Thursday 1 April 2010

Simo kinyang’anyiro cha Urais – Dk. Mwinyihaji

Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, anaeshughulikia Fedha na Uchumi Dk. Mwinyihaji Makame, amevunja ukimya kwa kutangaza hadharani hana nia ya kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi Mkuu ujao.

Dk. Mwinyihaji aliyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akichangia mswada wa kuunda sheria ya kuiruhusu Tume ya Uchaguzi kuendesha kura ya maoni katika ukumbi wa Barzaa la Wawakilishi Mjini Zanzibar.

Waziri huyo alisema ameamua kuelezea suala hilo baada ya kuwapo kwa tetesi hizo lakini yeye hana nia hiyo bali atabakia kuwania Jimbo analolitumikia sasa la Dimani.

Hatua ya Waziri huyo ilikuja baada ya kuelezea kuwa nia yake kuwania Jimbo la Dimani kutokana na kudai kuwa ana uhakika wananchi wa Jimbo hilo wataweza kufahamu uamuzi wa serikali katika kuweka kura ya maoni itayokuja baadae.

Matamshi ya Waziri huyo yalisababisha baadhi ya Wajumbe wa baraza hilo kumhoji baada ya kumtumia ujumbe mfupi uliokuwa ukimuuliza kama kweli anaendeleza nia yake hiyo ya kuwania Jimbo huku nafasi ya Urais kama ni basi.

“Kuna mtani wangu mmoja hapa ameniletea ujumbe hapa baada ya kusema kuwa nitagombea tena Jimbo langu la Dimani na ataekuja nitapambana nae sasa ananiuliza jee ile nafasi ya Urais basi tena” alisema Waziri huyo.

Waziri huyo amekuwa akijumuishwa na viongozi kadhaa wa CCM Zanzibar kutaka kuwania nafasi hiyo, katika uchaguzi Mkuu ujao akiwemo Naibu Waziri Kiongozi wa Zanzibar Ali Juma Shamuhuna, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud, Waziri wa elimu na Mafunzio ya Amali Haroun Ali Suleiman.

No comments:

Post a Comment