Thursday 6 January 2011

Na Zuhura Mgeni

 Alhamisi  Januari 6, 2011 
JUMLA ya wafanyakazi wanne walioajiriwa kwa mkataba usio rasmi katika skuli ya HIGH VIEW, wameachishwa kazi na kukoseshwa haki zao zote ikiwemo mishahara ya miezi miwili.

Wakizungumza na Zanzibar Leo wafanyakazi hao walisema uongozi wa skuli hiyo umechukua hatua ya kuwafukuza kazi kwa vile walikuwa wanadai haki zao kisheria.

Aidha walifahamisha kuwa mnamo Disemba 2 mwezi uliopita, waliandikia barua kwa uongozi wa skuli hiyo na kudai kupatiwa mishahara, posho la likizo na kupatiwa mikataba rasmi pamoja na kupatiwa vitambulisho vya ZSSF.

Walimu hao walisema wameajiriwa katika skuli hiyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili na tokea kipindi hicho wamekuwa wakikatwa fedha zao mfuko wa hifadhi ya jamii, lakini wanashangazawa kuona hadi kufikia hii leo hawajapatiwa vitambulisho vyao.

“Tumekwenda hadi ZSSF kudai mafao yetu tumeambiwa kuwa hakuna fedha zilizowasilishwa na skuli hiyo hivyo hawawezi kupata haki yoyote”, alisema mmoja wa walimu hao.

Hata hivyo waliongeza kwa kusema kuwa skuli hiyo imekuwa ikiwajiri walimu kwa mikataba isiyo rasmi kwani haipitii katika kamisheni ya kazi na inaishia kwa wakuu wenyewe.

Aidha walieleza kua uongozi wa skuli hiyo umekuwa ukiwanyanyasa wafanyakazi wake na kutowapa fursa ya kujitetea.

Hata hivyo juhudi za kumpata miliki wa Skuli hiyo ili kuweza kujibu madai hayo zimeshindikana kutoka na kuwepo kwa nje ya ofisi na walimu waliyokuwepo Skulini hapo walishindwa kujibu madai hayo.

No comments:

Post a Comment