Tuesday 6 April 2010

EU yaridhishwa na mradi wa WEZA

Na Mwanakhamis Mohammed
BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) Tanzania, Jim Cleark, amefahamisha kuwa Jumuiya anayoiongoza imekubaliana na Mawaziri wa Tanzania katika sera mpya ya kusaidia wanawake katika kujiletea maendeleo.

Alisema, wanawake wengi wana mwamko wa kujiletea maendeleo ila uwezo wao ni mdogo na kuwa wanahitaji nyenzo ili kufikia azma hiyo.

Balozi Cleark alisema hayo huko Mzuri Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja alipokuwa katika ziara ya kuvitembelea vikundi vya kuwawezesha wanawake vya mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi (WEZA).

Alisema, mpango wa wanawake wa kujiwekea akiba katika vikundi ni njia mojawapo ya kujikwamua kiuchumi, kwani vikundi hivyo vimekuwa vikitoa mikopo midogo midogo inayotumiwa na wanawake hao kuanzishia biashara.

Alieleza kuwa mradi wa WEZA umebadilisha maisha ya wanawake kwa kujiwekea akiba kitu ambacho hapo awali hawakuwa wakikifanya.

Aidha alifahamisha Jumuiya imefanya mazungumzo na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa lengo la kuendeleza shughuli za kujiletea maendeleo.

Balozi Clerk ameelezea kuchukizwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia pamoja na vitendo vya ubakaji na kuahidi kuwa yupo tayari kuzisaidia Jumuiya na Taasisi zinazoshughulikia masuala ya sheria ili kupambana na vitendo hivyo.

“Tayari tumeshafanya mazungumzo na TAMWA ili kuangalia ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia wanawake katika kujiletea maendeleo”, alieleza Cleark.


No comments:

Post a Comment