaka kujiunga uanachama wa Jumuiya ya OIC, ambapo ikakataliwa na Jamhuri ya Muungano Tanzania, sambamba na Jumuiya ya Afrika Masharikiri kuingia moja kwa moja na badala yake iingie kupitia Serikali ya Tanzania.
Mwandishi wa Habari kutoka Idara ya Habari Maelezo, Salama Njani, akichangia mjadala huo alisema vyombo vya habari bado havina uhuru wa kutosha katika kuandika na kufichua uovu unaendelea kutokea na kujitokeza siku hadi siku, hususani vyombo vya Serikali vinabanwa katika kuibua mambo ambayo yanakiuka katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo likiwemo hilo la kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mapema Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti la Serikali Zanzibar, Abdulla Mahammed Juma aliwasilisha mada juu ya mchango wa waandishi wa habari katika kuimarisha Muungano huo, alisema habari nyingi zinazoandikwa ni za upande mmoja wa muungano huvutia kwake, ambapo wale wa Tanzania Bara kinachozungumzwa na viongozi wa Zanzibar dhidi ya Muungano ndiyo huwa habari na wale wa Zanzibar nao hutumia hicho kama habari muhimu kwa maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano huo.
"Hali hii kwa kweli kwa kiasi kikubwa inadhoofisha muungano kwa wanahabari kutumika katika kuonesha zaidi upande mmoja ambao mara nyingi huwa Zanzibar kuonekana unachafua au kupinga muungano wakati pengine vyombo au waandishi hao vingeweza kuonesha kwamba Zanzibar inadai haki na fursa zake ndani ya muungano na kuchangia uimarikaji wake", alisisitiza Abdulla.
Alisema wengi wanathubutu kusema kuwa matatizo ya muungano yameanza tokea unazaliwa ambapo hapakuwa na uwazi kuhusiana na mipaka yake na maamuzi ya upande mmoja wa muungano huo ambao ni Zanzibar, unaoelezwa kwamba muafaka ulikosekana katika Baraza la Mapinduzi kuhusiana na kuunganisha nchi hiyo.
"Baada ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar na muasisi wa Muungano huu, Marehemu Mzee Abeid Karume, ambae alizieleza wazi kero za muungano na kuzikataa wazi wazi kasoro za Muungano, kasoro hizo zilikuwa zikiogopwa hata kuzungumzwa na aliyejaribu kufanya hivyo alitiwa muhuri wa uchochezi na wengine wamepoteza ajira zao", alieleza.
Alisema kutokana na kasoro hizo Zanzibar imepoteza utaifa, kutotambulikana kimataia kwa mfano UN, Jumuiya ya Madola na AU, pia imepoteza hadhi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuundwa kwa Benki Kuu ya Tanzania ambayo haina maslahi na Zanzibar, japokuwa mtaji wake ulitumika kupitia Bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki kuanzisha benki hiyo.
Alifahamisha kuwa, makubaliano ya awali ya Muungano yalikuwa ni mambo 11 lakini sasa yamefikia 22, hivyo kunaonesha dhahiri kuna ujanjaujanja unafanyika, ambapo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania sehemu ya kwanza ibara ya tisa kifungu cha 34 (1) Rais wa Tanzania atakuwa na mamlaka ya mambo ya muungano na mambo yahusuyo Tanzania Bara, jambo ambalo linaikosesha haki Zanzibar ya kumpata mdau waliyeungana nae miaka 46 iliyopita.
Alileleza kwamba, wakati kifungu cha 34 (2) na (3) kinaeleza kwamba iwapo Rais wa Jamhuri wa Muungano hayupo nchini atakaimiwa na Makamo wa Rais kama hayupo Spika wa Bunge kama hayupo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
"Sehemu ya pili inayohusiana na Makamu wa Rais nayo pia ina kasoro tokea Rais wa Zanzibar kufutiwa fursa ya kuwa makamu wa Rais moja kwa moka kama iliyvokuwa katika makubaliano ya kwanza ya Muungano wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere.
Mhariri Mtendaji huyo, alisema mchango wa wanahabari ni muhimu katika kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar, bila ya kukubali kuambukizwa jazba za wanasiasa, wanahabari wajifunze kwa kuongeza uelewa wao katika kuwasaidia watanzania.
Akizungumzia hatma ya muungano, Mhariri huyo alisema ili uimarike ni lazima serikali mbili zilizouanzisha ya Tanganyika (Tanzania Bara) na Zanzibar zikae tena kufikiria muundo mpya wa muungano ambao utapunguza malalamiko ya upande mmoja kunung’unika au kumezwa.
Pia alisema kutokana na mabadiliko ya ulimwengu na kukua kwa demokrasia, suala la kufanyika maamuzi ya wananchi kuhusu muungano huu sasa limefikia wakati wake, ambapo njia muafaka ni kutumia kura ya maoni kama zinavyofanya nchi nyengine duniani, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekwa hadharani mkataba wa muungano ‘articles of union’ ambao unaaminika kuwa umeelekeza mambo mengi ambayo hadi sasa hayajafanyika.
Nae Rashid Omar Mwandishi Mwandamizi, akitoa mada alisema changamoto za kimtizamo wa itikadi za vyama baadhi ya wanahabari kuzungumza Muungano kwa uwazi linamshabaha sana na itikadi za vyama vya siasa, kutokana na hali hiyo baadhi yao wameamua kukaa kimya ama kuwa na kigugumizi na huku wengine wakijaribu kuandika makala na kutayarisha vipindi vyenye mtazamo wa kutetea zaidi kuliko uhalisia, ambao wananchi wanapaswa kupatiwa kupitia juhudi za vyombo vya habari.
Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi wa Vijana, Mohammed Salim aliipongeza Jumuiya ya ODEYJO kwa kufanya kongamano hilo, ambalo linakwenda na wakati katika shamra shamra za kilele cha maadhimisho ya miaka 46 ya Muungano huo tokea Aprili 26, 1964.
Alisema kongamano hilo litajadili mafanikio yaliyofikiwa na Muungano huo kwa lengo la kuimarishwa zaidi na matatizo yaweze kujadiliwa na kuondosha ili uweze kuwepo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema changamoto kubwa zinazowakabili waandishi wa habari waache tabia ya kuandika habari za uchochezi zinazosababisha migogoro katika nchi na badala yake waandike habari zenye kuleta umoja na kudumisha utulivu na amani nchini.
No comments:
Post a Comment