Wednesday 21 April 2010

Sheria mpya biashara kuondoa urasimu

Na Suleiman Almas
WADAU wa taasisi zinazotoa na kuchukua mikopo wameshauri kuangalia umuhimu wa kujisajili ili kuweza kuendesha shughuli za biashara katika hali ya uhakika na usalama kwa raslimali zao.

Wakizungumza katika semina ya utoaji wa elimu kuhusu sheria mpya ya usajili wa biashara, katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Chavda, mjini Unguja, walifahamisha kuwa iwapo sheria hiyo itapitishwa na kutekelezwa itasaidia kupunguza urasimu katika shughuli za kibiashara zikiwemo za kutoa na kuchukua mikopo.

Wadau hao ambao wametoka katika taasisi mbalimbali za kifedha na kibiashara waliupokea ushauri huo kwa kuzingatia kuwepo kwa usalama wa kile wanachokitoa na kuhakikisha mteja anaeshirikiana nae kupata taarifa zake sahihi bila ya kujificha.

Aidha walifahamisha kwamba utaratibu wa kibiashara uliopo hivi sasa ni wa kuaminiana zaidi kwani bila kuwepo uhakika wa kikundi au hata mtu binafsi anaechukua mkopo kupata taarifa zake sahihi na inapotokea udanganyifu unakuwa ni vigumu kumnasa.

Nae mwendesha mafunzo hayo katoka Norway, John Olaisen, alieleza kuwa mabadiliko ya sheria katika masuala ya usajili wa biashara utaweza kusaidia kujenga imani kwa wakopeshaji na kuweza kutoa mitaji kwa wateja wao bila ya kuwa na wasiwasi kutokana na kuweko kwa uwazi wa taarifa za wahusika.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya mafunzo hayo, Msaidizi Mrajis wa Serikali Abdulbaq Ali, alisema rasimu hiyo ya mabadiliko ya sheria itakuwa katika maeneo matatu, ambayo ni sheria mpya kuhusu usajili wa biashara, rehani kwa mali zinazohamishika na rasimu ya sheria ya kufilisi.

Ali alifahamisha kwamba, sheria iliyopo ni ile ya dikrii nambari 168, inayohusisha usajili wa majina ambayo nayo inahitaji kufanyiwa marekebisho.

Alisema, Afisi ya Mrajis Mkuu wa serikali hivi sasa inatumia sheria nambari 153, ya mwaka 1952 ya usajili wa makampuni hadi hapo itakapopitishwa sheria hiyo mpya ya usajili wa biashara, rehani na kufilisi.

Kutokana na hali hiyo baada ya mapitisho ya sheria hiyo taasisi zote za kifedha na zile za kibiashara zitakuwa zikifanya kazi kwa ukaribu zaidi na Afsi ya mrajis mkuu wa Serikali kwa kupokea taarifa mbalimbali za wateja kupitia mawasiliano yao.

Katika mafunzo hayo taasisi zilizoshirikishwa ni pamoja na Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ), Exim Bank, NMB na NBC.

Nyengine ni Umoja wa watu wanaoishi na ulemavu (UWZ), ANGOZA, ZAAA na Jumuia ya wakulima na wenye viwanda (ZNCCIA).

Mafunzo hayo yameendeshwa chini ya usimamizi wa Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali kwa mradi unaodhaminiwa na Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania (MKUMBITA).

No comments:

Post a Comment