Wednesday, 21 April 2010

Wananchi wapinga ujenzi eneo la wazi Mchangani

Na Salum Vuai, Maelezo
WAKAAZI wa Wadi ya Mchangani mjini Zanzibar, wamesema wallazimika kuchukua hatua ya kuvunja uzio wa mabati uliozungushwa katika eneo la wazi lililopo pembezoni mwa jengo la Makao Makuu ya Kkampuni za Mfanyabiashara, Said Bakhresa.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo taarifa kuwa kuna mfanyabiashara mmoja maarufu aliyepewa eneo hilo ambaye anakusudia kujenga nyumba ya ghorofa tano, huku wananchi hao wakisema wanahitaji kulitumia kwa michezo ya watoto.

Mvutano ulioanza kujichomoza hapo uliwafanya wakaazi hao wa jinsia na rika tafauti kupinga ujenzi huo unaokusudiwa kufanyika kwenye kiwanja hicho, huku wakizungumza kwa hasira na waandishi wa habari waliofika kushuhudia kadhia hiyo.

Miongoni mwa wananchi waliojitokeza katika eneo hilo ni pamoja na Diwani wa Wadi hiyo, Ahmed Salum Ahmed, ambaye alisema hakuwa na taarifa zozote kuhusu eneo hilo kupewa mtu kwa ajili ya ujenzi na kukanusha kwa maelezo kuwa yeye ‘amekula’ fedha zozote kutoa baraka za kujengwa nyumba hiyo kama baadhi ya watu wanavyodai.

Alifahamisha kuwa, alipopata taarifa siku mbili nyuma kabla kujengwa uzio huo, alimuuliza Injinia wa Manispaa ya Zanzibar ambaye alisema eneo hilo keshapewa mtu anayekusudia kuliendeleza.

“Mimi nikiwa Diwani wa hapa, sina mkono wangu katika hili,lakini nimeambiwa eneo hili kapewa Bwana Jaku Hashim na ndiye aliyejenga uzio huu”, alisema.

Alieleza kuwa awali, vijana wa wadi hiyo walikusudia kuuvunja uzio huo kabla lakini kwa kutumia busara yeye pamoja na wazee wa mtaa waliwazuia lakini siku iliyofuata watu wote wakaungana kwa dhamira ya kuonesha kupinga kugaiwa kwa eneo hilo.

Naye Diwani wa zamani katika Wadi hiyo Ali Awadh, alisema katika miaka ya 2000 wakati akiwa Diwani, alikuwa na mpango wa kukitengeneza kiwanja hicho na kuweka pembea, mradi ambao ungefadhiliwa na Wajerumani, lakini ukaishia hewani kwa sababu zisizojulikana.

“Hili ni eneo la wazi na tunajua serikali imetoa agizo maeneo kama haya yasivamiwe kwani ili kuwapa fursa watoto kucheza na kufurahi, sasa kila pahala tutataka kujenga, wanetu wacheze wapi?” alifafanua na kuhoji.

Zahra Salum, Salma Magram na Attiya Ali Magram, wote kwa pamoja waliweka msimamo wa kutokubali eneo hlo kujengwa nyumba bali liachiwe kwa ajili ya watoto.

“Hatuko tayari kuruhusu ujenzi wowote hapa ambao hautawahusisha watoto, viwanja vyote vya wazi lazima viheshmiwe sio kila mwenye fedha azioneshe kwa kuinua maghorofa”, walibainisha kwa umoja wao.

Naye Abdallah Suleiman Ali (Mrusi), ambaye alikuwa mmiliki wa pili wa eneo hilo baada ya mtu aliyekuwa akilimiliki awali Edi Mbaraka kufariki dunia, alisema hatua za makabidhiano kati yake na Jaku yalifanyika kisheria kwa kupitia ngazi ya mahakama, na kwamba haoni ubaya wowote kujengwa kwani hayo ni maendeleo.

Sheha wa Shehia ya Mchangani Nassir Mohammed Ali, alisema hakuna ombi lililopita kwake kuhusiana na ujenzi wa uzio huo wala kinachokusudiwa kujengwa baadae, lakini anayo nakala ya barua kutoka Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe inayoonesha kuwa Jaku ameruhusiwa kulitumia eneo hilo.

Sheha huyo alionesha nakala ya barua hiyo kwa waandishi ambayo iliandikwa tarehe 25 Machi, mwaka huu ikiwa na kumbukumbu namba MHUMM 156 VOL. XIX/2010/964 iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Issa Sariboko Makarani kwenda kwa Jaku Hashim Ayoub.

“Mamlaka inatoa ruhusa ya awali kuzungushia uzio wa mabati eneo hilo kwa upana wa mita 1 na sentimita 70 kutoka kwenye mzunguko wa mpaka wa kiwanja hicho baada ya kuridhika na vibali vyako,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Alipoulizwa Mkurugenzi huyo, alisema Jaku anavyo vibali kutoka Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi vilivotolewa miaka kumi iliyopita kumruhusu kulitumia neo hilo.

Hata hivyo, Makarani alieleza baada ya kuridhika na vibali hivyo, Mamlaka yake haiwezi kumzuia kujenga lakini lazima azingatie masharti ambapo hatakiwi kujenga majengo ya ghorofa au nyumba ya makaazi ya watu, bali ajenge maduka ya chini.

Hata hivyo, jitihada za mwandishi wetu kumtafuta mtu anayedaiwa ndiye mmiliki wa eneo hilo hazikuweza kufanikiwa.

No comments:

Post a Comment