Thursday, 6 January 2011

VYUO VYA AMALI MSINGI KUWAWEZESHA VIJANA - SAMIA

Vyuo vya amali msingi kuwawezesha vijana - Samia

Na Mwanajuma Abdi
Alhamisi Januari 6, 2011

WAZIRI wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa vituo vya mafunzo ya amali nchini unalenga kuwasaidia na kuwajengea uwezo vijana.

Alisema vyuo hivyo ni msingi wa kuwawezesha vijana ili waweze kujiari na kuajiriwa jambo ambalo litawasaidia kuepukana na ugumu wa maisha.

Alisema hayo jana, wenye ufunguzi kituo cha Elimu ya Amali huko Chwakwani, Wilaya ya Magharibi Unguja, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya Mapinduzi Zanzibar yanayotimiza miaka 47.

Alisema kujenga kwa kituo hicho ni chachu ya maendeleo na kupunguza umasikini kwa wananchi, ambapo inakwenda sambamba na sera za Serikali ya kuwawezesha vijana kupia vituo hivyo kwa ajili ya kujiajiri wenyewe na kuajiriwa.

Alieleza kituo chiho kitaoa mafunzo ya kompyuta, lugha ya kiingereza na ufundi wa magari kwa kuanzia, ambapo alitoa wito kutangazwa zaidi ili vijana waweze kujiunga na kufaidika na matunda hayo.

Waziri Samia alizichukuru taasisi zilizotoa msaada wa ujenzi wa kituo hicho ikiwemo Ujerumani ambayo ilishirikiana na ‘Pamoja Zanzibar’, ambapo jumla ya Euro milioni 47 zilitumika katika kituo hicho ikiwemo vifaa vya kisasa vilivyofungwa.

Hata hivyo, aliwakumbusha wananchi wanakila sababu ya kusherekea Mapinduzi Matukufu 1964, ambayo ndio yaliyowakomboa wananchi na matunda yake yanaonekana.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Shaaban aliwapongeza wahisani hao kupitia Jumuiya ya Pamoja Zanzibar na mashirikiano makubwa baina ya Chuo cha Ufundi na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia katika kufanikisha ujenzi huo, ambao unatokana na sera ya elimu ya kuwajengea uwezo vijana.

Nae Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dk. Guido Herz aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kukubali kujengwa kwa kituo hicho ambacho kitasukuma mbele maendeleo ya kiuchumi na kupambana na umasikini

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa taasisi ya Sayansi na Teknolojia, ambao ndio walenzi wa kituo hicho, Haji Abdulhamid alieleza Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alianzisha Chuo cha Ufundi Mbweni kwa ajili ya kukuza maendeleo kupitia sayansi na teknolojia.

Alisema uwepo wa chuo hicho ni kuziendeleza fikra za kiongozi huyo aliyeasisi Mapinduzi ya Zanzibar miaka 47 iliyopita.

No comments:

Post a Comment