Tuesday 18 January 2011

FAINI PEKEE HAITOSHI WANAOHARIBU MAZINGIRA

‘Faini pekee haitoshi wanaoharibu mazingira’

Na Abdulla A. Abdulla,

UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini B umeshauriwa kutoa adhabu kali kwa wanaochafua mazingira kwa lengo la kudibiti uchafuzi wa mazingira nchini.

Akiwa katika ziara fupi ya kukagua eneo la ardhi ilioharibiwa kwa kuchimbwa mchanga, bila ya idhini ya Serikali huko Kazole jimbo la Kitope, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alishauri adhabu stahiki zitolewe kwa mujibu wa sheria.

Alisema kwa Mujibu wa Sheria ya Mazingira No 2 ya 1996, muhalifu wa sheria hio anaweza kupewa adhabu ya faini, kifungo, kutaifishwa gari au zote kwa pamoja. Lakini mara nyingi hutolewa adhabu ya faini pekee jambo ambalo husababisha dharau kwani wahusika wanazo fedha nyingi.

Kwa hivyo, bila ya kuingilia maamuzi ya kisheria kwa wanaohukumu kesi hizo alishauri kutoa adhabu nyengine zinazostahiki kama kutaifisha gari ili kuondoa dharau za matajiri wanaovunja sheria kwa maslahi binafsi.

Kuhusu udhibiti mzuri wa eneo husika, Balozi Iddi aliwashauri walinzi kuweka vizuwizi katika njia zao za kienyeji kwa lengo la kuwakamata kwa kushirikiana na vyombo vya Dola.

Naye Sheha wa Shehia ya Kitope Bakari Khamis Simai allisema jitihada zake zimesaidia kubainika kwa uharibifu huo baada ya kushindwa kuwakamata wahusika na kuamua kuiarifu jamii kupitia vyombo vya Habari.

Akieleza jitihad wanazozichukua kukabiliana na wahalifu hao Afisa Mazingira wa Wilaya ya Kaskazini B Daudi Lugoha alisema wanashindwa kuwapata kutokana na kuwa na mtandao wao mkubwa wa kupeana taarifa wakionekana wanawafuatia.

Halikadhalika, Afisa mapato katika halmashauri ya Wilaya hio Ndg Bahati Khamis Hassan alieleza kuwa waliligundua eneo hilo baada ya kuarifiwa na raia wema walioona uharibifu huo na walipokwenda wakawakuta watu na magari matano namba zinahifadhiwa ambao walifanikiwa kukimbia.



Makamu wa Pili wa Rais ambaye ni Mbungea wa Jimbo la Kitope alipata habari za uharibifu huo wa mazingira kupitia taarifa ya habari ya Televisheni ya Zanzibari ya hivi karibuni. Kiasi ya ekari 10 za ardhi yenye rutuba nzuri ya kilimo zimeharibiwa.

No comments:

Post a Comment