Friday 14 January 2011

MAALIM SEIF ASISITIZA UAZISHAJI VIWANDA.

Maalim Seif asisitiza uazishwaji viwanda

Na Abdi Shamnah

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amepongeza juhudi zinazochukuliwa na wananchi, za kuanzisha viwanda vinavyotoa fursa za ajira kwa vijana.

Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa malengo ya serikali katika ya kuwawezesha vijana kujitegemea kupitia kazi za amali.

Makamu wa Kwanza wa Rais, alitoa pongezi hizo jana, wakati alipovitembelea viwanda vya MHANA kiliopo Mtoni na SCANZA Ltd kiliopo Selem Wilaya ya Magharibi, ambavyo hushughulika na utengezeaji wa samani za majumbani, hotelini na ofisini kwa kutumia mbao za mnazi na Mninga kutoka Msumbiji.

Alisema mbali na viwanda hivyo kutoa ajira kwa vijana, lakini pia vina jukumu la kuendeleza juhudi za kutoa taaluma ili vijana wengi zaidi ndani na nje ya Zanzibar waweze kunufaika.

Alisema kazi zinayofanyika katika viwanda hivyo, ikiwemo ya kuwafunza vijana kazi mbali mbali za uchongaji na usanifu ni muhimu kwa vile itawawezesha kufanya kazi popote pale.

Aidha alimtaka Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmeid Mazrui kuangalia uwezekano wa Kampuni ya MHANA kuuziwa jengo wanalolitumia hivi sasa kama walivyoomba kwa kuzingatia ubovu wa jengo hilo linalohitaji matengenezo makubwa.

Alisema iwapo kampuni hiyo italimiliki jengo hilo itaweza kupanua wigo wa shughuli zake na kuainisha kuwa ni vigumu kwa kampuni hiyo kupata maendeleo endelevu wakati inafanya shughuli zake katika jengo la kukodi.

Katika hatua nyingine aliutaka uongozi wa Kampuni ya SCANZA Ltd ambayo hutumia zaidi malighafi ya mnazi katika utengenezaji wa samani, kufanya utafiti wa matumizi ya mbao laini ya mnazi(soft woods) kwa kuunganisha na mbao ngumu (lamination), ili sehemu hiyo isipotee bure.

Aidha alizitaka kampuni zote mbili kujitangaza na kupanua wigo wa masoko yake kuelekea Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nae Meneja wa Kampuni ya MHANA alisema moja ya changamoto inayoikabili Kampuni hiyo ni ulipaji wa VAT, hatua unaozifanya samani wanazotengeza kuwa na bei tofauti ikilinganishwa na samani kama hizo zinazotengenezwa na watu wa kawaida.

Aidha liiiomba Serikali kuuziwa jengo hilo ili waweze kufanyakazi zao kwa upana zaidi na kuchukua vijana wengi zaidi.

Jumla ya vijana wapatao 100 wamepata ajira ya muda katika viwanda hivyo viwili.

No comments:

Post a Comment