Monday 12 April 2010

Waislamu endelezeni utajo wa Mwenyezi Mungu

Na abdi Shamnah
NAIBU Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna, amewataka waislamu nchini kuendeleza utamaduni wa kumtaja na kumsifia kwa wingi Mtume Muhammad (SAW), ili kuwarithisha watoto wao ibada hiyo.

Shamuhuna alisema hayo jana huko Mwera, Wilaya ya Pangani katika hafla ya Maulidi ya Mtume Muhammad (SAW) yaliyosomwa na waislamu wa kijiji hicho, kusherehekea uzawa wa mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu.

Akizungumza na waislamu hao, Shamuhuna aliwataka kuwarithisha watoto wao kumtaja kwa wingi na kumsifia Mtume kwani kuna fadhila kubwa ndani yake.

Katika hatua nyingine, Shamuhuna alisema mbali na Watanzania kujivunia umoja, udugu na mshikamano uliopo umeimarisha Muungano, pia alisema uislamu umekuwa ni kiungo muhimu na kushauri kubadilishana mialiko ya maulidi katika dhana ya kuuenzi Muungano.

Aidha aliwapongeza waislamu wa Mwera kwa mwamko walionao katika kusherehekea uzawa wa Mtume, kwa kuwashirikisha waislamu wa jinsia na rika tafauti ikiwemo wazee, vijana, wanawake na watoto.

Alisema hatua hiyo ndio jibu la pekee dhidi ya baadhi ya waumini wenye itakadi ya kuyaona maulidi kuwa ni bidaa.

Akitoa ‘daawa’ katika hafla hiyo, Sheikh Othman Maalim alisema waislamu wana kila sababu ya kumsifu kwa sifa njema Mtume Muhammad (SAW), kwa kigezo kuwa hata Mwenyezi Mungu amemsifia katika kitabu chake kitakatifu cha Quraan.

Alisema historia inaonesha kuwa maisha na tabia ya mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu kuwa ndio chimbuko la ustaarabu, hivyo aliwataka waumini kudumisha amani na usalama kwani ndivyo vinavyoweka mazingira bora katika utekelezaji wa ibada.

Maulid hayo ya kusherehekea uzawa wa Mtume Muhammad (SAW) yalifanyika katika mji mdogo wa Mwera na kusimamiwa na Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) wilaya ya Pangani.





No comments:

Post a Comment