Friday 23 April 2010

Uchaguzi mkuu 2010 wagombea wawindana 'kumfuata babu'

Na Mwantanga Ame
VITUKO vya imani za ushirikina kwa baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi za Uongozi uchaguzi Mkuu ujao, vimepamba moto baada Mwakilishi wa Pemba kulisukua ndumba la chupa ya damu mlangoni mwa nyumba yake.

Tukio hilo limetokea wiki iliopita huko kisiwani Pemba baada ya Mwakilishi huyo (jina linahifadhiwa) ambaye ni kijana mdogo, kuelezea Zanzibar Leo kukutwa na tukio hilo huko nyumbani kwake kati ya Majimbo yaliomo katika Mkoa wa Kaskazini.

Mwakilishi huyo alisema aliikuta chupa ya ndumba hiyo iliyozikwa katika mlango wake wa mbele wakati akilima kwa lengo la kupunguza majani nyumba kwake.

Mwakilishi huyo anaeishi na familia yake alieleza kuwa alishangazwa na tukio hilo baada ya jembe alilokuwa akilimia kugonga chupa hiyo na kulazimika kuita jamaa zake kuwafahamisha mkasa huo.

Alieleza kuwa baada kuifahamisha familia hiyo yeye binafsi halikumpa mshtuko kutokana na familia yake kumpa moyo kwa kuitisha kisomo cha Kur-ani ghafla na baadae kuendelea kuisukua chupa hiyo ya ndumba iliyozikwa ardhini.

Alieleza kuwa, baada ya kusukuliwa chupa hiyo ambayo hutumiwa kuwekea maji ndani yake waliikuta ikiwa na damu inayosadikiwa kuwa ni ya binadamu, vipande vya memo ya mnyama pamoja na vipande vinne vya nyama.

Kutokana na kukutwa vitu hivyo, Mwakilishi huyo alisema familia yao ilivichukua na kumruhusu yeye binafsi aivunje chupa hiyo kwa jembe alilokuwa akilitumia kwa kulimia na kisha kuichoma moto.

Alifahamisha kuwa tangu akutwe na mkasa huo ana mashaka makubwa waliotenda hilo ni kati ya wagombea wenzake waliojitokeza kuchukua fomu kwa Chama cha CUF kwa vile wapo waliomtishia na hilo.

Alisema usiku wa kuamkia siku hiyo ilinyesha mvua kubwa ikiambatana lakini walisikia kuwapo kwa vishindo, lakini familia yake haikuvitilia manani kwa kuona ni nguvu ya mvua.

Kwa mujibu wa Mwakilishi huyo, alifahamisha katika Jimbo ambalo yeye anaendelea kulishikilia tayari waliojitokeza kuwania nafasi ya Uwakilishi kwa hivi sasa wamefikia wagombea wanane huku nafasi ya Ubunge wakiwa ni 18.

Alieleza suala la ushirikina kwa wanaotaka kugombea nafasi mbali mbali katika uchaguzi mkuu ujao, hivi sasa lipo kwa kiasi kikubwa ambapo wengi wa waganga wanaona ni njia moja wapo ya kunufaika huku wengine wakishindana kupata waganga wakali zaidi.

Alisema hilo linajionesha baada ya kujitokeza kwa baadhi ya wagombea kuwahamishia waganga hao majumbani mwao huku wengine wakiwatoa nje ya Zanzibar.

Alifahamisha hivi sasa wapo watu wameamua kuwapa nyumba watu wanaosadikiwa kuwa ni waganga wa kienyeji kutoka sehemu mbali mbali ikiwa ni lengo la kupiga kambi kwa muda ili wafanye shughuli zao za biashara kwa msimu huu wa Uchaguzi.

“Hapa wapo wa kisiri siri wanatoka nje ya Zanzibar sijui wa Sumbawanga hawa ama Nigeria sijui hata wametokea wapi nasikia wapo” alisema Mwakilishi huyo.

Alifahamisha wengi wa wagombea hao wanaonekana kutojiamini kuingia katika mchakato wa uchaguzi ujao bila ya kutumia waganga huku wengine wakitoa hata vitisho vya kuwang’oa kwa kutishia maisha.

Hata hivyo, Mwakilishi huyo alisema licha ya kukutwa na mkasa huo bado hajavunjika moyo wa kuendelea na mchakato huo na atahakikisha kuwa anafanikiwa kuibuka kidedea katika kura za maoni.

Alisema hilo anaamini kuwa litatokea kutokana na kuweza kufanikisha mambo kadhaa ya maendeleo katika Jimbo analoliongoza huku bado akiwa na ushawishi kutoka makundi tofauti.

Wakati hilo likiwa kwa Upande wa Pemba wagombea walioonesha nia katika majimbo ya Unguja nao wanalilalamikia hilo kutokana na baadhi yao kukutwa na mikasa ya aina hiyo.

Akisimulia mmoja wa watu wenye nia ya kuwania nafasi ya Ubunge kwa Jimbo la Rahaleo, ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema yeye binafsi alipatwa na maradhi ya kupooza viungo vya miguu na kumlazimu kutibiwa kwa siri na familia yake kwa muda wa wiki mbili.

Alisema alipatwa na hali hiyo wakati akiwa nyumbani kwake jambo ambalo liliifanya familia yake kuzuiya kuonana na mtu yoyote wakati akiwa matibabuni jambo ambalo alieleza ugonjwa huo ulimshangaza.

“Bwana ushirikina upo na unafanywa kweli kweli mimi binafsi ndio nimeanza kutoka nje sasa nilikuwa siinuki wiki mbili nilikuwa ndani miguu hii nilitiwa kama nanga na viungo vikubwa unavyolemazwa mikono na miguu” alisema Mgombea huyo.

Alifahamisha kubwa zaidi wakati akiwa matibabuni mmoja jamaa yake anayejishughulisha na kazi za tiba ya jadi alifuatwa na mtu kutaka amsaidiea dawa ya kukatisha maisha yake lakini jamaa yake huyo alikataa kwa vile hakufahamu kama anauhusiano naye na ndie aliyeshiriki kumtibu wakati alipokutwa na tatizo hilo.

Kutokana na hali hiyo Mwanachama huyo alieleza hivi sasa tayari ameweza kupata matibabu na amerudi katika hali yake ya kawaida na kueleza kuwa ushirikina upo wa hali ya juu katika mbio hizo.

“Mie nasema kinywa kipana kweli ushirikina unafanywa mimi yamenikuta na hivi nimetoka matibabuni kwani kinanishangaza hata simu zangu zilizimwa watu wananambia sipatikani wakati ilikuwa wazi na hili sio langu pekee yangu katika Jimbo hilo yupo na mwengine sasa hivi mkono umeshapooza” alisema Mwanachama huyo.

Mwanachama mwengine ambaye nae ameonesha nia ya kugombania katika Jimbo la Jang’ombe, alidai suala la kutumia imani za ushirikina hivi sasa lipo kubwa na tayari limeanza kuwaandama wanaoonekana nyota zao kung’ara katika majimbo wayotaka kugombea.

Mwanachama huyo alidai kuwa hali hiyo tayari imeshamkumba mmoja wa wagombea hao kwa kupooza viungo vya miguu na mikono ambapo hivi sasa tayari familia yake inaendelea kumpatia matibabu.

Wakati hilo likitokea katika Jimbo la Jang’ombe, tukio jengine linadaiwa kutokea katika Jimbo la Fuaoni, ambapo mmoja wa waonesha nia ya kugombea katika Jimbo hilo amejikuta kukutwa na masahiba ya kuvunjwa nguvu za kupoteza kumbu kumbu kila anapojaribu kutaka kuzungumzia azma yake.

Mmoja ya wanachama wa CCM, alidai kuwa inasikitisha kuwapo kwa vituko hivyo ambavyo vinaonekana kutishia maisha kwa waonesha nia pamoja na kujawa kwa ghofu ya kupoteza maisha.

Alisema sehemu kubwa ya matatizo yanayoendelea kuwapa kwa imani hizo za kishirikina hivi sasa wengi waliokutwa na masahiba hayo wamepoozeshwa viungo vya miguu na mikono.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo tayari Tume ya Uchaguzi hivi sasa imo katika matayarisho mbali mbali.

No comments:

Post a Comment