SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema juhudi mbali mbali zimefanyika kwa kushirikiana na wadau tofauti wa ndani na nje ya nchi na kufanikiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa ugonjwa wa Malaria Zanzibar na kufikia chini ya asilimia moja.
Kaimu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Asha Abdallah Juma aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari, alipozindua wiki ya siku ya maadhimisho ya Malaria Duniani, ambapo kilele chake kitakuwa Aprili 25 mwaka huu.
Alisema, maadhimisho ya siku ya Malaria duniani kitaifa kwa nchi zote za Bara la Afrika mwaka huu, yataadhimishwa Tanzania katika Mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar itashiriki kikamilifu, ambapo pia Zanzibar kila Wilaya imepatiwa nafasi ya kuadhimisha siku hiyo kwa ngazi za shehia kwa ushirikiano wa kitengo cha Malaria.
Alisema ujumbe wa maadhimisho hayo mwaka huu, 'Maliza Malaria Zanzibar', ambao unawakumbusha wananchi kuwa hali ya ugonjwa huo imepungua kwa kasi kubwa hadi kufikia chini ya asilimia moja, kutokana na mikakati iliyopangwa na Wizara hiyo kupitia kitengo chake cha Malaria kufanikiwa.
Alisema katika miaka ya nyuma ugonjwa huo ulikuwa unasumbua jamii kwa zaidi ya asilimia 40, sambamba na kupoteza pato kubwa la familia, Serikali na Taifa kwa ujumla.
Aliwashajiisha wananchi kuondosha mazalio ya mbu katika maeneo wanayoishi, pia kutoa ushirikiano wa dhati wakati wa zoezi la upigaji dawa majumbani linapoendelea na kutumia dawa kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa afya.
"Napenda kutoa tahadhari kwamba ugonjwa bado upo na hasa ikizingatiwa vyanzo vya upatikanaji wa maradhi hayo vipo na mbu wapo katika visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo wananchi tutumieni vyandarua vilivyowekwa dawa wakati wa kulala", alisisitiza Waziri Asha.
Kwa mujibu wa Takwimu za ripoti za kitengo cha Malaria Zanzibar zinaonesha wagonjwa 2,437 waliofika katika Hospitali mbali mbali Unguja na Pemba, kwa ajili ya kesi za malaria kwa mwaka jana kati ya hao 33 ndio waliobainika kuugua Malaria, sawa na asilimia 1.4 na watu 27 wakiwemo watoto na watu wazima walifariki kwa ugonjwa huo, idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na miaka ya nyuma.
No comments:
Post a Comment