Wednesday, 21 April 2010

Pride yaanguka kimikopo

Na Fauzia Muhammed
SHIRIKA la Mikopo la Tanzania (PRIDE) tawi la Zanzibar limesema kwamba wateja wanaochukuwa mikopo ya fedha katika shirika hilo wamepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na siku zilizopita.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa PRIDE tawi la Zanzibar Omar Juma Omar, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi Afisini kwake Mlandege, Wilaya ya mjini Zanzibar.

Alisema kuwa wateja hao wamepungua kutoka 4,000 hadi kufikia 2000 na kwamba hali hiyo inapunguza ufanisi wa shirika hilo ambalo wakopaji wake zaidi ni wanawake.

Omar alifahamisha kuwa upungufu huo umetokana na mzunguko wa pesa Zanzibar kuwa mdogo ambao ulianza mara baada kukosekana umeme.

Alisema pamoja na umeme huo kurejea hali ya mzunguuko wa pesa haijarejea katika hali ya kawaida na hivyo kulifanya shirika lake kuwa katika wakati mgumu.

Hata hivyo, Omar alisema kuwa shirika hilo bado linaendelea na utaratibu wa utoaji mikopo kwa wazalishaji wadogo wadogo bila ya kuathiriwa na taasisi nyengine zinazotoa mikopo zikiwemo benki.

Alisema kuwa Shirika lake ni miongoni mwa Mashirika makubwa yanayoendesha shughuli hizo kwa uzoefu na kwamba halina masharti makubwa yatakayopelekea wateja kutochukua mikopo.

No comments:

Post a Comment