Saturday 3 April 2010

Mwanafunzi azimia masaa tisa

Na Jumbe Ismaily, Singida MWANAFUNZI wa kidato cha pili skuli ya sekondari ya Ilongero, wilaya ya Singida vijijini, Ajira Mohamedi, amelazwa kwenye kituo cha afya Ilongero baada ya kuzimia kwa saa tisa kufuatia kipigo alichopata kutoka kwa baba yake mzazi.


Mwenyekiti wa kamati za huduma za jamii wa kijiji cha Ilongero, Adija Majii alisema tukio hilo lilitokea Machi 30 mwaka huu majira ya saa 12 jioni.


“Niliitwa jana kwamba mtoto amepigwa nikaenda tukatafuta gari tukampeleka hospitali na alikuwa amezimia, tukaenda kuripoti polisi na baadaye baba yake akaenda kukamatwa”, alifafanua Majii.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo vipigo hivyo vimekuwa vikitokea mara kwa mara kwenye familia hiyo kwa kumpiga mkewe na siku nyingine mtoto na kwamba kitendo cha mwanafunzi huyo kupigwa hadi kuzimia ni cha pili.

Hata hivyo, Majii aliweka wazi sababu za mwanafunzi huyo kupata vipigo hivyo ni mwanafunzi huyo kutakiwa kwenda madrasa kusoma elimu akhera badala ya kuendelea na elimu dunia.

“Na hiki ni kipigo cha mara ya pili hadi kuzimia mtoto huyu anasoma kidato cha pili, lakini hata hivyo mwanzo alipofaulu babake alikuwa hataki kabisa aende shule tukamlazimisha na Mtendaji na Mwenyekiti ndipo mtoto akaenda kuripoti shuleni kwa kuchelewa”, alisisitiza kiongozi huyo.

Aidha alitoa wito kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuwachukulia hatua wazazi wa aina hiyo wanaowazuwia watoto, husunani wa kike kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

Kaimu afisa mtendaji wa kata ya Ilongero, Hamisi Malongo, alikiri kupokea taarifa na alipokwenda kwenye tukio alimkuta mtoto huyo akiwa na hali mbaya.

No comments:

Post a Comment