Thursday 22 April 2010

11 wajitokeza kugombea Uwakilishi Fuoni

Na Hashim Mlenge
KATIBU wa Umoja wa vijana wa CCM Jimbo la Fuoni, Abubakar Ali Hamdan ‘Abuu’, ametangaza nia yake ya kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kiti cha Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia tiketi ya chama hicho ndani ya Jimbo hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Abuu alisema nia yake ya kujiingiza katika kinyang’anyiro hicho uchaguzi ujao ni safi na kwamba sio mipango ya kupiga kampeni.

Alisema licha ya kuwa yeye ni miongoni mwa vijana wadogo ambae ameamua kuitaka nafasi hiyo, lengo lake ni kuwaletea wananchi wa Jimbo la Fuoni maendeleo.

“Nimeamua kuwania nafasi hii kwa sababu nina kila sababu ya kuwania, kwani nina nia, uwezo wa kuongoza na pia ni haki yangu kikatiba”, alisema.

Alieleza iwapo atafanikiwa kuchaguliwa atahakikisha Jimbo hilo linakuwa mstari wa mbele kimaendeleo kutokana na juhudi atazozichukua huku akishirikiana na wananchi wa Jimbo hilo pamoja na viongozi watakaokuwepo ili kuhakikisha wanaondoa kero zinazowakabili wanajimbo.

Abuu ni miongoni mwa wagombea 11 walioonesha nia ya kujitokeza kuwania kiti hicho.

No comments:

Post a Comment